webnovel

SURA YA TISA

Tayari Athalia ametuma maombi ya kusomea shahada ya uzamivu katika nchi yake yenye neema ya Mafanikio chuoni Highway. Mumewe nae mambo yamepamba moto kuhakikisha kwamba miaka mitatu anakuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Highway, mpaka mkewe amalize shule, mapenzi kizunguzungu, ugonjwa usio na mshauri. Johnson yeye mambo yametiki kilichobaki ni Athalia kupata udahili. Lakini wazo linalozunguka akilini mwao ni la nishati katika nchi yao nzuri ya Mafanikio.

Mafanikio ni nchi iliyojaliwa kila aina ya rasilimali, madini ya kila namna vivutio vya kila namna, ulimwengu unaishangaa nchi hii kwa kupendelewa, ukigeuka huku unakutana na maji kila upande na mengine yana rangi za kupendeza yenye kuvutia uyaonapo rangi waridi. Madini ya kila namna kama vile dhahabu, almasi ya rangi waridi, tanzanaiti yenye rangi ya bluu madini yapatikanayo Mafanikio tu. Hiyo haitoshi, milima ya kila namna, mlima mrefu kuliko yote katika ulimwengu wa dunia ya tano, wanyama wa aina zote, ndege, aaah! Natamani kulia, huku moyo ukivuja damu na macho yangu yanacheka ili hali machozi yanalengalenga. Dubwana gani limeivamia nchi ya Mafanikio uzalendo eti haupo.

Wanyama, vyura wazuri wazaao eti wasafirishwa kwenda nchi ya bepari wa kusini magharibi mwa ulimwengu. Mchawi karoga akili zetu. Amka toka usingizini maana saa ya kujikomboa imewasili uwanja wa ndege, ipokeeni kila mmoja aijaze moyoni mwake, shime kuchukua nafasi kwa kila mmoja na kwa uzalendo mkuu. Tuzilinde rasilimali zetu ambazo ni adimu, ulimwengu wazimezea mate. Haya mawazo yanazunguka akilini mwa Athalia jamani!

Siku zikayeyuka, mara udahili ukatoka, Athalia amedahiliwa, sasa kilichobaki ni maandalizi ya kwenda nchini Mafanikio. Lakini akili imegubikwa na wingu la mawazo kwani nchi yake imebarikiwa kuwa na amani lakini kasoro ni maendeleo. Madubwana yanaiua nchi ya Mafanikio. Tatizo la nishati limezoeleka kwa wanamafanikio, kutoona umeme zaidi ya saa ishirini na nne ni jambo la kawaida lakini maji ya kutosha yapo, makaa ya mawe yapo na gesi ipo. Nani ainuke aikomboe Mafanikio, lakini iko siku atapatikana shujaa wa kuilinda na kuiinua Mafanikio.

Mwezi Oktoba ukafika Athalia na mumewe na mtoto wao Furaha pamoja na Bahati wakakwea pipa kuelekea nchini Mafanikio. Wakawasili katika uwanja wa ndege mkubwa wa kimataifa wenye jina na raisi wa kwanza wa nchi hiyo ya Mafanikio, jijini Highway. Waliwasili majira ya saa nne asubuhi kwa sababu ndege waliyoipanda ilikuwa inapitia nchini Nipe Chako kisha Mafanikio.

Walipofika jijini Highway, Athalia aliendelea na usajili wakati mume wake akiendelea na kazi ya uhadhiri katika shule ya elimu, idara ya shule maalumu. Johnson ni mtaalamu wa elimu maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kama wenye matatizo ya kuona, kusikia, ngozi, ubongo na kadhalika.

Athalia akaanza rasmi kazi ya kujifunza masomo ya shahada ya uzamivu kama ilivyoamriwa na Kitivo cha lugha cha Chuo Kikuu cha Karimiwa nchini Ukarimu. Alianza kusoma kwa kasi somo la Kiswahili katika chuo Kikuu cha Highway. Hata hivyo Athalia na Mumewe walitakiwa kuwasili nchini ukarimu katika idara zao. Gharama zote za safari na makazi zilitolewa na Chuo Kikuu cha Karimiwa.

Athalia alisoma kwa bidii katika masomo yake ya isimu. Athalia anapenda sana masomo ya sayansi ya lugha hususani fonolojia ya Kiswahili, pia somo la tafsiri na ukalimani halikubaki nyuma na Isimujamii. Masomo haya aliyaona ndiyo msingi wa lugha hivyo alikuwa na umilisi wa kutosha.

Miaka ikayoyoma, hatimaye Athalia akamaliza tamrini yake kisha akaingia kwenye utafiti ambao aliufanyia katika lugha ya kibantu iitwayo Kinyacha. Katika utafiti wake alichunguza vipambasauti vya lugha hiyo ili kupata data itayomwezesha kufanya ulinganifu na mlinganuo baina ya lugha hiyo na Kiswahili.

Athalia alitimiza azma yake baada ya kukamilisha utafiti wake akatunukiwa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Highway nchini Mafanikio. Athalia aliamini sasa ndoto zake zimetimia kilichobaki ni kuutafuta uprofesa. Hakika penye nia pana njia. Athalia alifundishwa na maprofesa na madaktari waliobobea katika somo la Kiswahili nchini Mafanikio. Si hivyo tu Chuo Kikuu cha Highway ndicho chuo mama nchini Mafanikio.

Athalia alifuzu kwa alama za juu kabisa za daraja la kwanza. Maprofesa walimpenda na aliyemsimamia utafiti wake alitamani abakie chuoni hapo lakini masikini Athalia ametumwa na chuo chake kusomea somo hilo ili akalifundishe huko Karimiwa.

Shule imeisha sasa, Athalia na mumewe wakarejea nchini ukarimu huko wakaendelea na majukumu yao kila mmoja idarani kwake. Hakika maisha ni safari ndefu mno. Athalia akaendelea kuandika kazi mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili na lugha ya Kiisilisi ambazo ndizo lugha zinazotamba duniani. Kutokana na bidii yake ya kuandika na kuvumbua vitu mbalimbali katika taaluma yake, Athalia akatunukiwa uprofesa hapo ndipo azma ya Athalia ilipotimia.

**********************************************************

**********************************************************

Maisha yakaendelea, sasa Athalia ni profesa wa lugha ya Kiswahili katika idara ya lugha za Kigeni chuoni Karimiwa nchini Ukarimu. Ana watoto wawili Furaha na Samara, wote ni wa kike na wanapendana sana kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Hakika hakuna lisilowezekana iwapo nia ikiwepo litatimia tu, na Mungu akipanga hayupo wa upangua.

Katika tufani ya mafanikio ni wengi hupoteza matumaini wanapokaribia kuyafikia mafanikio. Lakini Athalia aliishinda na hatimaye ni profesa licha ya dharuba mbalimbali alizokumbana nazo akiwa safarini kuelekea uprofesa wake na maisha ya ndoa. Sasa Athalia anafanya kazi kwa karibu na vyuo mbalimbali vinavyoshughulikia lugha duniani.