webnovel

SHIKA HAMSINI ZAKO

'Nilishayavulia ila sidiriki tena kuyaoga. Mzigo japo wangu kama nundu ya ngamia, leo sioni haja kuendelea kuubeba. Sijui niseme nimekuwa mzembe ama mizungu ishanichusha. Nataka niutue. Naam nitautua mimi.
Kuwa mke na mume ni zaidi ya kuwa baba na mama. Kuwa mke ni zaidi ya kuwa mama wa wana. Huyu, huyu ameazimia kunitoa roho. Dhamira yake ni kuniumbua kila apatapo sababu japo kiduchu. Naona mambo ya ufa na ukuta hayatambui. Yuko tayari kuliangusha jumba japo kwa kidogo ambacho angezuia.'

"Umeamua hutaongea eh" Mawazo ya Yasin yalikatizwa tena na kauli ya mkewe,sauti ya makeke. Alikuwa ashayazoea ya kila mwisho wa juma. Leo yalikuwa yamevuka kingo. Hasira zilikuwa zishaanza kumvamia. Alipokuwa ameketi, joto lilikuwa lishampanda. Mikono karibu inamtetemeka kwa hamaki.

Aling'ang'ana akashusha pumzi nzito taratibu kisha, "Naongea nasema nini. Sielewi kelele zote hizi unazileta kwa nini."
"Hunielewi eh, yaani huko kuropoka kwote mpaka sasa hujui kinacholeta ugomvi? Mbona unapenda nishinde nikijirudia?"

"Ona, kama siku zote itakuwa ni kelele huachi kutwika na kuwika, naona hili la ndoa tulitue kila mtu ajijue. Nishatamauka eti, ama wewe huku kurushiana cheche huoni kama ni utoto?"
"Swali langu hujalijibu, wewe na Cecilia mna nini. Ana nini huyo ambacho sina. Kumbe wakati niko kwetu kwa ajili ya ujauzito nawe huku unatunga vingine. Habari ninayo yote. Mara akuletee chakula, mara uende ukale, mara muombane kimotosha mpaka mnaombana vikojozi"

"Hayo ya kuombana vikojozi ni yako. Mbona unaona shida watu wakiwa na mlahaka mwema. Unakwera na madogo ambayo hayana msingi kisha unayatia hamira yanavimba yanakuwa makubwa. Ukubwa wenyeww ni wa bure! Bure bilashi."

"Najua umelala naye, hutaki kukibali ila unajua kinagaubaga ninayoyasema ni ukweli. Mambo ya kutumia mwiko mmoja na vinyangarika havijajua kuosha chupi si laiki yangu kabisa."

"Kama ni vitoto mbona basi vinakupa kiwewe. Sioni kama kuna la mno. Huyo ni rafiki tu kama alivyo rafiki kwako