webnovel

CHAPTER 11

FARAJA STATION

Mkurugenzi alikuwa kwenye kikao, hivyo iliwabidi wamsubiri ofisini kwake. Wakati wakisubiri, Joy aliona aendeleze mada.

"Detective, kwanini tusingemuweka mama Zai kwenye ulinzi mpaka kesi hii itakapoisha? Ameshuhudia kifo. Maisha yake yapo hatarini.", Joy alishauri,

"Mama Zai bado hajafanya uamuzi. Sasa hivi yupo njia panda. Hajui kama ashirikiane na jeshi la polisi, au amfichie siri muuaji ili aendelee kulipwa. Pale atakapofanya uamuzi ndipo na sisi tutakapoweza kutumia resources zetu kumlinda.",

"Je, muuaji akimuua kabla hajafanya uamuzi?", 

Kabla Reuben hajajibu, mlango ulifunguliwa na mkurugenzi aliwasili. Wote wawili walimsindikiza kwa macho mpaka alipoketi nyuma ya meza yake.

"Ujio wenu umenishtua sana.", alisema Rajabu, "Siku zote nasikiaga habari zako. Nafurahi kukutana na wewe rasmi.", alimwambia Reuben,

"Mimi pia.", alisema Reuben, "Huyu ni msaidizi wangu, Joy.",

"Nashukuru kukufahamu, Joy.",

"Mimi pia.", Joy alijibu.

Kama kawaida, Joy aliwasha simu yake na kuanza kurekodi mazungumzo.

"Mkurugenzi, niambie jinsi ulivyomfahamu marehemu Montana Sabas.", Reuben alifungua hoja,

"Montana alituma barua ya maombi ya kazi kwenye ofisi zetu. Kwa bahati mbaya sasa hatuajiri, hivyo maombi yake yalikataliwa. Siku moja nilikuta barua yake mezani kwangu. Aliituma moja kwa moja kwangu bila kupitia ofisi ya human resource. Ndani ya hiyo barua aliandika kuwa anataka tumuajiri kwa mwezi mmoja tu, na aliweka hoja nzima ya kipindi chake.",

"Naamini uliona kuwa wazo lake ni la hatari. Kwanini ulikubali?",

"Mkuu, sisi ni wafanyabiashara. Uchumi wetu unatokana na idadi ya watazamaji na wasikilizaji wetu. Tangia station yetu ifunguliwe, hakuwahi kutokea mtu aliyethubutu kufanya kitendo alichofanya Montana.",

"Kwahiyo ulikubali kwasababu ulijua utatengeneza pesa na si vinginevyo, sio?",

"Ndiyo.", Rajabu hakubisha, "Lakini pia niliona ni vyema kuficha taarifa zote kuhusu Montana kwa ajili ya usalama wake. Hata vipindi vyake vyote vinne hakuvirekodia kwenye studio zetu. Tulimpatia gari yenye vifaa vyote vya kurekodia. Yeye alikuwa akiiendesha mpaka sehemu iliyomridhisha na kufanya vipindi hapo.",

"Kwa akili za haraka haraka, unahisi Montana amewezaje kujua taarifa zote za matajiri hawa?",

"Sifahamu hilo.", Rajabu alitikisa kichwa,

"Mkurugenzi, ofisi yako huwa ina utaratibu wa kufanya background check kwa watu waliowaajiri?",

"Ndiyo.",

"Bila shaka ulimfanyia background check Montana.",

"Ndiyo.",

"Naliomba faili lake tafadhali.",

Ingawa Rajabu alikubali, bado alionesha kuwa na wasiwasi kidogo. Hakuwa na uhakika kama awape ushirikiano au la.

"Nina swali tafadhali, kama hautojali.", Rajabu aliendelea,

"Uliza.", Reuben alimruhusu,

"Kwanini mnapeleleza taarifa za mtu aliyefariki, tena kwa kujiua mwenyewe?",

"Bwana Rajabu, nasikitika kukutaarifu kuwa Montana Sabas hakujiua, bali aliuliwa.",

"WHAT!", Rajabu alishtuka, "Una-unasemaje?",

"Jeshi la polisi litatangaza rasmi habari hizi. Hivyo, bwana Rajabu, taarifa yoyote ambayo unahisi itasaidia upelelezi wetu kufikia tamati successfully, usisite kunitaarifu.", 

Reuben alichomoa kadi yake kutoka kwenye koti na kukabidhi bwana Rajabu. 

"Mtalikuta faili mapokezi.", Rajabu alisema huku akiitizama kadi ile,

"Asante kwa ushirikiano.",

Reuben na Joy waliondoka.

Jioni, Leah alipotoka kazini alienda kwa mama mkwe wake. Ilikuwa ni wiki sasa tangu Paul ahamie kwa mama yake kwa muda mpaka watakapokamilisha talaka yao. Alijua ni muda gani mume wake alitoka kazini, na kwa bahati nzuri alimkuta. Paul alikuwa kibarazani na mama yake wakipata chai ya jioni.

Baada ya mama mkwe kumuona Leah akishuka kwenye gari, tabasamu lake lilipotea. Chuki ilikuwa imejijenga kifuani mwake, akiamini kuwa Leah alikuwa akimtesea mwanae. Alisubiri kwa hamu siku ambayo Leah na Paul wataachana rasmi ili na yeye aweze kuwa na amani. Leah alifahamu yote hayo na alijitahidi kutomwekea mama mkwe wake sura ya mbuzi.

