webnovel

SURA YA SITA

Alikatizwa na mbisho uliosikika kutoka kwa mlango wa nje, akamwangalia mkewe, Bi. Tabasuri alivuta khanga lake akafuta machozi kisha akaelekea mlangoni kumfungulia mgeni wao.

Mlangoni alimpata Labibu amesimama, kando yake alikuwa amesimamisha sanduku lake la shule na upande mwingine godoro iliyokuwa imehujumiwa na nyaya za kitanda cha shule.

"Mshafunga shule au ndo likizo fupi?," Mamake alimuuliza baada ya kuona vitu vile. Labibu alimwangalia na kunyamaza, "ama we ni mgonjwa."

Bw. Nadama alitoka ndani kwa haraka kuja kuona yule ambaye mkewe alikuwa anazungumziwa naye. Alipofika mlangoni na kumuona bintiye, nguvu zilimwishia mithili ya mbwa mfa maji.

"Semezana nami binti yangu," mamake alimwambia kwa upole, "au we ni mgonjwa."

"Mgonjwa gani anayekuja na vitu nyumbani, au unafikiri shuleni kwao hakuna zahanati," babake alirukia kati, "huyu ametalikiwa shuleni kwa sababu ya utukutu wake."

"Huna tofauti na mwanamke, unarukia maneno kama tumbili msituni arukiavyo miti," mkewe alimkashifu, "hata huwezi kumuuliza kama yuko salama, ushafika na visababu vyako visivyojua "be" wala "te"

"Zako zinazojua ziko wapi? Unamdekeza sana huyu binti yako, hujui kwamba mchezea tope humrukia."

Labibu alipokuwa amekaa akiwasikiliza alianza kutokwa na machozi, alijihisi mkimbizi nyumbani kwao penyewe. Aliona babake anamchukua kama mtu asiyemfahamu.

"Nimekukosea nini baba?" Labibu alimuuliza akiwa amepiga magoti miguuni pake, "kama nishakukosea kwa kujua au kutojua naomba unisamehe. Lakini sikumbuki popote ambapo nishakutenda maudhi, ila kwa niaba yangu na mamangu naomba msamaha."

"Hujui makosa yako sio! Subiri nikukumbushe makosa yako, si moja na wala si mawili," Bw. Nadama alisimama akijaribu kukumbuka popote ambapo bintiye ashamkosea lakini akashindwa.

"Hebu fikiri tabia zako za shuleni, hilo si jambo la kumfanya mtu audhike?!"

"Am sorry, but it's not true."

"Unamaanisha yote yaliyosemwa ni uongo?!"

"Ndiyo."

"Utaitikia kujiondolea lawama, ingekuwa wanafunzi wenzako ningeelewa kwamba wanakuonea gere kwa sababu moja au nyingine, lakini walimu wenye akili zilizokomaa kama zangu hawawezi kufanya hivyo."

"Unasema akili yako imekomaa sio?!" Mkewe aliingilia kati, "mbona vitendo vyako ni sawa na vya kijusi katika ufuko wa uzazi."

"Usinifike utosini, nakuonya kabisa, na hii ndiyo mara ya mwisho, siku nyingine nitaongea lugha ya makonde na mateke."

***

Labibu pale alipokuwa ameketi akiangalia mto Numbi uoga ulimjaa, maji yalilalama yakipita mbele yake kwa hasira. Mto huo ulikuwa umekunja uso kama ambao ulikuwa umeghadhabishwa na kuwepo kwake pahali pale.

Aliinuka alipokuwa ameketi akaanza kuelekea pahali ambapo ulipinda, alienda kwa mwendo wa kobe mpaka pale alipokuwa amekusudia. Pale napo maji aliyaona kama yaliyomchekea kwa udhaifu wake.

"Nitarudi siku nyingine ukiwa umepunguza hasira," aliambia mto, akaupungia mkono kisha akaanza kuondoka.

Alikuwa ameinamisha kichwa, picha jinsi alifukuzwa shuleni ilikuwa mbele yake, alijaribu kujisahaulisha alivyoshauriwa na mamake lakini ikashindikana.

Aliinua kichwa kuangalia alikoelekea, lakini macho yake yakatua juu ya mvulana mmoja aliyekuwa anamjia, alipinda kona kumuondokea kisha akaanza kwenda kwa kasi.

"Ah! Labibu, usiniondokee mi' mwenzako," yule mvulana alimpazia sauti akijaribu kumfikia.

"Mi' mwenzako" , Labibu alifikiri yale maneno ambayo yule mvulana alikuwa amemwambia.

"Hebu ningoje," yule mvulana alimwambia akifikia mkono wake.

