webnovel

MUELEKEO WA MSHALE

Sinta alijibanza kwenye uchochoro, gizani, akisubiri. Watu walipita na kurudi bila kumuona. Baada ya kusubiri kwa zaidi ya dakika kumi na tano, hatimaye alisikia sauti ya hatua zikijongea kichochoroni.

Muhudumu wa Tarura alikuwa akirudi kwenye makazi yake baada ya kumaliza pirika zote za kuandaa mwili wa kuhani mkuu kwa ajili ya mazishi. Alikuwa kachoshwa na mengi, na kilichomuuma zaidi ni kwamba mmiliki wake alikuwa kafariki. Kutokana na sheria za ikulu, alitakiwa kufunga virago vyake na kuondoka siku iliyofuata. Wahudumu wengi walikuwa masikini. Kufanya kazi ikulu iliwapa uwezo wa kusaidia familia zao kijijini. Sasa alikuwa matatani kurudi umaskinini tena. Ilimpatia unyonge.

Alipokaribia kichochoroni, moyo ulimruka baada ya kuvutwa na mtu asiyejulikana gizani. Alitetema akijitahidi kuona sura ya mtekaji wake.

"We-wewe nani?", aliuliza kwa woga.

Sinta alicheka kidogo, "Mimi ni mtu nayeweza kuokoa maisha yako na ya familia yako kama utafanya nitachokuamuru.", alisema.

Muhudumu aliifahamu sauti ya Sinta. Isitoshe, harufu tamu ya marashi ilikuwa imewazunguka. Bila shaka ilikuwa ni yeye.

"Binti mfalme?", muhudumu aliita kwa kiulizo.

"Ewaa! Kama sikosei unakwenda kuanza kufunga mizigo yako.",

"Ndiyo, binti mfalme.",

"Kwa bahati nzuri, ninahitaji muhudumu wa kiume wa kusaidia wahudumu wangu wa kike kufanya kazi ngumu kama kubeba mizigo mizito.", Sinta alisema, "Ningependa sana nikuchukue wewe.",

Matumaini yalifurika moyo wa muhudumu. Furaha ilimpelekea kuangukia magoti na kuanza kubusu miguu ya Sinta.

"Nitafanya chochote utachoniamuru, binti mfalme. Nahitaji hii kazi.", alisema kwa hamasa.

"Nafahamu hilo. Sharti langu ni moja tu, kuna kitu nataka ufanye.",

"Kitu gani, binti mfalme?",

"Baba yangu yupo kwenye moto sasa akitaka kujua kilichomkuta kuhani mkuu. Ulipoenda kumuita, ulimwambia chochote?", Sinta aliuliza,

"Hapana. Nilimwambia tu kuwa kuhani mkuu alihitaji kuongea naye.",

"Haukumwambia kuwa ulimuacha na mimi?",

"Hapana, binti mfalme.",

"Vizuri. Basi nataka ufanye hivi; Nenda kwa mfalme, mwambie kwamba ulipokwenda kumuita ulimwacha Tarura na mgeni. Mwambie kuhusu karatasi la ujumbe ulilopewa na kuhani mkuu na pia mueleze ya kuwa mgeni huyo alikupokonya.",

Muhudumu alipata wasiwasi, "Binti mfalme, unataka nikamwambie baba yako kwamba ulikuwa wa mwisho kumuona kuhani mkuu?",

"Hapana. Mfalme akikuuliza mgeni huyo alikuwa nani, mwambie alikuwa Aera, dada wa konsoti Gema.",

"Lakini _",

"Kama unataka kuendelea kufanya kazi ikulu, basi huna budi kunisikiliza. Uamuzi ni wako.",

Muhudumu aliwaza sana, hatimaye alifikia hitimisho.

"Tafanya ulivosema, binti mfalme.", alitamka.

Sinta alivaa tabasamu ovu.

Ndiyo kwanza malkia Omuro alikuwa amewasili chumbani kwake na kuanza kuvuliwa nguo zake kwa ajili ya kupumzika, lakini hodi ilisikika kutoka mlangoni. Malkia alikuwa hategemei mgeni yeyote, na alikuwa amechoka. Alimuamuru muhudumu wake mmoja akaangalie ni nani mbishaji hodi. 

Muhudumu alirudi ndani baada ya dakika chache;

"Malkia Omuro, ledi Kompa amekuja kukuona.", alisema,

"Umemwambia nimechoka?", malkia aliuliza,

"Ndiyo, ila amesema anachotaka kukwambia ni muhimu sana.",

"Mruhusu aje.",

Muhudumu alikwenda kumkaribisha mgeni ndani. Ledi Kompa alimpa malkia heshima yake kisha kunyanyua kichwa. Malkia alisitisha kubadilisha nguo kwa muda ili aweze kumsikiliza ledi Kompa na shida iliyomleta. Alivuta kiti na kuketi kisha ledi Kompa alifwata baada yake.

