webnovel

SURA YA KUMI

Bi. Adimu alikuwa amesimama mlangoni kwa dakika kadhaa akimtazama mumewe kwa mshangao, mumewe alipofikia aliweka begi la nguo zake miguuni kisha akainuka na kumwangalia kwa jicho la kuchukiza.

"Sasa ndiyo umesimama kama sanamu mlangoni na kunikodolea macho kodokodo badala ya kunisaidia," alimkemea mkewe.

"Nikusaidie najua unaenda wapi au ndiyo..."

"Au ndiyo nini," alimkatiza, "sijui nilio nini hiki!"

"Usianze matusi," mkewe alimuonya akimnyoshea kidole, "unanikaripia kwa safari nisiyojua na ukaamua kuondoka bila kunipa taarifa."

"Nikuarifu niendako kama nani?!"

"Mwenzio wa ndoa."

"Ndoa ipi unayozungumzia?!"

Mkewe alisonga nyuma hatua mbili kumpisha, machozi yalianza kumlengalenga machoni, swali aliloulizwa lilifanya akajiona mjinga kuliko watu wote dunia nzima. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka ipitayo ishirini lakini hata swala la kufunga pingu za maisha kihalali au cheti chochote kilichohalalisha kuwepo kwao kama wanandoa hakufikiria.

"Lakini mume wangu unaenda wapi kufanya ufunganye virago namna hii?,"

alimuuliza kwa sauti ya kusinasina.

"Nenda mbali ambako labda hatutaonana tena mbasi wangu," mumewe alimjibu kwa sauti ya chini, akambusu shavuni kisha akaendelea na safari yake kupeleka vitu garini.

"Kwa nini hukunieleza nami nijipange tuondoke sote pamoja!"

"Sasa sina haja ya kukutajia kwa sababu unaona nifanyacho lakini umesimama kuonyesha huna shughuli yoyote, hii ni ithibati kamili kwamba hutaki tuandamane."

"Sasa ningejua vipi bila kuniarifu."

Bw. Vura alipita kama ambaye hakuwa amesikia maneno ya mkewe, Bi. Adimu alisalia mlangoni akitapatapa, alishindwa achukue mkondo upi, aamue kumfuata mumewe bila kujua waendako wala kiini haswa cha safari hiyo au asalie pale nyumbani aishi maisha ya upweke.

Mumewe aliingia garini tayari kuondoka. Bw. Vura alimwangalia mkewe aliyekuwa amesimama mlangoni akimwangalia kwa macho ambayo ni kama yalipasha ujumbe wa kumsihi asiondoke akampungia mkono.

Kabla hajaanza kuondoka, langoni paliingia gari la polisi, akatoka garini kwa haraka na kukimbia mpaka mgongoni pa mkewe.

"Waone hao makafiri wamefika," alimwambia mkewe kwa mnong'ono, "'mi siwapendi kabisa."

Mgongoni aliposimama alitamani kuingia ndani ya rinda la mkewe kujificha lakini akashindwa. Alipiga moyo konde akatoka nyuma ya mkewe na kuenda kukutana na askari waliokuwa mbele yao.

"Karibuni nyumbani," Bi. Adimu aliwakaribisha.

"Asante," Bi. Linda aliitikia mkaribisho.

"Mnaweza kuwa mnahitaji msaada wowote kutoka kwetu au..."

"Hapana dada, tumefika kumchukua mumeo."

Maneno yale yalifanya Bi. Adimu akapigwa na butwa, alimwangalia tena mumewe ambaye ni kama yale mazungumzo hayakumhusu, licha ya kuwa alijua chanzo cha wale askari kufika kwake, alijitia hamnazo.

"Amefanya chochote kibaya?!" Bi. Adimu alimuuliza kwa mashaka.

"Hapana, tunafanya uchunguzi fulani kuhusu kifo cha wajiriwa wake."