"Nipishe," Labibu alimsukuma kando kisha akaendelea na mwendo.

Mvulana waliyebishana naye alikuwa mpenziwe wa shuleni, lakini kutoka alipopata talaka shuleni Mkanya, hakutaka kuongea wala kumsikiza yeyote. Alirudi akatulia chini ya mkorosho uliokuwa umemea happy kando, alifunika uso kwa vitanga vyake, hakutaka kuonana na yeyote.

"Hebu basi nisikilize kwa sekunde kama tatu ni mwigo," yule mvulana alimuomba akiketi kando yake, "ni hatari kwako kuwa mahali kama hapa ukiwa pekee yako."

"Please Shomari, niache niishi nitakavyo," Labibu alimuomba kwa sauti ya uchungu akimsukuma kando, "if the society is seeing me as a dangerous creature, then I must be in dangerous places."

"Unako..."

"Acha nikosee, wewe endelea kuwa sawa," Labibu alimkatiza.

Shomari alisalia kuangalia mawingu, naye mwenzake akifuta machozi. Alikuwa akifikiri jambo ambalo anaweza kumwambia mwenzake angalau amuondolee huzuni na chuki moyoni lakini akashindwa, alichukua khanga aliyokuwa amekalia akamfuta machozi.

"Mara yangu ya kwanza kuongea nawe, nilijiona kama mtu ambaye anaongea na malaika," Shomari alimkumbusha mara yao ya kwanza walipokutana. Yale maneno yaliacha tabasamu usoni mwa mwenzake, kitu alichofurahia.

"What of now? Do you think you are talking to the devil?!" Labibu alimuuliza tabasamu ikiwa usoni lakini ya kuogofya.

"Unakusudia nini ukisema hayo?!" Shomari alimuuliza akimshika begani kumuondolea uoga, "naona naongea na malaika wangu wa kutoka mwanzo."

"Don't you fear me!"

"Kwa nini nikuogope, nionyeshe pembe na mkia wako, huna, kumaanisha we' ni mwanadamu wa kawaida," Shomari alimwambia kumpa tumaini, "au wewe ni kiumbe gani hapa duniani mgeni."

"Hata huoni shuleni wananiogopa; walimu kwa wanafunzi, wote mamoja. Hakuna hata wa kusimama nami."

"Hata kama wote wameondoka baada ya kusikia yale ambayo yamesemwa juu yako, mi' na we' labda kifo kitutenganishe," Shomari alimbembeleza akimkaza kifuani asione machozi yaliyokuwa yanaaza kumlengalenga.

Labibu alijiona amepata mfariji baada ya muda mrefu wa kudhulumiwa na ndimi za watu pale kijijini kwao na wanafunzi shuleni.

"Au nimesukumiwa majini!" Labibu alimuuliza, "roho za wafu zinaniandama."

Shomari baada ya kusikia maneno ya mwenzake aliangua kicheko kilichomshitua mwenzake akainuka, alicheka kwa sekunde kadhaa huku mwenzake amemwangalia kwa mshangao, kicheko kile kilimfanya Labibu akajiona mdogo na mjinga mbele ya mwenzake.

"Sasa nini unachekea?," Labibu alimuuliza akiwa ameghadhabika.

"Naichekea imani yako," Shomari alimjibu akizuia kicheko.

"Kwani wewe huamini kama ambayo nimekwambia yanaweza kuwa ya kweli? Au huamini kama kuna roho za wafu zinazoeza kuwasumbua watu hai!"

"Naamini, ila si kwa asilimia kubwa hivyo," Shomari alimjibu akifuta machozi yaliyokuwa yamemtoka, "mahasidi wakubwa wa binadamu si roho za wafu kutoka makaburini usemavyo wala si wanyama wa mwituni. Adui wa binadamu mkubwa ni binadamu mwenyewe."

Labibu aliposikia kauli ya mwenzake, alianza kufikiria maisha upya, si kama hapo awali ambapo imani kuhusu roho ilimtawala.

Shomari alipokuwa ameketi aligeuka na kumwangalia barabara usoni akitarajia kusikia neno kutoka kwake.

"Una maana kwamba huenda kufukuzwa kwangu shuleni kunahusiana na wanafunzi wengine na walimu ambao hawanitakii mema!"

"Ndiyo, lakini lazima tusahau yaliyopita tugange yajayo," Shomari alimshauri, "maishani si vyema kuishi kwa yaliyopita, haswa yakiwa ya kukutonesha kidonda, bali ni kuangalia uendako."

Waliinuka kwa pamoja wakakumbatiana, Shomari alihisi machozi yakipita mgongoni akamtoa mwenzake polepole, kisha akatikisa kichwa kama ishara ya kumkanya asilie."

