webnovel

chapter 31

" na mlima unahusiana nini na laana" anauliza mkono wake ukienda kwenye paji la uso wake kufuta jasho lisije likafanya chakula kuwa kitamu zaidi."inasemekana huko ndiko walikomuulia Ndesha,walimtoa kafara chini ya mbuyu juu ya jiwe lililokuwa likitumika kumfanyia matambiko wakamwacha siku tatu,na kuua familia yake ndipo mzimu wake ulikasirika na kuilaani nchi na eneo lile mpaka leo hii amna anayeingia huko akatoka mzima" Tulya anabaki ameganda akiifikiria ile ndoto kinachosimuliwa ni kama alichokiona " itakuwa ni mawazo yalienda huko tu baada ya kusikia hadithi ndio maana akaota" anajiwazia .

" kwa nini wasifanye tambiko kuuondoa" anatoa wazo " unadhani hawakufanya hivyo?" anasema Sinde " walifanya?" anauliza " Ndio,lakini ikashindikana kwa sababu Ndesha sio mzimu mzuri na mzimu wa kisasi,walichokifanya ni kuufungia huko tu usitoke na Kuja huku, na watu wakazuiliwa kuingia kule,lakini watu wengi hawaamini hujaribu kwenda na huishia kunyigwa na Ndesha"

" hilo tatizo sasa na wanyama ndio wamehamia huko" anaongea Tulya akivuta pumzi ndefu.

" hawajahamia"

" mhh!"

" watu wanasema Ndesha ndio anawaita wanyama kuwavuta watu ili akwanyonye damu"

" ehhh! nahakika amna mtu atakayeenda"

" ni mtu Mmoja tu anayeweza kuingia kwenye msitu ule " wanamsikia mtu akiongea wanageuka na kumuona Bibi Sumbo " mama umefika saa ngapi?" anauliza Tulya akimpatia kigoda akae naye anasimama,bibi sumbo anakaa " watu watamaliza kazi nyie hamjamaliza kupika maana mnaongea kwa kutumia mikono" wote wanacheka Sinde anabeba chungu na kusimama kwenda kubandika jikoni " tunamaliza Sasa hivi mama" anaongea Tulya akikaa kwenye mkeka,Sinde anarudi na yeye anakaa kwenye kigoda " hadithi hiyo ulisikia wapi?" anamuuliza Sinde akiangalia chale zake mkononi Tulya anamuona " unaumwa mama?" anamuuliza uso ukiwa na wasiwasi." usijali mwanangu,mkono umekuwa ukinisumbua sana siku mbili tatu hizi nimeenda kwa Mzee Ndabi hapo kanichanja chale kasema nitakuwa sawa" " upunguze kushona ukili" Tulya anamwambia " nitakuwa sawa mwanangu,Mzee Ndabi ni mganga mzuri sana na wote tunamwaminia hapa Kijijini,nikiupumzisha Leo na kesho tu nitakuwa sawa,hujaniambia nani kakuhadithia hiyo hadithi" anarudisha swali kwa Sinde " yule Mzee aliyenyongwa na familia yake" Sinde anamjibu " Mzee Ndelea"

Anamtajia jina " atakuwa ndio huyo simkumbuki jina nilikuwa bado mdogo" " ndio maana unaikumbuka vizuri Mzee Ndelea alikuwa Yuko vizuri kusimulia hadithi" anaongea Bibi Sumbo macho na uso wake vikionyesha kumpeleka mbali katika nyakati nzuri." je ni nani anayeweza kuingia kwenye milima ya nkyala mama" anauliza Tulya na kumtoa Bibi Sumbo kwenye kumbukumbu zake " ni mtu mwenye nguvu kama zake ndio anaweza kuingia huko" " kwani mtu huyo yupo?" anuliza Sinde.

" ndio,kwa sababu Ndesha alipozaliwa alipewa nguvu kubwa sana na mizimu,alikuwa na uwezo wa kutambua au kuona vitu vingi visivyooneka ndio maana ilikuwa rahisi kwake kugundua kuwa mtemi alikuwa na lengo baya hivyo kumuondoa Ndesha inabidi aje mtu aliyemzidi uwezo wake au mwenye uwezo sawa na yeye na uwezo wa ile mizimu inayoishi kwenye kasri la mtemi" anaongea akimwangalia Tulya " namwonea huruma huyo atakayekuja kupewa nguvu hizo maana kupigana na mizimu ni hatari hata kufikiria tu inanifanya mwili kuchemka je nikiiona si nitakufa hata kabla sijapigana" anaongea Tulya akinyanyua mabega yake.