"Kabla ya yote, nataka kufahamu urefu wa maongezi.", malkia Omuro alianza,

"Sidhani kama yatakuwa marefu sana, malkia.", ledi Kompa alijibu.

Kama kawaida, wahudumu waliwapisha ili kuwapa usiri.

"Malkia Omuro, nimekuja na habari mbaya.", alisema ledi Kompa,

"Unamaanisha kuna habari mbaya zaidi ya kifo cha kuhani mkuu?",

"Ndiyo, malkia.",

"Habari gani?",

"Habari zinamuhusu Aera, dada wa konsoti Gema.",

Malkia Omuro alirudi nyuma kuegamia kiti chake. Hakusema neno lolote.

"Nina wasiwasi kuwa Aera amekuja hapa kwa lengo la kumtega mfalme wetu na kumnasa kimapenzi. Nimeshuhudia kwa macho yangu Aera akimkumbatia mfalme mbele ya bwawa la samaki.", ledi Kompa aliendelea, "Sisi kama wake wa mfalme inabidi tushirikiane pamoja kuepusha janga hili lisitokee.",

Malkia Omuro alicheka, "Janga?", aliuliza, "Kwanini unaita hili swala janga?",

"Malkia Omuro, Aera sio mtu mzuri. Amebeba chuki na nia mbaya.",

Malkia Omuro alimsoma ledi Kompa kimyakimya. Alikuwa ni mkubwa zaidi yake hivyo alijua mengi sana kuhusu kila kitu kilichokuwa kikiendelea ndani ya himaya yao. Kuna mwitikio ambao ledi Kompa alikuwa akiutegemea kutoka kwake, lakini kwa bahati mbaya, malkia hakuwa kwenye kiwango chake kiumri wala kiakili.

"Unajua siku mbaya kuliko siku zote kwenye maisha yangu ni ipi?", malkia Omuro aliuliza, 

"Ha-hapana, malkia.",

"Ilikuwa siku niliyomzaa Sinta. Nilifurahi sana kupata mtoto wa kike, na nilitegemea kuwa mume wangu angefurahi pia. Ilipofika jioni, hata maumivu hayajaisha, nililetewa habari kuwa wazee wa baraza wamemtafutia mfalme mke wa pili na yeye amekubali. Baada ya siku tano, ledi Erini aliwasili.", malkia alisimulia, "Baada ya hapo nilifahamu nafasi yangu kwa mfalme, ya kwamba kwake mimi ni mwanamke tu kama wanawake wengine na hakunipenda kwa dhati kama nilivyompenda mimi.",

"Malkia Omuro, huyu Aera _",

"Kama mfalme amevutiwa na Aera na kutaka kumfanya ledi kama wewe na Erini, basi tamuonesha mfalme ushirikiano kama niliomuonesha alipomleta Erini, na alipokuleta wewe. Sina sababu ya kumchukia Aera.",

Ledi Kompa aliumizwa baada ya kugundua kuwa malkia hakuwa na msaada aliotegemea. 

"Nakuhurumia sana, ledi Kompa.", malkia aliendelea, "Mwanaume akishaleta mwanamke mwingine ndani ya nyumba ambayo anaishi na mkewe, kaa ukijua hatoacha. Zamani ilikuwa ni mimi na yeye tu. Kisha ikawa mimi, yeye na Erini. Baadaye tukawa mimi, mfalme, Erini na wewe, na sasa itakuwa mimi, wewe, Erini, mfalme na Aera. Miungu ikimjalia mfalme maisha marefu, basi na Aera atapata mwenzake. Haya ndio maisha yetu.",

"Mimi nilikuja na nia nzuri ya kumpenda na kumjali mfalme wetu.", ledi Kompa alijitetea,

"Bila shaka na Aera atakuwa na malengo hayo.",

"Malkia Omuro _",

Malkia alipiga mwayo na kumkatisha, "Usiku sasa, ledi Kompa, na mwili wangu umechoka sana. Nahitaji kupumzika.",

Sentensi hiyo ilijitosheleza. Ledi Kompa alinyanyuka na kuinamisha kichwa kwa kujing'ang'aniza, "Usiku mwema, malkia Omuro.", alisema huku akiuma meno.

"Usiku mwema, Kompa.",

Ledi Kompa aliondoka na moyo mgumu. Mtu pekee ambaye angeweza kumsaidia amemtupa. Je, ajichukulie sheria mikononi mwake?

***