"Sifirahi kuona kuona unalia," alimkatiza akifuta machozi yaliyokuwa machoni, "kwa sababu nimekuweka moyoni kama chombo cha thamani sana maishani ndo maana ukilia pia unaweka moyo wangu katika hali ya majonzi."

Labibu alimwangalia mwenzake akiwa ametabasamu, kisha wakaanza kuondoka.

"Napenda kuona tabasamu lako kwa sababu hufanya siku yangu kung'aa zaidi ya nyota angani."

Waliandamana wakizungumza mpaka penye njia panda wakasimama, Labibu hakutaka kumuachia mwenzake. Waliangaliana bila kusemezana kwa sekunde kadha, kisha kila mmoja akashika njia ya kuelekea kwao.

Shomari alianza kuelekea kwao, lakini baada ya hatua kadha alipoangalia nyuma kumwangalia mwenzake, alimuona amesimama pale walipoachana akimwangalia.

"How I wish we had not parted," Shomari alimpazia sauti.

"Hata nami vivyo hivyo."

"Naamini tutakutana, ila si katika mazingira ambayo tumekutana leo."

"Lazima tutakutana kwa sababu sisi si milima ambayo haitasonga."

"Nipe ahadi kwamba sitakupata tena mahali pale."

"I rarely give promises."

Baada ya maneno yale, waliangaliana kwa dakika mbili hivi wakabadilishana tabasamu, kisha kila mmoja akampungia mwenzake mkono na kuagana.

****

Majuma matatu yalipita kama Bw. Vura hajaizuru kampani lake, Bw. Siga alianza kuhofia moyoni kwamba huenda mwenzake alikuwa amepatwa na janga lililomzuia kumtembelea.

Licha ya kuwa alikuwa amejua doa ambalo alikuwa amemtia mmoja wa wafanyakazi wake, hakuona hiyo kama sababu kuu ya kumzuia kutembelea milki yake.

"Kweli mazoea yana taabu," Bw. Siga aliwazia akiinuka kutoka alipokuwa amekaa, "kujaribu kumbaka hirimu ya mtoto wake."

Alitoka nje kuangalia watu wake walivyokuwa wanafanya kazi, kwa ghafla kimya kilitanda kisha akaona watu wote wakiinama, bila kuuliza, alijua ni bwana Vura amewasili. Aliona wote wameinama isipokuwa Arina.

Arina alipokuwa amesimama alitamani kumrukia na kumrarua Bw. Vura vipande akashindwa, alijiona kama mawimbi ambayo hutoka baharini kwa nguvu, lakini yafikapo ufuoni na kugonga mwamba, nguvu zake huishia hapo pasi kuudhuru mwamba hata chembe.

Bw. Vura alipokuwa anapita kwenda kukutana na mwenzake, alimkonyezea jicho.

"Napenda ujasiri na ushujaa wake," Bw. Vura alimwambia mwenzake baada ya kumfikia na kumsalimu.

"Ni mfanyakazi bora kuliko wote hapa ndani," Bw. Siga alimsifu, "kazi yake huifanya kistarabu."

"Nafikiri siku kuu ya wafanyakazi ifikapo tunafaa kumzawadia, au unanishauri vipi!"

"Ni kweli usemayo, tunafaa kumpongeza."

Bw. Vura alianza kuchunguza manthari yake, kuta zilikuwa zimebambuka rangi ikaacha alama za kuchukiza, alipoangalia kiti alichokalia mguu mmoja ulikuwa umevunjika.

Mezani karatasi zilizagaa kote kuifanya ionekane kama jaa la taka. Naye alipokuwa ameketi, Bw. Siga alinyamaza kumpima mwenzake kama atasimulia chochote kuhusu kile alichokuwa ameambiwa na Arina walipokuwa pamoja mara ya mwisho.

"Amekwambia chochote kuhusu yaliyotokea kati yetu?," Bw. Vura alimuuliza kwa sauti isiyo imara.

"Nani unayezungumzia," mwenzake naye alimuuliza kujifanya hajui lengo la swali, lakini alikuwa ashang'atua palopolengwa na mkubwa wake, "nipe dira."

"Huwezi kunihadaa kwa lolote hapa ndani, chochote kitokeapo hapa wewe ndiye wa kwanza kupata taarifa hata kabla ya mtu mwingine yeyote."

"Oh! Unamzungumzia Arina!"

"Ndiyo."

"Nilipata, lakini karatasi zenyewe alizoleta nili...," alikata maneno yake akaanza kupekuapekua faili iliyokuwa kwenye mkono wake wa kulia, alisita akamwangalia mwenzake usoni. Bw. Vura alikuwa amekunja sura kama wingu lililokuwa tayari kumwaga mvua, "nimekumbuka, nilizitupa ndani ya ndoo ya taka zilizomwagwa jana."

