Uwa wa mama Zai ulijaa watu; ndugu na jirani. Kutokana na tamaduni za kiislamu, siku hiyo pia ilikuwa siku ya mazishi. Mahema yalikuwa yameshafungwa na chakula kilikuwa kikipikwa. Miziki ya kuomboleza ilipigwa na kila aliyemfahamu mama Zai alikuwa kwenye majonzi mazito.
Polisi walijitahidi kuusogeza msiba mbali na chumba cha mama Zai ili wasiharibu ushahidi. Reuben na Joy waliwasili, Joy akiwa amevaa nguo nyeusi kama heshima ya msiba. Askari mmoja alimfata Reuben mara tu alipomuona akiingia getini.
"Mkuu, tunashukuru kwa kuitikia wito.", alisema askari yule,
"Ni kazi yangu. Nipe mtiririko mzima.", Reuben aliongea huku akijongea chumba kile.
"Tulipata simu alfajiri kutoka kwa jirani wa marehemu akisema kuwa amesikia milio ya risasi. Alipokwenda kuhakikisha alimkuta marehemu akivuta pumzi ya mwisho.",
"Wasafishaji wameshasafisha eneo la tukio?",
"Hapana. Amri imetolewa kuwa mtu asishike chochote mpaka umalize ukaguzi mzima wa chumba.",
"Vizuri.",
Reuben alitoa gloves nne mpya kutoka kwenye mfuko wa koti. Mbili alivaa yeye na mbili alimkabidhi Joy avae. Hatimaye mlango wa chumba ulifunguliwa. Joy alipeleka mkono wake puani kutokana na harufu nzito iliyotoka ndani. Nzi wengi walichoropoka kwenye upenyo wa mlango, na kisha wao wakaingia.
Eneo lilitisha. Kwa mwenye roho nyepesi angeshikwa na kichefuchefu na kwenda nje kutapika. Damu ilitapakaa kila mahali; kwenye sakafu, ukutani na kwenye makochi. Meza ya kioo ya sebuleni ilikuwa imevunjika, na vioo vilikuwa vimelowa damu.
"Marehemu alikutwa juu ya hivyo vioo.", alisema askari aliyekuwa nyuma yao.
Reuben hakusema kitu. Aliendelea kukagua kila kona ya chumba. Kisha alitoka sebuleni na kugagua jikoni na vyumba vya kulala. Huko hakukuwa na mtafaruku wowote, hivyo alirudi sebuleni. Akielekea mlangoni, jicho lake liliona kitu kama karatasi likichungulia kutoka chini ya meza ya redio. Reuben alimpa ishara Joy ya kuokota karatasi hilo.
Karatasi hilo lilikuwa limekunjwa mara mbili.
"Likunjue.", Reuben alisema.
Joy alikunjua karatasi lile na kukuta maandishi ya kalamu nyeusi. Alionesha kushtushwa na ujumbe uliokuwa umeandikwa. Haraka alimpatia Reuben karatasi lile. Ujumbe ulisema;
UJUMBE HUU UMFIKIE ASKARI ALIYENIHOJI JANA. SINA NAMBA YAKO YA SIMU HIVYO INANIBIDI NIANDIKE KWENYE KARATASI. NIMEPATA SIMU KUTOKA KWA NILIYEMUONA USIKU WA KIFO CHA MONTANA. ANASEMA ATAKUJA KWANGU ILI TUZUNGUMZE. SINA AMANI NAYE, HIVYO NAANDIKA BARUA HII NA KUIFICHA NIKIAMINI KWAMBA KAMA KITU CHOCHOTE KITANITOKEA, BASI WEWE UTAWEZA KUIONA.
KITU PEKEE NACHOWEZA KUKWAMBIA NI; MWANAMKE NILIYEMUONA USIKU ULE NI MIONGONI MWA WANAWAKE WALIOTAJWA NA MONTANA. NASIKIA UNASIFA KUBWA YA KUTATUA KESI NGUMU. BASI HICHI NI KITENDAWILI NAKUACHIA. UKIWEZA KUKITEGUA, KIFO CHANGU HAKITAKUWA CHA BURE.
