Mwezi wa sita uliingia. Harakati za harusi zilikuwa zikikaribia kuiva. Habari zote zilikuwa zikimfikia Omuro huko alipo. Siku moja, jioni yenye mvua kali, hodi ilisikika malangoni. Walikuwa na taratibu za kutembelewa na walimu wa Omuro lakini sio kwenye saa hizo. Wasiwasi ulimfanya Omuro aongozane na wahudumu wake kwenda kufungua mlango pamoja.
Kulikuwa na watu watatu, kila mtu na farasi wake. Mavazi yao yaliwafahamisha kuwa ni wanawake. Walivaa mitandio iliyofunika nyuso zao na walikuwa wamelowana chapachapa.
"Nyie nani?", Omuro aliuliza,
"Hatimaye nimekupata.", alisema mmoja wa wageni.
Sauti yake haikuwa ngeni masikioni pa Omuro. Mgeni alivua mtandio na kujidhihirisha kuwa ni Stara. Omuro alirudi nyuma hatua chache kwa mshangao. Stara amewezaje kujua alipo na amefikaje?
Wageni wengine wawili walikuwa wasaidizi wa Stara nao walimsaidia kushuka kwenye farasi kwa umakini. Aliposimama wima, tumbo lake lilionekana. Lilikuwa kubwa, tayari miezi nane. Uso wa Omuro ulivaa swali;
"Umefikaje hapa?", aliuliza,
"Usijali, sitakaa sana.", alisema Stara, "Nimekuja kuongea na wewe. Tukaribishe ndani na utusaidie nguo kavu.",
Omuro hakujibu. Aliwaonesha ishara wahudumu wake kisha kuanza kuondoka. Wageni wao waliwafata nyuma. Walipofika kwenye chumba cha Omuro, wahudumu wao waliaacha peke yao na kuondoka. Stara na Omuro waliingia ndani.
Omuro alitoa nguo kavu kabatini na kuzirusha kitandani;
"Nina maswali mawili tu.", alisema, "Umejuaje nipo hapa na umekuja kufanya nini?",
Stara alivua mavazi yake mabichi. Alipokuwa akivaa nguo kavu, Omuro alitazama tumbo lake. Roho ya huruma ilimuingia lakini hakutaka kuonesha udhaifu. Alipomaliza kuvaa, Stara alipanda kitandani. Alikuwa akihema kwa nguvu kwa uchovu maana safari ilikuwa ni ndefu.
"Nilidhani utafurahi kuniona, lakini macho yako yananifukuza.", Stara aliongea kwa kutabasamu,
"Umekuja usiku bila taarifa _",
"Kwa hiyo nahitaji kutoa taarifa nikiwa nakuja kumuona dada yangu?",
Omuro alikosa jibu.
"Kwa nini uliondoka ikulu, tena bila kuniaga?", Stara aliuliza,
"Hatudaiani, Stara. Ulitaka tufatane kila sehemu?",
"Hapana, lakini ningefurahi kama ungenipa taarifa. Miezi yote hii nimepambana kukutafuta. Ni baada ya kumuomba sana malkia mama ndipo akanieleza. Aliniambia ukiniona utafurahi, lakini naona amekosea.",
Muda wote Omuro alikuwa amesimama pembeni ya kitanda. Aliogopa hata kuketi pembeni ya mwenzie.
"Nikwambie kitu, Omuro? Nakuelewa. Hata ingekuwa mimi ningeondoka.", Stara aliendelea.
"Huelewi chochote, Stara.",
"Naelewa, na ndiyo maana nimekuja hapa.",
"Sijui umekuja kufanya nini lakini bora usingekuja.", Omuro aliangalia pembeni akijitahidi asimwage chozi.
Stara alivuta tena pumzi, "Harusi yangu inakaribia. Tarehe yangu ya kujifungua inakaribia pia. Hizi ni siku muhimu sana kwangu na ninahitaji uwepo wako.",
"Stara, tafadhali _",
"Mimi na wewe ni kitu kimoja, Omuro. Naelewa kwanini una hasira na unataka kukaa mbali na mimi, lakini nakuhitaji. Ni bora wote wasiwepo lakini wewe uwepo.",
Omuro hakujibu kitu. Stara alitikisa kichwa baada ya kuona juhudi zake hazikuzaa matunda.
"Mimi na wasaidizi wangu tutaondoka kesho asubuhi kurudi ikulu. Tutashukuru kama utatusaidia chakula na maji kwa ajili ya safari.",
"Tawaambia wahudumu wangu.", Omuro alijibu kwa ukavu.
