webnovel

SURA YA TISA

Mle ofisini Bw. Siga alikuwa akimwangalia mwenzake kama ambaye hakuamini alipokumbuka walichokusudia kumtenda Bw. Nadama usiku uliopita. Macho ya Bw. Vura yalikuwa yenye ubaridi, yalifanya aonekane kama muuaji aliyebobea katika kutekeleza mauaji. Wekundu wa macho yake ulimuogofya mwenzake.

"Unafikiri atanyamazia kisa cha jana ama atatuandama?," Bw. Siga alimuuliza kwa hofu.

"Hata akituandama hana ithibati yoyote kuonyesha sisi ni wahusika."

Ndani ya moyo wake hasira ilikuwa ikimenyana na nafsi yake kwa nguvu zaidi, japo alijaribu kujizuia kuonyesha hisia zake kamili, mwenzake alizisoma kutoka usoni pake. Makunyanzi yalikuwa yametoka kipajini.

"Nani aliyemfunulia ukweli kuhusu mpango huu kufanya akwepe hii dakika ya mwisho...hata nilikuwa nimeahidiwa," Bw. Vura aliwazia. Mwenzake alikuwa amebaki akimwangalia kwa mshangao.

"Sir! Are you alright...," Bw. Siga alikatizwa kwa mlango uliofunguliwa kwa fujo kisha bawabu akasimama mbele yao.

Bw. Vura alimwangalia mwenzake kwa mshangao kama aliyetarajia neno kutoka kwake.

"Is everything ok!" Bw. Siga alimuuliza kwa wasiwasi.

"Unaitwa nje," mlinzi alimpa taarifa.

"Na nani?."

"Afisa wa polisi sir!"

Bw. Siga alipoketi alinywea kitini akamtazama mwenzake kwa macho ya uoga, naye Bw. Vura aliingiwa na wasiwasi mara moja baada ya kusikia kwamba askari walikuwa walimkuwa mle ndani wakitaka mdogo wake.

"Wanamtaka kwa zuri au baya?," Bw. Vura alimuuliza akiwa amemwangalia kwa macho ya kumushutumu, "na nani aliyewaruhusu kuingia humu!"

"Labda sir wanataka kumhoji kuhusu kujitia kitanzi kwa Arina."

"Arina 'kajitia kitanzi?!" Bw. Siga alijiuliza, mikono yake ilikuwa imefunika kinywa kama aliyekuwa anajizua kusema maneno fulani.

"Nani akawafahamisha askari hata kabla ya kunijuza hayo! Na kwa sasa wanafanya nini?."

"Wanainyongoa maiti kutoka kitanzini sir!"

"Hawana waranti yoyote inayowaruhusu kukuuliza maswali, huyo aliona heri ajingonge kuondokea matatizo ya dunia, 'sa kinyongo chake kinakuhusuni! Nakushauri usiende popote, baki mumu humu," Bw. Vura alimwambia Bw. Siga akimwashiria bawabu aondoke kwa kidole.

"Wako kwa kazi yao bwana wee, nikiwazuia kunihoji wataona naficha ukweli fulani."

Bw. Siga alipoketi alikuwa amemwangalia mwenzake kama ambaye angemtolea suluhu ya matatizo yake, alikuwa anajaribu kuvuta kumbukizi zake kukumbuka kilichosababisha kujitia kitanzi kwa Arina lakini ikawa kizungumkuti kwake. Pale ambapo mwenzake alikuwa, dira yake ilikuwa isharudi nyuma miezi kadha akatambua kilichosababisha Arina kujiangamiza na kwa wakati huo pale alipokuwa ameketi alikuwa anapanga atakavyopata upenyu aondokew mtego uliokuwa karibu kumnasa.

"Mi' sijui wala sihusiki kwa chochote watakachokuuliza," Bw. Vura alimwambia akiinuka tayari kuondoka, alipofikia komeo alisita akageuka na kumwangalia mwenzake, "ulishindwa kuepuka donda, sasa ni wakati wa kukabili kovu."

Baada ya kumwambia maneno yale, Bw. Vura aliondoka mle ofisini akamuacha amezika kichwa katikati ya mikono yake. Msemo aliombiwa ulizua shauku ndani yake ya kutaka kujua kilichomaniashwa, baada ya kufika maegeshoni Bw. Vura aliondoka muondoko wa kinyonga asitake hata kuonekana hata kwa wafanyakazi wake. Ofisini, Bw. Siga alisalia akitapatapa, alijaribu kushika kalamu lakini ikamtoroka mkononi.