"Now you is talking," Bw. Vura alimpa shukrani kwa kizungu.

"I know, silence is the best boat to sail in," Bw. Siga alimwambia akisukuma kando faili aliyokuwa anaangalia.

"Unaanza kukoma kiakili, si kama hapo awali ulipokuwa unajaza maskio yangu na wimbo wa haki."

"Ni kweli usemayo, hata mimi pekee yangu nikiwa mhaki sitabadili chochote nchi nzima."

"Fuata nyuki ule asali, alikwambia amemweleza yeyote!"

"Hapana."

"Basi nawe tia nta maskioni kisha upake gundi mdomoni."

Bw. Siga aliitikia kwa kichwa baada ya kusikia yale maneno, Bw. Vura alichomoa kibunda cha noti mfukoni akaweka mezani.

Mwenzake alitokwa na macho kama aliyesakamwa na kitu kooni, aliangalia nje ya dirisha kisha akakiweka kwa haraka ndani ya sefu iliyokuwa pembeni mwake.

Kitendo kile kilifanya akatokwa na jasho chepechepe, akafikiri labda ni kwa sababu in ilikuwa mara yake ya kwanza kupokea hongo ili kuficha ukweli.

"Si...i...i...wezi se...ma chochote," alimwambia kwa sauti ya kutetemeka, "itakuwa nari...b...u p...i...cha yetu na kampuni kwa jumla ma...a...choni pa umma."

"Kutetemeka kote ni kwa nini?!" Bw. Vura alimuuliza baada ya kuona kigugumizi kilichompata mwenzake.

"Sijashika pesa kiasi hiki kabla!"

"Ukifuata nyuki lazima utapata asali, isipokuwa ukimfuata kwa kumtupia vijiwe atakurudia na kukutia adabu ambayo hutasahau maishani."

Wote walicheka kwa pamoja. Bw. Siga aliinuka akafungua jokofu na kutua maji kisha akamimina ndani ya bilauri iliyokuwa mezani na kumkabidhi mwenzake.

Alitoka nje akamuacha mgeni wake akikata kiu, alienda akaketi kwenye fomu iliyokuwa nje ya ofisi akifikiri kuhusu pesa alizopewa. Hakuamini kama amepewa pesa kiasi kile.

"Ni kweli amenipa au ananipima...ni haki kweli kutomshughulikia aliyedhulumiwa...hata nikichukuwa hongo mara moja kutakuwa na madhara kweli...mambo haya yakijulikani nitaficha wapi uso wangu...na angekuwa dadangu au mwanangu katika hali hii j..."

"Unafikiri kuhusu nini?," Fikra zake zikikatizwa kwa swali la mwenzake aliyekuwa amesimama mlangoni akimtazama.

"Ah! Nilikutilia maji upate kupumzika!" Bw. Siga alimdakia mwenzake kwa mshangao.

"Hapo ndani ni kujiongezea uchovu, joto pekee limenitimua, na wewe je!"

"Ah...hakuna jambo, nimetoka nje kupunga hewa safi ya adhuhuri."

"Pesa hizo nishakupa ni zako," Bw. Vura alimhakikishia, "ila kuna jambo dogo nataka tuzungumze kabla sijaondoka."

"Lipi tena?!" Bw. Siga aliuliza kwa wasiwasi. Waliingia ndani wakafungulia kipunga upepo.

"Unamkumbuka yule kijana mkorofi aliyefika humu kunishika makoti, sio!" Bw. Vura alianza.

"Ndiyo, namkumbuka."

"Nataka tumfunze adabu. Asiyefunzwa na mamake hufunwa na ulimwengu, nami nitakuwa ulimwengu kwake."

"Hapana haja ya kumlisha kalenda," Bw. Siga alipinga maoni ya mwenzake, "usione kifushi cha jifu kinachotoa moshi ukafikiri ndani hakuna kaa la moto linaloweza kuchoma. Hakuna haja ya kuwasha moto uliokuwa unazima."

"Hayo maneno yako ndiyo yafanyayo tukapitana mara kwa mara tukiwa pamoja."

"Wewe ndiwe kichwa, nami ni mwili, nitafuata agizo lako."

"Bora ufanye nilivyokuelekeza."

"Nitaziweka hata ambapo hewa haitafikia."

Baada ya maongezi yale yasiyozidi dakika tano, Bw. Vura alimuaga mwenzake. Pale ofisini, Bw. Siga alisalia akipambana na fikra zilizokuwa zinamsumbua ubongoni."