webnovel

SURA YA KWANZA:

Maisha ya mwanadamu chini ya jua yamegubikwa na mambo mengi mithili ya aina ya miti iliyomo ndani ya msitu mkubwa. Wakati mwingine mwanadamu hupita katikati ya misitu mikubwa iliyotanda kiza kinene kama mawingu ya mvua yenye utusitusi mwingi, hupanda milima mirefu ya maisha lakini ama huweza kukifikia kilele au akashindwa kukifikia kilele hicho. Katika kupambana na maisha unaweza kukumbana na misukosuko mingi mfano wa dhoruba baharini, lakini huna budi kupambana nayo. Hakika maisha ya mwanadamu ni kitendawili ambacho mteguzi wake ni Muumba mwenyewe.

Mbali na kwamba kuna mamba, nyangumi na watawala wengine bado huyu mwanadamu yupo katikati yao na hana budi kuishi kadri ya mazingira yanavyomruhusu. Akijaribu kutafuta riziki katika msitu anakumbana na wazee wa nchi akina simba, chui wote watafuta kumfutilia mbali anajaribu kujitetea lakini bado wanamwonea, kwani rasilimali za dunia ya tano ziko mikononi mwao. Mwanadamu anajiuliza mbona wote ni wa kundi moja la mamalia? Kwa nini wananionea? Amesahau kuwa survival for the fittest, wenye nguvu ati ndiyo huishi kwa amani duniani. Haya ndiyo maisha ya mwanadamu katika dunia iliyojaa ufedhuli na udhalimu wa kila namna.

Katika safari hii ya maisha ya wanadamu, wengi husafiri safari ambayo ama ni fupi au ndefu sana katika kukifikia kilele cha mlima wa maisha. Mbali na kwamba wapo wengi wanaosafiri lakini ndani yao kuna msichana aitwaye Athalia ambaye ni rafiki yangu mkuu, mimi Dorine. Msichana huyu alizaliwa katika kijiji kimoja kiitwacho Elimu haina Faida miaka ishirini na nane iliyopita. Ni mtoto wa sita kuzaliwa katika familia ya bwana Daniel Abija na bi. Sarah Isaya. Msichana huyu ana umbo la wastani, kimo cha kati, rangi ya maji ya kunde, nywele zake nyeusi mithili ya nywele za singasinga, ana sura ya mviringo na meno yake yamepangika kama mstari wa askari jeshi walio katika maandalizi ya kupambana na adui na mwanya wa wastani. Athalia anapenda sana maendeleo na kufanya kazi kwa bidii sana. Ana upendo wa dhati kwa wote wenye kuonesha upendo kwake, ni mkarimu kwa watu mbalimbali anaowafahamu na asiowafahamu. Athalia Daniel anapenda sana elimu na kupigania haki zake na za watu wengine walio wanyonge.

Kaka yake mkubwa aliitwa Hoshea ambaye ndiye aliyemsomesha elimu ya sekondari hadi alipoingia Chuo Kikuu cha Highway katika nchi yao ya Mafanikio. Hoshea alikuwa na mapenzi ya dhati kwa ndugu zake ijapokuwa yeye aliishia darasa la saba lakini hakuona shida kumsomesha mdogo wake Athalia. Alijinyima kula ili mradi tu mdogo wake asome. Athalia ana dada zake wawili, Rehema na Hana, pia ana wadogo zake wawili Naomi na Jackline. Kaka yake mwingine aitwaye Jeremia, naye aliwajibika kwa nafasi yake. Huyu ni mrefu kama alivyokuwa Hoshea na wote wana umbo la wastani, lakini Hoshea alikuwa ni mweusi wakati Jeremia ana rangi ya maji ya kunde. Jeremia ana mapenzi ya dhati kwa ndugu zake wakati wote na wala hana kinyongo hata kwa watu wengine. Jeremia ni mbishi sana pale unapomshauri, huona yeye yuko sahihi wakati wote hata pale anapokosea lakini ni mwepesi wa kuomba msamaha. Siku zote wazungumza lugha ya taifa la Mafanikio husema kujua kwingi ni hasara lakini sifa ya pekee ya Jeremia ni kutubu akikosea.

Athalia katika maisha yake ana ndoto za kusoma hadi kuufikia uprofesa. Lakini Mungu husema kile anachokiri mtu ndicho kilicho katika nafsi yake na atapatiwa hicho akitenda kwa bidii. Athalia anaamini Mungu hatamwacha katika elimu yake na kile anachokikusudia kukifanya.

Athalia akiwa na umri wa miaka sita alitamani sana kusoma shule lakini kwa kuwa alikuwa mfupi wa kimo hakuruhusiwa kuanza darasa la kwanza. Ilipofika mwezi Machi mwaka huo huo Athalia kwa ung'ang'anizi wake wakaamua kumsajili darasa la kwanza kwa masharti kwamba darasa hilo atasoma miaka miwili. Hilo halikuwa gumu kwa Athalia kwani yeye anachotaka ni kusoma tu. Athalia akaanza darasa la kwanza mwaka huo na alipokuwa darasani alisoma kwa bidii sana kama simba aliyeko mawindoni, alikuwa na akili sana, hata wakati mwingine walimu wake walimshangaa sana kwani alikuwa mwerevu kimasomo. Alikuwa mwepesi wa kujieleza mithili ya sungura, walimu wapenda maendeleo wakampenda sana.