" nadhani hupokea mafunzo jinsi ya kupigana nayo" anaongea sinde " hiyo hainiambii kuwa siwezi kufa,hunipeleki hata kwa mkuki" anaongea Tulya akinyanyuka kwenda kuangalia mboga jikoni Sinde anacheka " unavyoogopa kufa" anamwambia " kwani wewe huogopi kufa? Mimi sitaki kufa umri huu,tena tuachane kabisa na hii maada maana Sasa hivi inanitisha mambo ya kupigwa na radi kiangazi hiki hata siyataki " anaongea Tulya na Sinde anazidi kucheka " Tulya mdadisi kaenda wapi?" anauliza Sinde na Bibi Sumbo kukubaliana naye kwa kichwa.

"kama udadisi utaniingiza matatizoni nauacha bila hata kupepesa jicho" anawajibu akitoa mboga jikoni na kubandika chungu kingine chenye maji." usipoenda watu wengi wataangamia hivyo utake usitake lazima uende" Bibi Sumbo anasisitiza " ndio hilo nalo la muhimu" anaongea kwa sauti ya chini mikono yake ikienda kiunoni na meno yake yaking'ata midomo yake ya chini " aaa hilo halinihusu Mimi kwani sio Mimi ninaeenda atakayefanya maamuzi ni yule atakayekabidhiwa majukumu hayo, siwezi kuamua sababu sio Mimi" anaongea akirusha mikono juu.

" tunachosemea ni iwapo utakuwa wewe " Bibi Sumbo anamwambia " siwezi kuwa Mimi na sitaki kuwa mimi hata kuwaza kufanya maamuzi hayo sitaki" anaongea akikaa tena kwenye mkeka" huwezi kujua hatima ya maisha yako mwanangu,ni mizimu pekee" Bibi Sumbo anamkumbusha " nadhani hata hiyo mizimu haiwezi kumpa kazi ya muhimu kama hiyo mtu kama mimi,na ikifanya hivyo itakuwa imepungukiwa na uwezo wa kutoa maamuzi kwani Nina uhakika kibarua chao kitaota nyasi " anaongea kwa uhakika asitake kujihusisha na mambo ya kupigana na mizimu kwani hata wazo tu linamkausha damu.

Baada ya kumaliza kupika Nzagamba na marafiki zake wanakula na kuondoka Nzagamba akibeba mitego yake na ulimbo.

Kiza kimeingia na Nzagamba hajarudi nyumbani,Tulya anakaa nje akimsubiri " atakuwa bado yuko na marafiki zake kwa nini usiingie ndani huku,huko nje baridi" Bibi Sumbo anamwambia aliyemuona Tulya amekaa nje kwa mda mrefu.Tulya ananyanyuka na kuingia ndani. wanakaa na kuanza kuota moto " unachukia majukumu makubwa kiasi hicho" anaongea Bibi Sumbo macho yake yakiwa kwenye moto vidole vyake vikiwa vimekumbatiana. " majukumu yapi hayo mama" Tulya anajibu akimwangalia lakini Bibi Sumbo hatoi macho yake kwenye moto " ulisema mchana ukipewa majukumu kama ya Ndesha huwezi kuyapokea"

" aaa kumbe unazungumzia hilo,kupambana na mizimu mtu anahitaji nguvu ya ziada mama,Mimi nitapambana nayo vipi" anaongea akipeleka macho yake kwenye moto na mkono wake unaenda kuuchochea " utafanyeje endapo utapewa nguvu hizo" anaongea Bibi sumbo na Tulya anageuza sura yake na kukutana na macho yake yaliyojaa umakini ,Tulya anameza mate funda macho yake yasiondoke machoni kwa Bibi sumbo " eee-endapo ningepewa,aaah sijui nadhani ningekuwa nimejiandaa endapo ningekuwa najua tangu awali,kuokoa watu wengi ni kazi ngumu"