"Shikamoo mama.", Leah alimwamkia mama Mkwe,

"Mbona unakuja bila taarifa? Hapa sio kwako.", mama mkwe alijibu kwa kejeli,

"I know. Nisamehe.",

"Umekuja kufanya nini?",

"Nina maongezi na mume wangu.",

Paul alimtazama Leah bila kusema kitu chochote. Mama mkwe alibeba kikombe chake cha chai na kuingia ndani kwa jazba. Leah aliketi kwenye kiti kilichokuwa wazi sasa, kisha alifungua mkoba wake na kutoa bahasha aliyopewa na Paul wiki moja iliyopita, iliyobeba fomu zao za talaka.

Paul alichukua bahasha ile kwa haraka na kuifungua. Alijitahidi kuficha furaha yake akiamini kwamba talaka imekamilika na sasa atakuwa huru. La hasha! Sahihi ya Leah haikuwepo. Paul aliganda kama mwizi, macho akiyatumbua.

"Ni nini hiki?", Paul aliuliza kama haelewi alichokiona,

"Nimefanya uamuzi.", Leah alitamka, "Hakutakuwa na talaka.",

Paul alidondosha fomu zile bila kujua, "Leah, naomba usinitanie.",

"Sio utani, nipo serious.", 

Mwitikio wa Paul, Leah aliutegemea. Alijua kabisa kuwa kitendo cha yeye kukokuweka sahihi yake kingempatia Paul manung'uniko ya moyo.

"Paul, hivi unajua mimi na wewe tumetoka wapi? Unajua ni vitu gani nimejitolea na kuvumilia mpaka tumefika hapa? Unahisi naweza kukubali kukupa talaka bila hata sababu ya maana? Utakuwa ulihisi I'm stupid or something.",

"Leah, ni kitu gani huelewi? Mimi sikupendi!", 

"I don't care. Kama umechoka kuishi na mimi, chukua funguo ya nyumba yetu ya Buyuni ukaishi huko. Sitakusumbua. Lakini tukio lolote litakalohitaji uwepo wetu mimi na wewe, tutakwenda pamoja kama mume na mke.",

Paul alipandwa na hasira iliyopelekea jicho lake la kushoto kumwaga chozi, "Kwanini unanifanyia hivi, Leah?",

Leah alicheka kidogo, "Hujui ulichofanya, si ndio? Basi tuendelee kukomeshana.",

Mlango ulifunguliwa na mama mkwe alitoka nje kwa jazba. Kifua kilikuwa kimevimba kwa dukuduku alilokuwa amelibeba. Alitamani sana kumkamata Leah kwa kola ya shati na kumchapa vibao.

"Wewe mtoto ni shetani!", alipayuka, "Umenitesea mwanangu miaka yote hii na bado hutaki kumuachilia? Unataka umle nyama? Unataka umfanye mwanangu zoba?",

"Haya maongezi ni kati yangu mimi na mume wangu.",

"USIMJIBU JEURI MAMA YANGU!", Paul alifoka, "TAKUKATA VIBAO!",

Leah alinyanyuka na kuwatazama wote wawili. Kwa mbali walimfurahisha.

"Paul, mimi naenda. Ukihitaji ufunguo utaniambia.", aliongea kwa utaratibu,

"Mwanangu hakupendi, anampenda Cecy!", mama mkwe aliendelea kutema sumu, "Ndoa imeshakushinda. Miaka kumi umeshindwa kumtunza mume wako. Muda wako umekwisha. Sasa ni zamu ya mwingine.",

Leah alitabasamu na kunyanyua mkoba wake, "Usiku mwema.",

Hata alipokuwa akielekea kwenye gari, bado alikuwa akiyasikia maneno machungu yatokayo kwenye kinywa cha mama mkwe. Uwezo wa kujibishana nae alikuwa nao lakini hakutaka kujishusha kiasi hicho. Alichotaka kusema kilikuwa kimeshasemwa. Hivyo alipanda gari yake na kuondoka maeneno hayo kabla mambo hayajawa mengi.

Asubuhi na mapema, Reuben aliamshwa na mlio wa simu yake. Akiwa bado na usingizi, alipenyesha mkono wake chini ya mto na kuvuta simu yake. Mwanga ulimuumiza macho lakini aliweza kusoma jina. Alikuwa ni Joy hivyo ilimbidi aipokee simu ile.

"Good morning, Joy?", Reuben alizungumza wa kwanza,

"Detective, kuna shida.", aliongea Joy. Sauti yake ilifanana na ya mtu mwenye haraka, au aliyekimbizwa.

"Shida gani?", Reuben aliuliza, taratibu usingizi ukianza kupotea,

"Mama Zai amefariki dunia nyumbani kwake leo asubuhi.",

"What!", Reuben alinyanyuka na kukaa kitako, "How?",

"Amepigwa risasi mbili kifuani. Mwili wake umepelekwa hospitali ya Temeke.",

"Wewe upo wapi sasa hivi?",

"Naelekea hospitali _",

"Hapana.", Reuben alimkatisha, "Tukutane nyumbani kwa mama Zai.",

"Sawa detective.",

Joy alikata simu. Mkono wa Reuben sasa ulikuwa kwenye paji lake la uso. Kifo cha mama Zai kilimsikitisha. Hasa kwasababu kuna majibu alipaswa kusikia kutoka kwake lakini sasa haikuwezekana. Bila kupoteza muda alitoka kitandani na kujiandaa.

***