Bw. Vura alitoka alipokuwa amesimama akiwasikiliza akamvuta Bi. Linda kando, akambusu shavuni kisha akatoa kibunda cha kama laki tano hivi na kukiweka mikononi mwake. Mkewe alimwangalia kwa mshangao alipokuwa anambusu Linda.

"Tafadhali msamehe," Bi. Adimu aliomba radhi.

"Ungemfunza tabia njema na kuheshimu wanawake," Bi. Linda alimwambia mwenzake akipanguza shavuni.

Hata Bi. Adimu alishindwa kwa tabia mbi za mumewe, Bi. Linda aliachilia kibunda cha pesa alichokuwa amepewa na Bw. Vura kisha wakamchukua na kuondoka. Gari lilipokuwa linaondoka, Bi. Linda alimwangalia mwenzake alivyokuwa anafuta machozi akamsikitikia.

***

"Ndiye huyo anakuja,"

Mmoja kati ya rafiki zake alimwambia akimgusa begani.

Shomari kwa haraka aligeuka kuangalia alikoonyeshwa na sahibu yake. Aliangalia kwa muda bila kushika dira alichoonyeshwa, yule aliyekuwa amemwambia aliendelea kumsisitizia. Mmoja kati ya rafiki zake watano alionekana kusonya.

"Ni muda mrefu hatujaonana naye," Shomari aliwaambia baada ya macho yake kutua juu ya Labibu.

"Labda ni kwa sababu si mtu wa kutumika ovyo na wazazi wake," mmoja kati yao alimwambia.

"Kutoka enzi za shule sijapata kumuona msichana mwenye roho nzuri, mrembo na mkarimu kama yeye," Shomari alimsifia mpenziwe.

"Ni kweli unayosema, kutoka shuleni alionekana kukujali si kidogo."

"Ndo maana nasema ni mkarimu, ni mara nyingi amenisaidia mpaka nyumbani.

"Sijui kwa nini mnamsifia Labibu kama Mungu," aliyeonekana kusonya alitoa hoja yake kwa mara ya kwanza.

"Chanzo cha chuki kati yenu ni kipi? Hakuna siku nikakusikia ukimtaja kwa zuri," mmoja kati yao alimpinga.

Aliyepingwa alimwangalia aliyekuwa amemtaja kwa kijicho kisha akamwangalia Shomari, Labibu alikuwa amekaribia pale walipokuwa wakila gumzo akaanza kutembea mwendo wa paka. Shomari alijipata akim'miminia sifa.

"Ananipenda kutoka moyoni, tena anaogopaga kushare," aliwaambia wenzake kwa sauti iliyomfikia Labibu alipokuwa anapita.

"Unajua vipi. Usisifie kipande cha mti ndani yake mkakasi," aliyekuwa akiwapinga alimwambia akimpa kisogo.

"Amiri, kuna uwezekano wa kusifia tunda ambalo hujatia kinywani?," Shomari alimuuliza.

"La."

"Au ukasifia uzuri wa mji ambao hujauzuru?."

"Huwezi."

"Basi ni hivyo kwa huyu banati tunayemzungumzia, 'mi najua uzuri wake kukuliko kwa Sababu nishamjua kitambo kirefu."

Labibu alikuwa ameenda umbali wa mita thelathini hivi kutoka walipokuwa wanamzungumzia, licha ya kuwa umbali huo alijitahidi kusikiliza maongezi yao kwa sikio moja kama si mawili.

Alipofika kwa njia panda alisimama asijue cha kufanya, alionekana kama mtu ambaye hakuwa na sababu murwa katika matembezi yake. Baada ya kusimama pale kwa dakika kumi, alianza kurudi alikotokea.

Alipoangalia walipokuwa wameketi, aliona wote wamemkodolea macho kama ambao walikuwa wanatafuta kosa. Alitembea himahima hadi pale walipokuwa kisha akasonga kando ya baraste, Shomari aliinuka akaelekea kwake.

"She was among the cutest girls in our school," Labibu alisikia mmoja wao akimsifia.