"Hodi," alisikia sauti ya kike mlangoni pake.

"Karibu ndani," aliitikia kwa sauti ya mashaka.

Mlango ulifunguka kisha kijana wa kike mwenye umri wa kama miaka ishirini na minane hivi akasimama mbele yake, urefu wake ulikuwa futi tano na inchi kadhaa. Alivalia suti ya samawati na kitambaa cha rangi ya zambarau shingoni. Tabasamu ilikuwa imeng'aa kwenye uso wake wa rangi ya dhahabu iliyokolea. Bw. Siga alimwangalia kwa uoga, akatoa kitambaa mfukoni na kufuta jasho, hofu ilikuwa imemzidia baada ya yule kijana kusimama mbele yake.

"Have a seat and feel free," alimkaribisha mgeni wake.

"Asante," yule mwanadada alimshukuru akivuta kiti katibu yake.

"Naitwa Bw. Siga, meneja wa kampuni hii."

"Nimefurahi kukufahamu," yule mwanadada alimwambia akimpokeza mkono kwa salamu, "nami naitwa inspekta Linda, kutoka kituo cha polisi cha Mladi."

Bw. Siga aliachilia mkono wake kwa haraka baada ya kusikia cheo chake, akainuka na kufungua dirisha lililokuwa limefungwa. Alisimama dirishani kupoteza wakati, alikuwa hata ameogopa kurudi kitini. Bi. Linda alimwangalia akaona kijasho kinamtiririka usoni.

"Sir, am here to ask you a few questions concerning the death of one of you employees," Bi. Linda alimuomba kwa utulivu.

"Kifo chake hakinihusu ndewe wala sikio," alijibu kwa jeuri kutoka pale dirishani, "alivyojinyonga, mngeacha akajinyongoa mwenyewe."

"Bw. Siga, ni heri urahisishe kazi yangu nay'o iwe salama, yafaa uwajali wenzako na kujua kila linaloweza."

Bw. Siga alimtazama Bi. Linda kutoka pale dirishani akaona tabasamu aliyokuwa nayo ikiwa imeyeyuka na likabaki juso lenye hamaki.

"Bi. Linda tafadhali, sina mwanga kuhusu chochote kilichokuwa kinaendelea...eeh...naomba unielewe."

"Mkurugenzi wako yuko wapi?."

"Sijui mkubwa."

"Usinitie pilipili machoni," Bi. Linda alimtahadharisha, "nafikiri tukimpata tutapata taarifa fulani. Niambie chochote unachojua, mwenyewe nitaendeleza uchunguzi wangu kutokea hapo."

Bw. Siga alishawishika kumwambia Bi. Linda kuanzia mwanzo mpaka kifo cha Arina. Alirudi akaketi na kuvuta nje mtoto wa meza tayari kutoa faili aliyokuwa ameficha baada ya kulishwa kadhongo na mwenzake, Bi. Linda alimwangalia kwa makini.

Bw. Siga alipoinua uso wake na kumwangalia tena mwenzake alibadili nia akaisukuma ndani kwa haraka, Bi. Linda alimwangalia akatabasamu, tabasamu la hamaki.

"Sina chochote kuhusiana na kifo chake," Bw. Siga alimwambia akifungulia kiyoyozi kilichokuwa kando yake.

"Heri mahojiano yetu yabadili manthari yake," Bi. Linda alimwambia akiinuka tayari kuondoka, "boys, get him and let's be gone."

Hata kabla Bi. Linda hajamalizia maneno yake, afisa wawili walikuwa washaingia na kumtia pingu. Hapo ndipo alipoanza kutoa machozi, alitaka kumuita inspekta kumweleza mawili kama si matatu akashindwa.

"Hapana haja y kumkamata mamba kinywa kwa niaba ya mwenzako," Bi. Linda alimwambia akimgeukia, "una hakika utamshika kwa muda gani kabla hajakugeukia na kukumaliza."

Bw. Siga alijua kwamba mwenzake alimwambia ukweli aliokuwa anaogopa, alisukumwa ndani ya gari la polisi kisha wakaondoka. Wafanyakazi walikuwa wameuzingira mwili wa mwenzao wakiomboleza, gari la hospitali lilifika maiti ikachukuliwa na kupelekwa chumba cha kuhifadhi maiti.

