webnovel

SURA YA PILI

Baada ya miaka saba Athalia akahitimu darasa la saba, na akafanya vizuri sana kwenye masomo yake mbali na kwamba mwaka huo huo aliondokewa na kaka yake mpendwa Christopher ambaye alimwachia ziwa. Athalia alijaliwa kuona mbali hivyo alihakikisha kwamba ndoto yake, siku moja inatimia. Alifanya kazi mbalimbali kama kuuza maembe, mboga za majani, viazi mviringo, mahindi na kadhalika sokoni. Alifanya vibarua vya kupalilia mashamba ya watu ili mradi apate pesa za kununulia vifaa vya shule. Alilima maharagwe hata alipovuna pesa zake alizielekeza katika taaluma yake. Mwaka uliofuata alijiunga na shule ya sekondari ya Malengo. Hapo alisoma miaka mitatu yaani kidato cha kwanza hadi cha tatu kisha akahama kufuatia vurugu zilizokuwa zikiendelea shuleni hapo. Mwaka wa nne alijiunga na shule ya sekondari moja ya Mwendelezo iliyoko mkoani Mtamani. Hapo alimaliza kidato cha nne.

Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri wa Athalia kuitimiza ndoto yake. Hakika Mungu si Hitla kwani alimtendea Athalia kadri ya sala zake kwake. Matokeo yakatoka ya kidato cha nne, haya yalifunua ukurasa mpya katika familia ya bwana Daniel Abija. Binti yao Athalia alifuzu vizuri kwa alama za daraja la tatu na akachaguliwa kuendelea na kidato cha tano. Athalia alifurahi sana kuona kwamba ndoto yake inakwenda kutimia haijalishi ni lini atakuwa profesa. Aliamini mafanikio hayaji kwa mkupuo bali ni hatua moja baada ya nyingine kama mtoto azaliwavyo, hukaa, hutambaa, husimama kisha akatembea. Katika hatua hii Athalia alijiona ameanza kutambaa katika maisha yake ya kindoto ambayo siku moja yatakuwa kweli. Mwaka uliofuata alijiunga kidato cha tano katika shule ya sekondari ya Maendeleo.

  Hoshea alimwandalia mdogo wake mahitaji ya shule akiwa mkoani Mtamani wakati mdogo wake Jeremia alimwandalia nauli Athalia ya kumfikisha shuleni Maendeleo. Shule hii iko mkoani Usicheze. Athalia aliondoka asubuhi sana nyumbani kwao, akapanda basi kutoka wilayani Chanua hadi kufika shuleni Maendeleo. Wilaya ya Chanua inasifika kwa kuwa na chakula kingi na ukijani wa kutosha mwaka mzima. Wakazi wa wilaya hii mwaka mzima wanalima mazao mbalimbali kama ndizi, viazi mviringo, viazi vitamu, maharagwe, karanga, magimbi, matunda ya kila namna na kadhalika. Huko ndiko atokako Athalia kwenye neema ya chakula.

Athalia alikuwa si mwenyeji wa mkoa wa Usicheze. Akiwa katika basi la Ayubu la kutoka wilani Tulia mkoani Matamvua ulioko mpakani mwa nchi ya Sikomo hadi Highway alikuwa akijiuliza nitafikaje shuleni Maendeleo. Lakini kwa utashi wake mkuu alizikumbuka nasaha za baba yake na maelezo yake. Saa kumi ya jioni alifika stand ya Hapa Kwetu mkoani Usicheze. Hapo alipanda gari la Loveness na kushika njia ya kwenda Maendeleo. Saa kumi na mbili za jioni aliwasili Maendeleo, hapo alimkuta makamu mkuu wa shule bwana Suleman. Athalia alipokelewa vizuri na makamu mkuu wa shule kisha akapelekwa kwa mwalimu wa bweni. Athalia alipofika bwenini alihisi yuko katika nchi ya ugeni. Alikuwa hajawahi kuishi mbali na ama na wazazi au ndugu zake, lakini sasa hana budi kuachana na ndugu zake kwani siku zote mtaka cha uvunguni sharti ainame. Wakati huo wote Athalia hakujua aanzie wapi maisha ya upweke, lakini kwa kudra za Mola alikutana na binti mmoja aitwaye Hilda.  Huyu akawa rafiki mkuu na mfariji wa Athalia. Hilda yeye amewahi kusoma shule ya bweni huko kwao Parani hivyo ana uzoefu wa maisha ya jela ya shule za bweni. Hilda alimfundisha rafiki yake Athalia maisha yalivyo ya bweni na jinsi ya kuishi.