"Naweza kulala hapa na wewe?",
"Hatuwezi kubanana kitanda kimoja. Mimi talala chini.",
Kila neno lililotoka kinywani mwa Omuro lilimchoma Stara kama misumari. Hakusema kitu kingine. Alifumba macho na kusubiri usingizi umvae. Omuro alitoka nje.
…
Jogoo aliwika alfajiri. Omuro alifumbua macho taratibu. Alishangaa kujikuta kitandani wakati kwenye kumbukumbu zake alikuwa amelala chini. Alitizama kushoto na kulia kama Stara alikuwa pembeni yake lakini hakukuwa na mtu.
"Ameondoka?", alijiuliza mwenyewe.
Haraka alishuka kitandani na kutoka nje ya chumba chake. Ole! Nje kulikuwa pakavu, hakukuwa na tope wala tone la mvua. Muhudumu wake aliwasili na sinia ya chai. Hakutegemea kukutana na Omuro mlangoni.
"Binti mfalme.", aliinamisha kichwa,
"Wageni wameondoka saa ngapi?", Omuro alimuuliza,
"Wageni gani?",
"Stara na wasaidizi wake wawili, wameondoka saa ngapi?",
"Binti mfalme, Stara na wasaidizi wake hawajawahi kufika hapa.",
Omuro alipigwa na bumbuwazi, "Ja-jana usiku, Stara alikuja, mvua, farasi _",
"Binti mfalme, mvua haijanyesha wiki hii.",
Uhalisia ulirudi akilini na ndipo aligundua kuwa hiyo ilikuwa ni ndoto. Ilikuwa kama kweli. Tokea aondoke ikulu hakuwahi kuota ndoto kama hiyo. Alifahamu kuwa kuna kitu hakitakuwa sawa.
"Nenda kawaambie wenzio wajiandae.", Omuro alitoa amri, "Tunarudi ikulu.",
…
Mkunga mkuu, Jolani, aliitikia wito wa malkia. Jukumu lake lilikuwa kuwasaidia wanawake wote wa kifalme kujifungua. Binti aliyekuwa akikaribia ni Stara, hivyo bila shaka wito huo ulimhusu yeye.
Malkia alimkaribisha vizuri na kuamuru wengine wote watoke nje.
"Umekwenda kumuona Stara leo?", malkia aliuliza,
"Mguu huu umetoka kwake.", Jolani alijibu,
"Wanaendeleaje?",
"Wanaendelea vizuri, tunashukuru miungu.",
"Siku zake zinakaribia. Bado wiki mbili tu kama sikosei.",
"Ndiyo malkia.",
Malkia Waridi alisogeza kiti chake mbele, "Mmeshajua jinsia ya mtoto?", aliuliza,
"Hapana, ila kuna dalili za mtoto kuwa wa kiume, malkia.",
"Maskini.",
"Kwanini unasikitika? Ni habari nzuri.",
"Ingekuwa habari nzuri kama hatima yao ingekuwa tofauti.",
Jolani hakuelewa, "Nafahamu hatima ya mama, lakini mtoto ni baraka.", alihoji,
"Mimi na mfalme tulikwenda kumuona Tapa kipindi mimba ya Stara ilipogundulika. Alituonesha waraka uliozungumzia hilo swala. Waraka unasema kuwa mtoto aliyemo tumboni mwake ana damu chafu yenye kukasirisha mizimu hivyo anapaswa afe.",
"Unasema?", Jolani alishtuka, "Malkia, unasema nini?",
"Jolani, hatima ya koo zetu zipo mikononi mwa kiumbe kilichomo tumboni mwa Stara. Hivyo tusipokiua kitakuja kutumaliza wote.",
"Sasa unashauri tufanyeje?",
"Hii ni kazi yako kwani wewe ndiye mwenye jukumu la kumzalisha. Usiruhusu mtoto huyu aishi zaidi ya sekunde moja. Akiwa anatoka tumboni mwa mamaye, mnyonge shingo yake kisha useme alifariki akiwa tumboni.",
Jolani alimeza mate kwa hofu. Hakuwahi kufanya kitendo cha kikatiri hivyo tangia aanze kazi ya ukunga. Ulikuwa mwaka wake wa hamsini sasa na uzalishaji wake wote ulikuwa na mafanikio.
"Ukiweza kufanya hivi, mfalme atakupa zawadi nono. Uje na msaidizi utakayemuamini. Nakuahidi. Hakuna atakayejua kilichofanyika.", malkia alitoa ahadi.
Je, yeye ni nani akatae ombi la mfalme na malkia wa Natron?
***