***

Bw. Nadama alifika kazini kwake mwendo wa saa tatu kasorobo, hakuwa amevalia mavazi rasmi ya ofisi, labda hakuwa tayari kwa kazi. Gloria kwenye masjala alipomuona kwa mara ya kwanza hakumtambua kwa sababu alionekana mdogo wa umri.

"Welcome sir!" Gloria alimkatiza alipoina anapita bila hata kumsalimu.

Bw. Nadama alipita bila kusema lolote hata baada ya kukaribishishwa na mhazili wake, Gloria alibaki pale amezuba. Alishangazwa kwa tabia za mwajiri wake, lakini akafikiri labda ni kwa sababu ya uchovu wa safari.

Baada ya nusu saa, Gloria alipanda vidato kuelekea katika ofisi ya mkuu wake akijua ashatulia, alipofika mlangoni alibisha lakini hakujibiwa.

"Ni salama kweli! Au kuna matatizo?," Gloria alimuuliza akifungua mlango kuingia ndani.

"Ni salama mke wangu, usitie shaka. Mumeo yuko salama," Bw. Nadama alimtania.

"Nimefurahi kusikia hayo, hata mwenzangu kule nyumbani yu heri!" Gloria alimuuliza akitaraji kusikia habari zaidi kutoka kwake lakini alikuwa kimya. Gloria alishindwa kumuelewa, kimya chake hakikuwa cha kawaida, alijua labda yaliyozagaa akilini mwake hayakuwa mepesi ya kuzungumzia.

"Umepanga vipi kuhusu ziara yetu ulokuwa umeniahidi?," Gloria alimuuliza baada ya fikra za ziara kumpitia akilini.

Pale alipoketi alikuwa kama sanamu, hakutikisika wala hakusema lolote na mwenzake. Gloria alianza kukusanya pamoja makaratasi yaliyokuwa yamekaa ovyo mezani, aliona labda kabla ya mjo wake, mwenzake alikuwa akitafuta karatasi fulani.

Baada ya kufanya usafi pale mezani, aliinuka tayari kuondoka kumpa muda zaidi wa kupumzika.

"Please sit down," Bw. Nadama alimuomba alipoona anaondoka.

Gloria alirudi akaketi tayari kusikiliza aliyokuwa anaenda kuambiwa. Bw. Nadama alimtazama mhazili wake hata akahisi aibu kuhusu yale aliyotaka kumwambia, alijaribu kufungua kinywa kutamka aliyotaka lakini kinywa kikawa jangwa la maneno.

"Sir! Am back," Gloria alimwambia kwa sauti nyororo yenye utulivu fulani.

"He nearly killed me at 11pm with my family," Bw. Nadama alimwambia aliyokuwa ameweka kwenye sakafu ya moyo wake.

Gloria alishtuka kwa taarifa aliyopewa, alihisi mwenzake anamchezea shere. Maneno yale yalimfanya akashindwa kumuelewa hata zaidi, kutoka alipoingia, neno la tano kutoka kinywani mwake lilihusu mauaji. Alimwangalia kwa mara nyingine akatoa tabasamu hafifu usoni, alitarajia kumuona mwenzake vivyo hivyo lakini uso ukawa umekauka kama mwamba.

"Karibu uuwawe na nani?," Gloria alimuuliza, "utani wa aina hiyo si mzuri."

"Si utani, kwani we ni bibi au shemeji yangu ndo nikutanie!" Bw. Nadama alimuuliza, "kwa sasa ningekuwa nishaongezewa jina la marehemu."

"Lakini nani?."

"Vura."

"You must be joking," Gloria alimwambia katikati ya kicheko, "your very best friend."

"Ukiniangalia hivi unaona nakufanyia masihara sio!" Bw. Nadama alimuuliza kwa hasira.

"Kwa nini ajaribu kukuangamiza?!"

"Nd'o maana nimekwambia ufikiri nami, mke wangu wa nyumbani naona hanifai kwa lolote."

"Si vyema kumchukua mkeo kama zulia la mlangoni."

Gloria alianza kuzungukwa na kichwa kwa sababu ya habari aliyopewa na mwenzake, aliwaza na kuwazua akijaribu kufikiri kinachoweza kuzua ugomvi kati ya hao marafiki wawili akashindwa. Ni kama mwenzake alikuwa ashamwambukiza ugonjwa wa mafikirio ya kila wakati.

"Ajenti wa kampuni hiyo ashapiga tena simu?," Bw. Nadama alimuuliza.

"Ndiyo, alipiga siku iyo hiyo lakini nikamwambia kwamba hatutaki mkataba wao, alipopiga kwa mara nyingine nilisusia."