Hilda ni mrefu wa wastani, ana sura ndefu, mweusi, mwembamba na mrembo, ana hekima katika kuongea lakini ni mkali kama mbogo ukimkorofisha. Binti huyu alijulikana kwa jina la utani black beauty. Hilda alipenda sana shule lakini masomo ya kidato cha tano na cha sita yalikuwa kiboko yake. Somo la Historia lililofundishwa na mwalimu Study well, lilikuwa tishio katika maisha yake. Siku moja alipokuwa ameketi dekani alimwita Athalia na kuanza kumweleza yanayousibu mtima wake. "Athalia unajua somo la Historia ni gumu sana kuliko hata somo la Kiingereza moja" alisema Hilda. Athalia akamjibu "usikate tamaa Hilda, tutaweza tu! Kwani kila mwanzo huwa mgumu sana lakini, mwisho wake huwa ni mzuri unapoanza kuona mafanikio. "Hilda alikubaliana na usemi wa Athalia na mara kengele ya kuashiria saa ya chakula ikagongwa.

Athalia na Hilda wakachukua sahani zao na kwenda kupanga foleni mithili ya wapiga kura ili kupata ugali na maharagwe. Baada ya chakula walirudi bwenini na kuanza kujisomea somo la Historia mbili, wakajisomea hadi majira ya saa kumi na mbili jioni tayari kwa msosi wa usiku. Kama samaki baharini walivyo na pilika pilika, basi wanafunzi wa bweni nao wana pilika pilika haziwaishi mara sehemu ya chakula kupata chakula, mara kusafisha meza sehemu ya kulia chakula. Wengine wako busy na vitabu madamu tu anafanya kazi. Usiku ndo kivumbi na jasho wengine waliozaliwa na wazazi wao wako busy kujisomea ama kujisomea mmojammoja au kwa majadiliano. Watoto wenye roho za kishetani ndio wakati wa kujirusha kwenye kumbi za starehe. Wakirejea bwenini utasikia leo dance lilikuwa la kukata na shoka. Wazazi wahurumieni walimu wa bweni kwani wana vita ambavyo hawajui silaha azitumiazo adui wao. Lakini Athalia na rafiki yake Hilda wao wanajali nini kilichowapeleka shule. Wakati wa usiku wao huungana na wenzao akina Pamela, Jesca, Rahma, Adela, Tuuli, na Jackline kujisomea huku wakifuata ratiba yao waliojipangia.

Ama kweli hakuna vya bwerere duniani, kwani wakati mwingine Athalia alikuwa akiamka saa tisa usiku kujisomea lengo kuu ni kuitimiza ndoto yake. Athalia alikuwa mzuri sana katika somo la Kiswahili moja na mbili, Kiingereza moja pamoja na Historia mbili. Mwiba wake mkubwa ulikuwa katika somo la Kiingereza mbili (fasihi ya Kiingereza) na Historia moja. Hata hivyo alijivika uso wa gumegume ili kupambana na dhoruba ya masomo hayo.  Mwili na akili kwa pamoja vilishangilia mithili ya maji mengi. Athalia alikuwa mchwa atengenezaye nyumba yake kwa mate, Athalia alisoma kwa bidii hata kama masomo ni magumu kiasi gani. Athalia aliamini kuwa chini ya jua hakuna lisilowezekana, kinachotakiwa ni kugangamala kama nyangumi baharini anapotafuta chakula. Kila alipofanya mitihani yake alifaulu vizuri sana hadi walimu wakajua wana hazina ya taifa la kesho.

Mitihani ilipoisha Athalia alirejea nyumbani kwao kwa ajili ya likizo. Kama ilivyo ada yake ya uchapakazi, Athalia alifika nyumbani na kuanza kazi za shamba. Alilima viazi mviringo kwa bidii, akapalilia, hata wakati wa mavuno alikuwa amesharudi shuleni tayari. Lakini mama yake aitwaye Sarah hakuchelea, mara tu baada ya mavuno alimtumia mtoto wake fedha kwa njia ya posta. Athalia kwa uaminifu wake alizitunza pesa hizo hata alipopata tatizo la ugonjwa ndipo alipotumia elfu tano. Athalia aliumwa malaria na typhoid alipokuwa shuleni Maendeleo, kwani wahenga walisema "mazoea yana taabu yake" yeye alizoea kunywa maji yaliyochemshwa sasa huko shule mara wanywe maji ambayo hayajachemshwa, mara icecream zisizo salama, vitu hivi vilimletea madhara katika tumbo lake. Kutokana na maradhi hayo alilazimika kulazwa hospitali ya mkoa ya Usicheze kwa matibabu. Rafiki yake Rebeka alimuuguza hata aliporuhusiwa. Rebeka alikuwa bega kwa bega na Athalia, alihakikisha kwamba Athalia anarejea katika hali yake ya kawaida, alimhimiza kula matunda kwa wingi na chakula bila kusahau maji mengi kama ilivyoshauriwa na daktari. Ashukuriwe Mungu Athalia akarejea katika hali ya uzima tena, hivyo akarejea darasani na kuendelea na masomo yake pamoja na huduma yake ya ukatibu ya chama chao cha GALEFEMA (God's Assembly of Learners Fellowship Mafanikio). Pesa zake zilizokuwa zimebaki katika matibabu aliamua kununulia vitabu vya masomo yake ili aweze kufanikisha azma yake.