Bibi Sumbo anavuta pumzi ndefu macho yake yanarudi kuutazama moto " majukumu huja mwanangu,na huwezi kuyakimbia,jambo la muhimu ni kukabiliana nayo,pasipo kutetereka sababu maisha ya watu wengi yapo mikononi mwako.wakati wa vita ukionyesha kutetereka adui anapata nafasi ya kujua udhaifu wako,muda wote hakikisha unamwangalia machoni"

Tulya anabaki akimsikiliza asijue mazungumzo haya yanaelekea wapi " changamoto ikija siku zote inanjia ya kutatulia,na ukiona pambano haliko upande wake rudi nyuma jipange na utafute njia njingine ya kupitia kwani kwendelea Mbele katika hali kama hiyo unaweza kuumiza wengi hasa pale unapokuwa na vingi vya kupoteza,weka hiyo akilini siku zote.na ukipewa madaraka na nguvu usije ukatumia vibaya kwa faida yako binafsi siku zote kuwa na busara kabla ya kuamua usije ukafanya maamuzi ukiwa na hasira"

" mama bwana unaongea utadhani hiyo mizimu imegonga mlangoni na kusema Bibi Sumbo mkweo ni mrithi wa Ndesha" anaongea Tulya akicheka " nimekwambia tu huwezi jua hatima ya kesho na pengine wakati huo sitakuwepo kukupa ushauri" anamwangalia usoni na kuona anachokiongea anamaanisha " anapatwa na nini huyu" anajiuliza moyoni " mama uko sawa" anamuuliza kabla Bibi Sumbo hajajibu wanasikia sauti ya mbwa nje " kitoto cha mbwa?" anauliza Tulya akisimama na kuelekea nje akifuatiwa na Bibi Sumbo

Wanatoka nje na kumuona Nzagamba akiwa na vitoto vya mbwa viwili " umekuja na mbwa?" anauliza Tulya miguu yake ikiganda alipo " ndio,Mkita kanipatia" anajibu akipiga hatua kuelekea alipo Tulya " usinisogelee!?" anapiga makelele Tulya akipiga hatua kurudi nyuma na miguu ya Nzagamba kuganda ghafla " Kuna nini?" anauliza na baada ya kuona Tulya anazidi kurudi nyuma anamuuliza " unaogopa mbwa?" " ndio" anajibu na kupiga hatua nyingine kurudi nyuma " lakini hivi ni vitoto tu" anamjibu akipiga hatua kumfuata lakini Tulya anatoka mbio na kujificha mgongoni kwa Bibi Sumbo " usinisogelee,viwe vitoto lakini bado ni mbwa tu" anaongea akichungulia alikojificha mgongoni na kumfanya Bibi Sumbo kucheka

" haya hao mbwa utawaweka wapi?" Bibi Sumbo anamuuliza " nawaweka huko uani nimewajengea kijumba huko" anajibu akivipapasa " huko uani watawezana na mkeo" " nilikuwa sijui kama anaogopa mbwa,nitafanya mpango wa kuwahamisha kesho" anaongea akiondoka huku akitabasamu kujua mbabe Tulya anaogopa mbwa. " haya kamwandalie mumeo chakula mbwa wameshaondoka" anamsikia Bibi Sumbo na kupumua kwa ahueni,anaingia ndani na kuanza kuandaa chakula " beba upeleke nyumbani kwenu Mimi nataka kulala" anabeba chakula nakumtakia mama mkwe wake usiku mwema na kuondoka.

Usiku Tulya akiwa amelala anajikuta kwenye msitu mnene tena,baridi likipenya kwenye ngozi yake " Niko wapi?" akiangalia huku na kule.Anapiga hatua asijue anaelekea wapi, baada ya muda anaona miale ya moto na kusogea karibu na miale inapotokea anaona watu wakiwa wamezunguka kitu " wanafanya nini usiku huu hawa" anajiuliza na kusogea karibu na pale walipo alichokiona kinamfanya moyo wake utake kutoka kwenye banda lake la mbavu "mizimu nisaidie!?" anapiga makelele na kuamka " kile nini!?" anajiuliza akishika kifua chake kuutuliza moyo.