Bw. Nadama alitikisa kichwa kwa utaratibu kama aliyegundua kitu fulani, Gloria alimwangalia kwa mshangao.

"Naenda kumuona Bw. Vura sasa hivi," alimwambia taarishi wake.

"Lakini itakuwa hatari, kama alitaka kukuangamiza basi kwa himaya yake itakuwa rahisi kukutenda baya," Gloria alimtahadharisha.

Mwenzake alimtupia jicho la shauku, akachukua koti lake kitini na kuondoka.

***

Bi. Tabasuri baada ya kukamilisha shughuli zake za hapa na pale, alienda mpaka sebuleni akaketi kando ya mumewe. Mwenzake hakuwa ametambua uwepo wake. Mkewe alitaka kuanzisha mazungumzo akashindwa, aliona mumewe akiwa katika mazingira mengine tofauti kabisa kiakili.

"Hakuna haja ya kujitia mawazo kwa yaliyopita madaam uko hai," mkewe alimshauri akiondoa chupa ya soda iliyokuwa mezani.

"Niko sawa kabisa mke wangu, kwanza binti yangu yuko wapi? Kutoka saa tano sijapata kumtupia jicho juyo dhahabu ya moyo wangu."

"Una hakika kabisa!"

"Ndiyo."

"Yule pale bustanini anafuma kitambaa."

Bw. Nadama aliinuka akachungulia dirishani kuhakikisha alichoambiwa na mkewe. Alipomuona amezama kiakili kwa kile alichokuwa anafanya aliridhika.

"We have a great daughter," alimwambia mkewe.

"Sure."

"Si bure nikakwambia haya, ninapomwangalia naona kipaji fulani. Tokea kisa hicho kilipotokea, alinionekania katika muonekano mpya na ikawa kama siku mpya katika maisha yangu."

Mkewe alimwangalia akaona tabia yake dhidi ya bintiye kutoka walipovamiwa ikiwa imebadilika. Kumkaripia alikokuwa amezoea hakusikia tena pale nyumbani kwao. Alipokuwa anaangaza macho yake mle chumbani, alivutiwa na picha waliyopigwa wakiwa maharusi, akaona mkufu uliokuwa shingoni.

Kwa kuona mkufu ule, alianza kukumbuka siku ambayo mumewe alifika na wavyele wake kumpa posa. Ilikuwa siku ya Jumatano asubuhi mwendo wa saa tatu mumewe alipofika akiandamana na wazazi wake. Wazee wake walikuwa wamevalia suti za vitenge kila mmoja, naye mumewe akawa na kaptura. Walivyoleta mara moja viliwekwa mbele ya wazee waliowapata barazani, ilikuwa mihogo mitano, mbuzi wawili weusi wa kike na kibuyu cha maziwa.

Baada ya mazungumzo kati yao, aliitwa naye akaingia akiwa mwingi wa haya, alikuwa amefunga khanga iliyofika mapajani na nyingine iliyofungwa kifuani. Nadama alimkazia macho mpaka alipogongwa kisogoni na babake. Waliangaliana kwa macho ya chinichini kila mmoja akimuogopa mwenzake, kwa amri ya babake aliondoka akawaacha wakiendelea na maongezi.

Aliwaona wazee wake wakitoka nje na kuanza kunong'onezana kando ya baraza hilo.

"Naona heri mjukuu wangu Tabasuri asioleke kwake," alimsikia babu yake akimwambia babake.

"Ah! Mume wangu," alimsikia bibiye akipinga mumewe.

"We mwanamke, hebu kuwa kimya mbele yangu, wanawake siku zote ni kama watoto wadogo," babuye alimkaripia, "kile ambacho mzee kama mimi naona kikiwa umbali wa maili hamsini hata kiwe mita tano kijana hawezi kuona. Tabasuri mjukuu wangu ambaye bado damu ya ujana inamuenda mbio ndani ya mishipa yake hatakubaliana nami."

Walizungumza kwa toni za chini kisha kila mmoja akaingia ndani wakiwa wamefikia maridhiano isipokuwa babuye aliyeingia ndani akitikisa kichwa kama ambaye hakuwa amekubaliana na uamuzi wao. Waliingia kisha babake akamuagizia, baada ya kuingia palipokuwa na mkutano aliagizwa akarudi na chungu kilichojaa gongo. Wale wazee walianda sherehe ndogo kisha wakawaaga wageni wao kwa furaha.