"Urembo upi ambao hiki kisichana kinao," alimsikia mwingine alimpinga wa kwanza, "angalia miguu ya matege, urembo gani huu unaoweza kutaja mbele ya watu. Mi'ningekuwa Shomari hata singetaka kuonekana naye."

"Angalia ngozi yake ilivyo nyororo na ya kupendeza," sauti ya kwanza ilimsifia.

"Angalia shingo lake, limejaa miviringo kama nyoka."

"Katika utamaduni wetu, hiyo ni ishara ya mtoto kipenzi kwa wazazi wake, si kama mwenzako Rosy mwenye manyama tebweretebwere."

"Umenifika kooni na sasa ni wakati wa kukutapika," Amiri alimwambia mwenzake kwa sauti iliyohamaki.

"Washikaji msigombane, tena sioni haja yenu kubishana," mmoja wao aliingilia kati, "kama wewe ni mpenda chungwa hapana haja ya kuchukia tufaha."

Watatu kati ya wale vijana waliokuwa wakila gumzo waliinuka na kuondoka bila hata kumuaga Amiri aliyesalia pale, walipita karibu na ambapo Labibu na mwenzake walikuwa wakawaaga kisha wakaondoka. Shomari alionekana mtu aliyekuwa anashawishiwa kutenda jambo.

Amiri pale alipokuwa aliwaangalia akamuona Labibu akimvuta mwenzake aliyekuwa anasitasita kisha wakaondoka.

"Huishi kuniliwaza Shomari," Labibu alimwambia mwenzake walipokuwa wanaondoka, "maongezi yenu nilikuwa nayasikiliza, nikaona ulivyokuwa unanivutia kamba."

"Au nilifanya vibaya!" Shomari alimuuliza akisita na kusimama.

"Hapana maabuba wangu, nilipenda ujasiri wako kati yao."

"To love you have to be really courageous than that of Moses when he passed through the red Sea"

Maneno yale yalimfanya Labibu kutabasamu, alijua ni kweli kwa sababu kupenda hakukuwa rahisi jinsi wengi walichukulia. Walitembea mpaka nyumbani kwa wazazi wake Labibu.

Shomari alimuona mbwa mweusi aliyekuwa anabweka kwa nguvu akitishia kukata nyororo. Kuwepo kwake mle ndani ni kama kulimtia wazimu yule mbwa, aliruka akiwa na nia ya kumfikia Shomari lakini akazuiliwa na nyororo iliyokuwa shingoni. Kitendo kile kilimtia uoga Shomari akasonga na kupita mbali.

Kisa hiki kilimtia kicheko mwenzake hata akasahau kwamba alikuwa anamtenda maudhi, mbwa wao pale kwenye nyororo alikuwa akimwangalia kwa macho ya kumkashifu.

"Naona sasa huo ndo ujasiri upitao wa Musa katikati ya bahari ya Shamu," Labibu alimtania akizuia kicheko, "mbweko wa mbwa, wewe huyo ushatundika miguu begani."

"Mbwa si mapenzi," Shomari alijitetea akijitia kicheko cha kulazimisha, "mbwa hajui ushujaa wa mapenzi."

"Ni kweli, kwa muoga huenda kicheko, kwa shujaa huenda kilio."

"Now you are talking sense," Shomari alimuingilia, "si mambo eti natupa miguu karibu kufikia mbingu, 'mi sina ukoo na huyu mbwa wenu."

Labibu alimuongoza mwenzake hadi bustanini kisha akaondoka kuelekea katika kasri lao. Shomari alibaki pale akiyatalii yale manthari kwa macho; miti ya matunda kama vile Tufaha, Tomando na Machenza ilikuwa imepandwa upande mmoja wa jumba hilo na upande mwingine pakajengwa kijumba cha makuti kilichowanufaisha mapumuzikoni, kisha pakajengwa kibwawa kidogo cha samaki kando yake.

Karibu na veranda, aliona maua yaliyotiwa ndani ya mikebe , usoni pa jumba hilo palipandwa nyasi za kizungu mpaka karibu maegesho ya magari.