Athalia alipokuwa darasa la tano alifanya mapinduzi makubwa ambayo ilikuwa siri ya familia yake na mwalimu mkuu aliyeitwa Malammbughi. Athalia alichukizwa sana na mambo yaliyokuwa yakiendeshwa katika shule yao, alijiuliza hata lini tutakuwa watumwa wa mashamba ya matajiri wa wilayani Chanua? Kwa nini mkuu wa shule ametufanya vitega uchumi wake? Kwa nini tunateseka kiasi hiki? Je, ni lini matatizo haya yataisha? Maswali haya yalikuwa yakizunguka kichwani mwa Athalia, akiwaza na kuwazua akitafuta dawa ya mambo hayo.

Wanafunzi wa shule ya Katela walikuwa wakienda shule majira ya saa 12 asubuhi baada ya kuhesabishwa namba, mbiu ilikuwa ikipigwa kwenda mashambani kuvuna mahindi na kuyapukuchua katika msimu wa mahindi, kuvuna maharagwe msimu wa maharagwe na kuyapiga. Msimu wa viazi mviringo Athalia na wenzie wako kuvuna viazi mviringo wajaze magunia ya watu na mapato yanaingia mifukoni mwa walimu. Wanafunzi hawa waliteseka mno. Mara nyingine utakuta wako kung'oa nyasi biashara ya walimu. Unyonyaji uko kila sehemu, wanafunzi wanatoa jasho kuzalisha ili mifuko ya walimu itune, duuu! Hii ndio nchi ya Mafanikio.

Siku moja Athalia alijiuliza na kulia sana! Dada yake aitwaye Hana alimuuliza unalia nini Athalia? Athalia bila kuchelea akajibu dada naona kero hata kwenda shule kwa sababu ni mateso makubwa, kama sio kuvuna basi ni kulima na kufyeka mashamba ya walimu na matajiri wa wilaya hii ya Chanua. Hana aliona amsaidie mdogo wake, alimwambia amani haipatikani ila kwa ncha ya upanga. Hana alimshauri mdogo wake amwone mratibu kata wa shule za msingi. Athalia akapata kujiona mwepesi kwa kiasi fulani.

Siku iliyofuata Athalia alifika shuleni kama kawaida yake, mtu haachi asili yake, mbiu ikatangazwa kwenda kuvuna viazi mviringo vya tajiri mmoja aliyejulikana kwa jina la Maro. Athalia alifika shambani na kuchimba mistari miwili kisha akajificha na kuendelea na mambo yake. Athalia aliandika barua ndefu kuhusu mwenendo wa uongozi wa shule yake, walimu na uwajibikaji wao kwa kila somo. Alikaa mafichoni hapo mpaka saa moja jioni wanafunzi waliporuhusiwa kurudi nyumbani. Siku imepita bila kuwepo masomo.

Kesho yake Athalia alitinga ofisini kwa mwalimu wa darasa na kuomba ruhusa ya kwenda hospitali. Bila ajizi mwalimu alimruhusu Athalia laiti kama angejua asingemruhusu kwenda maana anapeleka bomu kwa mratibu wa kata. Athalia siku ya gulio la Lembuka aliwasili hapo na kuelekea ofisini kwa mratibu. Athalia bila kigugumizi mithili ya chiriku alishusha hoja nzito kwa mratibu, mratibu alipigwa butwaa. Baada ya kumaliza maelezo alikabidhi barua kwa mratibu. Mratibu alimuuliza swali moja la msingi: Je, walimu na wanafunzi wenzio wanafahamu lolote kuhusu hii barua? Athalia alijibu hakuna hata mmoja anayefahamu juu ya hilo. Mratibu akajibu sawa! Nitalifanyia kazi, lakini alimtega Athalia kwa kumpatia barua aifikishe kwa mkuu wa shule au makamu wake.  Athalia akatunga sheria baada ya kuipokea, akaifikisha kwa makamu mkuu wa shule alipoulizwa ameitoa wapi alijibu alipokuwa akienda posta alikutana na mratibu ndiye aliyempatia kwani anamfahamu vizuri mara nyingi hufika nyumbani kwao akifanya mazungumzo na baba yake.

Kama ilivyo ada ya muda hauchelewi baada ya mwezi mmoja mratibu alitinga shuleni huku akiwa tayari ameuagiza uongozi wa shule uwape taarifa kamati ya shule iwasili siku hiyo. Paliwaka moto, kikao kilikuwa kirefu mambo yakawekwa hadharani, Athalia yeye alikuwa miongoni mwa wanaoshangaa kikao. Kikao kiligharimu saa 6 bila mapumziko. Kikao kilipoisha mambo yakawa mshikemshike.

Mwezi mmoja ukapita mwalimu mkuu akahamishwa na kuletwa mwalimu mwingine. Mwalimu mkuu aliyefika alikuja na mabadiliko makubwa. Wanafunzi wanachofanya ni kujifunza na shughuli za shule tu. Muda wa kurejea nyumbani saa 8 kama ilivyo kwa shule nyingine. Hakika shule ya akina Athalia ilikuwa Giningi ndogo.

Athalia aliteuliwa kuwa dada mkuu wa shule, wanafunzi walikuwa wakimheshimu sana, yeye huongea pale inapotakiwa kuongea tu. Mambo haya yaliwafanya wanafunzi wenzake wengi wampende kutokana na misimamo yake ya kiutawala. Athalia alikuwa mhudhuriaji mzuri darasani, mchapakazi na mwenye bidii katika taaluma yake.