Reuben aliisoma barua ile tena kwa mara ya pili. Mwili wake uliingiwa na joto mithili ya homa. Alitoka nje ya chumba kwa haraka, barua akiwa ameishika mkononi. Aliuma ukuta wa midomo yake. Damu ilimchemka kwa hasira aliyokuwa nayo. Kifo cha mama Zai kilimuuma mno kwa sababu uwezo wa kumsaidia alikuwa nao. Ilimuuma zaidi baada ya kugundua kuwa yeye ndiye mtu mama Zai aliyemtafuta alipogundua anaweza kufariki. Hivyo aliona kuwa amemuangusha. Kesi haikutakiwa kuwa ndefu. Sasa kwanini jibu limemponyoka?
"Detective, upo sawa?", Joy aliuliza,
"Suzanne Depo, Janat Marko, Annabella Majimbo, na Leah Shahidi; muuaji wetu ni mmoja wao.", Reuben aliongea kwa sauti ya juu ili kila mmoja wa askari aliyekaribu asikie, "Ameua watu wawili sasa, sio kitu cha kupuuzia. Kitu pekee tunachojua ni kucha za bandia na tracksuit nyeusi. Hakuna kupumzika mpaka mwenye hatia apatikane.",
Kesi ilianza rasmi. Umakini mkuu ulielekezewa kwa watuhumiwa hawa wanne. Mmoja wao alikuwa na damu zisizo na hatia mikononi mwake, na sasa ilikuwa ni kazi ya Reuben na Joy kutegua kitendawili kile.
…
Mkuu wa jeshi la polishi, Bwana Msumari alisimama mbele ya vyombo vya habari. Tukio hilo lilikuwa likirekodiwa na kurushwa hewani muda huohuo.
Suzy alikuwa nyumbani kwake kajifungia. Filamu aliyokuwa akiangalia ilikatishwa kutokana na habari iliyokuwa ikirushwa. Hakuwa na budi kusikiliza kilichokuwa kikiendelea duniani, yaani, nje ya nyumba yake.
"Ndani ya masaa 24, jeshi la taifa kwa msaada wa mpelelezi Reuben Pasua, tumeweza kufahamu ukweli kuhusu kifo cha Montana Sabas kilichotokea juzi saa nane usiku. Hospitali waliweza kukuta sumu kwenye mishipa ya damu ya marehemu na kuhitimisha kuwa marehemu alijiua." alisema Msumari,
Suzy aliangua kicheko. Kwa sababu zisizofahamika, habari ile ilimfurahisha sana.
…
Vivyo hivyo na Janat, aliyekuwa kajifungia ndani ya nyumba yake alikuwa akiangalia habari kwenye TV.
"Tunasikitika kuwataarifu kuwa kifo cha Montana Sabas hakikuwa mikononi mwake, bali aliuawa na mtu mwingine.",
Janat hakuonesha mshituko wowote bali aliendelea kunywa mvinyo wake taratibu.
…
Annabella alikuwa akisikiliza kupitia redio ya gari. Baada ya kukaa sana ndani alihitaji kupigwa na upepo, hivyo sekretari wake, Thomas, alikuwa akimuendesha mjini jioni ile.
"Mama mwenye nyumba wa marehemu alitoa ushahidi huo jana akiwa kituo kikuu cha polisi na kuahidi kumtaja aliyemuona usiku ule. Kwa bahati mbaya, mama Zai amekutwa na umauti kwa kupigwa risasi mbili za kifua.",
Annabella aliguma na kuendelea kutazama nje.
"Jeshi la polisi litaanza mahojiano na watu wote waliokuwa na connection na marehemu Montana. Kwenye ujumbe mfupi ulioachwa na marehemu mama Zai, watuhumiwa wetu wakuu ni wanne, nao ni hawa wafuatao; Suzanne Depo, Janat Marko, Annabella Majimbo na Leah Shahidi.",
Annabella aligeuza kichwa na kumuangalia Thomas. Alivaa uso wa mshangao.
"Nimesikia vizuri au la?", Annabella aliuliza bila uhakika, maana alikuwa akifikiri vitu vingi kwa wakati mmoja,
"Umesikia vizuri.", Thomas alimuhakikishia,
"What's wrong na hawa watu lakini? That bitch messed with my life and died but hata baada ya kifo bado anataka kuniandama? Hivi wapo serious kweli hawa?",
Thomas alikaa kimya.
"I need to travel. Hii nchi inanisuffocate. Siwezi. I need to breathe.",
"Unataka kwenda wapi?",
"Anywhere. Ukifika nyumbani, book me a flight ASAP.",
"Yes, boss.".
***