Karibu na ukuta huo wa matofali uliokuwa umezunguka jumba hilo palipandwa maua yaliyokamilisha uzuri wa mazingira yale, Labibu alirejea kutoka ndani akiwa na bilauri mbili mikononi.

"Karibu nyumbani,"alimkaribisha mwenzake akiwa mwingi wa haya.

"Kabla sijaridhika na mkaribisho wako, nambie kitu cha thamani zaidi unachoweza kumpa umpendaye," Shomari alimuweka njia panda akivuta kiti.

Waliangaliana kwa muda Labibu akiwa ametandaza tabasamu usoni mwake, alishindwa kwa nini mwenzake akamuuliza swali lile, ari ya kutaka kumuuliza kusudi ya swali lile ilimjia akajikaza kiume.

Akilini alikuwa akifikiri vitu vya dhamana kubwakubwa ambavyo vingemfurahisha yeyote, Shomari pale alipoketi alikuwa ametulia akisubiri jawabu kutoka kwa mwenzake. Kimya chao kilivurugwa na mgurumo wa gari uliotokea langoni, Labibu alifunika kinywa kwa uoga.

"Wamerejea, sio!" Shomari alimuuliza kwa utulivu, alimwangalia mwenzake alivyokuwa anatapatapa kitini akatabasamu.

"Ndiyo, wamerejea," Labibu alimjibu kwa wasiwasi, "wamerudi haraka kuliko nilivyotarajia."

"Hakuna haja ya wasiwasi, watatuelewa...tu...hatukuwa tunafanya chochote cha kukera."

"Wee...labda mama, lakini baba ni simba," Labibu alitia shaka.

Wakiwa bado katika mazungumzo yao, walimuona Bi. Tabasuri akifungfua lango kisha gari likaingia mpaka maegeshoni. Pale alipokuwa ameketi, moyo ulidunda kwa nguvu, alimwangalia Shomari kwa mshangao kwa sababu kwake mambo yalionekana shwari kabisa.

"Shikamoo," alimsikia mwenzake akisalimu na kuinuka pale alipokuwa ameka. Hakuwa ametambua kuwepo kwa babake pale.

"Sina haja na shikamoo zako, ushaziona mwenyewe," Bw. Nadama alinguruma, "we nani?."

"Naitwa Shomari."

"Unafanya nini kwangu."

"Nilikuja kuongea na La..."

"Wakati wazazi wake hawapo!" Bw. Nadama aliuliza kwa kufoka, kisha akamuashiria atoke kwa kidole.

"Lakini baba u..."

"Lakini ya nini?! Ukitaka kuzungumza naye, mfuate huko nje. So ndani ya majengo haya."

Shomari alimtazama Labibu kisha akaondoka kwa utaratibu, Labibu alisalia amefura kwa hasira. Alitamani kuondoka pale alipokuwa amesimama amfuate mpenziwe lakini akashindwa.

"Now I can see why you were behaving so weirdly in school," babake alimwambia, "na mamake yuko tu pale hashughuliki na mwanawe, sijui nitakuita chongo a kengeza. Unayaona maasi yangu ila ya mwanao unayafumbia macho."

Aliondoka akamuacha mwanawe analia pale bustanini, Bi. Tabasuri alipoona mumewe ameondoka, alitoka akaenda na kuketi mkabala na mwanawe.

"Ah! Mwanangu, tabia gani hii unayoonyesha mbele ya wazazi wako?!" Mamake alimuuliza kwa sauti ya chini, "kuleta waume mpaka chini ya paa la babako, huna hata haya."

"Lakini mama huyo mvulana ni mtu mzuri, si mnavuomdhania, baba hakumpa hata wakati wa k..."

"We...we...we! Usijaribu kumtetea," mamake alimuonya, "si' tulifunzwa kuwaogopa wanaume kama sumu."

Labibu aliinua uso wake na kumwangalia mamake kisha akaondoka, mamake alisalia pale bustanini akimwangalia mpaka alipoingia ndani ya nyumba.