Athalia katika maisha yake yote anapenda sana kuabudu, alipokuwa shule ya msingi alikuwa hakosi kwenye shule ya Jumapili ya watoto (Sunday school) na alikuwa mwimbaji mzuri wa kwaya ya watoto. Alipofika darasa la saba hadi kidato cha tatu mwanzoni mwa mwaka Athalia alibadilika kabisa, aliacha kwenda kanisani, alikuwa anashinda nyumbani siku za jumapili. Athalia alikuwa na pilika za kuimba taarab, maaskini alizama kabisa katika taarab kama mzaliwa wa pwani. Lakini cha ajabu ni kimoja kwamba mbali na kuimba nyimbo za taarab na kucheza muziki, alikuwa akifunga. Hili lilipelekea dada yake Hana kumhubiria kila wakati na kumwambia funga yako haina maana wala nyimbo zako hazina utukufu mbele za Mungu. Hivyo ni bora tu akaokoka ili uimbaji na funga zake zimfikie Mungu. Haya yote yalikuwa ubatili mtupu kwa Athalia, akaendelea na mbwembwe zake.

Siku moja akiwa kidato cha tatu mnamo mwezi Agosti alimwandikia barua kaka yake mkubwa Hoshea wa mkoani Mtamani akiomba atumiwe ada, huku dada yake Rehema akiwa huko huko. Barua iliwasili siku moja kabla ya dada yake Rehema kung'oa nanga mkoani Mtamani. Hoshea alimkabidhi Rehema pesa na kumwagiza aende moja kwa moja nyumbani kwao Chanua badala ya kufikia nyumbani kwake mjini Matamvua. Rehema alifanya kama alivyoagizwa sawia na utamaduni wa jamii ya Wanyacha ambao kaka mkubwa anaheshimiwa kama baba mzazi.  Siku hiyo hiyo Rehema aliwasili mjini Chanua na kuwakuta akina Athalia. Kitu cha kwanza ilikuwa ni kukabidhi pesa kwa Athalia zilizotumwa na kaka yao Hoshea.

Athalia alipozipokea pesa hizo aliomboleza sana na kujua kuwa Mungu yupo na anaweza kufanya mambo yasiyowezekana kwa binadamu wa kawaida. Huu ulikuwa mwanzo wa Athalia kumpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa Maisha yake. Athalia aliendelea na wokovu huku akisoma kwa bidii sana kwani aliamini kuwa "Kumcha Mungu ni Chanzo cha Maarifa." Athalia anaamini kuwa kila aliye na akili amepewa na Mungu kwa sababu asili ya akili na ubongo ajuaye ni Muumba pekee. Hivyo ndiyo imani ya Athalia ilivyo.

Baada ya kuokoka Athalia alijiunga na chama cha wanafunzi waliookoka shuleni kiitwacho GALEFEMA (God's Assembly learners' Fellowship Mafanikio). Athalia alikuwa akiwahubiri wenzake neno la Mungu na ndiyo sababu akapendwa sana na walimu pamoja na mkuu wa shule. Alipokuwa kidato cha tano alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa GALEFEMA tawi la shule ya Maendeleo. Wakati wa kipindi cha Pasaka alichaguliwa kuwa katibu wa GALEFEMA mkoa wa Usicheze. Athalia kwa sababu alikuwa anampenda Mungu alifanya kazi kwa bidii za GALEFEMA na hakuacha kusoma kwa bidii. Athalia alikuwa akizunguka kama pia, mara Mapinduzi sekondari, Heri sekondari, Pema sekondari, Kioo cha Jamii sekondari na kadhalika za mkoa wa Usicheze.

Katika kufanya kazi zake za kiutumishi na za shule ilifika wakati wenzake walimwona mjinga asiye na akili hata rafiki yake wa karibu Hilda, walimcheka na kumkejeli wakisema "eeehee! Sijui akifeli mitihani kwao atasema alikuja kwa ajili ya GALEFEMA, maana kila siku yuko busy na mambo ya Mungu utafikiri ni mtakatifu sana kuliko wengine". Haya Athalia aliyanyaka kwa masikio yake mwenyewe, na wala hakujali aliendelea na time zake. Alichoamini yeye ni kwamba kusoma anasoma na Mungu anamtumikia.

Katika shule ya Maendeleo walikuwa na mitihani ya kila wiki na huko ndiko mtego wa Athalia ulikowekwa. Mkuu wa shule hiyo alimshutumu Athalia kwa madai kuwa aliwabadilisha wanafunzi wake imani zao kwa sababu tu Athalia alikuwa akiwahubiri neno la Mungu, na kuwaombea wanafunzi wenzake ambao baadhi yao waliamua kujiunga dhehebu analoabudu Athalia. Ama kweli usilolijua usiku wa giza, kwani Mkuu wa shule alikuwa gizani, hakujua kuwa Athalia alikuwa kinga kwa wanafunzi wenzake wa bweni kwa sala na maombi yake akiwa na kikundi cha maombi.

Wakati wa likizo siku moja iliripotiwa kuwa wanafunzi waliokuwa wakifanya usafi mabwenini waliona mtoto mdogo akitambaa bwenini lakini walipofungua na kuingia ndani hawakuona kitu. Hali hii ilileta wasiwasi, mwalimu aliyehusika na wanafunzi wa bweni alitoa kauli mbiu kwa wanafunzi "walokole tunaomba maombi iwe ni kaida katika eneo hili la mabweni ili kuwe na usalama." Hili lilikaririwa akilini mwa wanafunzi wa bweni. Hivyo wanafunzi waliookoka walijenga desturi ya kuomba na kuombea wanafunzi wote na jamii ya shule yao kila wakati.

Siku moja Athalia akiwa kidato cha sita akijiandaa na mitihani ya Jumamosi, akiwa bweni A, aliona wanafunzi wawili wa kidato cha kwanza na pili wakija kwa kasi na walipofika usawa wake walimwambia Athalia kuwa anaitwa bweni C. Athalia ni mbishi aliwauliza kwani kuna nini, wakajibu wamesema ufanye haraka kuna tatizo limetokea. Athalia aliwaambia msiponiambia kilichotokea siendi, wale wanafunzi wakamjibu kuwa kuna wanafunzi wawili hawawezi kupumua hivyo msaada wa maombezi unahitajika. Athalia akaridhia akang'oa nanga na kuongozana nao wakatia timu bweni C. Huko akamkuta Israel akisubiri dakika itimie achukue roho zake. Bila kufanya ajizi Athalia aliuliza kilichotokea, akaelezwa kwa ufupi na ufasaha naye akawaombea mabinti hao wawili wakapona. Wanafunzi hawa wakasimulia kisa kizima jinsi jini lilivyowajia na kutaka kuwaangamiza kwa madai eti wanatoa siri zake. Athalia akaomba amani na ulinzi juu ya mabweni yao yote.

Siku iliyofuata Athalia alitakiwa kusambaza barua za ruhusa kwa ajili ya jointmas, alifanikiwa kufanya zoezi hilo akiwa na mwenyekiti msaidizi wa GALEFEMA Joanita Raphael. Baada ya zoezi hilo Athalia aliandika majina ya watakaohudhuria jointmas huku wenzake wakiendelea kujisomea. Athalia alihangaikia ruhusa hiyo kuanzia Alhamis hadi Ijumaa saa nane ndipo ruhusa ilipokamilika. Athalia hakufanya ajizi mara moja akashika daftari na kuanza kujisomea tayari kwa kujiandaa na mitihani ya Jumamosi (kesho yake). Siku ya Jumamosi kulikuwa na mitihani ya Kiswahili moja na Historia mbili. Athalia alisoma bila kupumzika na kufunga bila kupenda, jioni ya Ijumaa alikutana na wenzake kwenye discussion, akateuliwa kuwa mwenyekiti wa discussion. Walisoma somo la Kiswahili moja mpaka saa nne za usiku. Saa tano usiku alianza kusoma Historia mbili hadi saa sita. Usiku saa tisa akaamka kujisomea tena.

***********************************************************