webnovel

SURA YA PILI

RA YA PILI

Helena alipofika langoni pa chuo, aliwaona wanafunzi sufufu foleni wakisubiri kusajiliwa. Aliwaona wengi wao wakiwa wamevalia nyuso za tabasamu, wengine walisimama makundi madogo madogo wakipiga gumzo kwa furaha. Aliwaona mabanati wa hirimo yake wakinong'ona huku wakimwonyesha kwa kidole na kucheka. Kwa aibu, alijificha nyuma ya dereva wa mamake, akaanza kulia.

"Usilie," dereva alimkanya akimpa kitambaa cha kufuta machozi.

"Au nilivyovalia kama boya?" Hellena alimuuliza baada ya kujiangalia na kujilinganisha na kundi la wale mabinti watundu, "wananidunisha mimi."

Akiwa angali angali anazungumza na dereva wao, alimwona banati mmoja kati ya lile kundi akija kwa upande wao huku anamchekea.

"Naitwa Christabel," yule binti alijitambulisha kwake baada ya kuwafikia akimnyoshea mkono kumsalimu, "nimevipenda viatu vyako, ni vizuri."

"Naitwa Hellena," nayw alijitambulisha kwa mwenzake, "nimefurahi kufahamiana nawe."

"Nami kwa upande wangu pia nimefurahi, wale wanakuchekea kwamba wewe ni wa umri mdogo mno katika maisha haya ya chuoni."

"Kwa nini ikiwa sote tunaonekana marika!"

"Kutoka kwa mwonekano wako, you are not much exposed to the nature," Christabel alimpa sababu yake.

Hellena aliburura begi lake kumwondokea mwenzake baada ya kuhisi kwamba amedunishwa. Mambo yalienda mbio, usajili ukakamilika kisha dereva akaingia garini tayari kuondoka.

" Usiniache!" Hellena alimlilia.

"Sina budi kuondoka, Bi. Zena atakuwa na mazonge asiponiona kwa wakati," dereva alimjuza kisha akaondoka.

Alisalia amesimama pale pale kama sanamu hajui cha kufanya, alioona watu wengi kila mtu katika pilka pilka zake, wote walionekana kutomjali, akaonekana mtu aliyepotea katika dunia yake. Alionekana mtu asiyejielewa, kwa upole alianza kuondoka.

"Hi beautiful!" Alisikia sauti ya kiume nyuma yake ikimsalimu, kwa uoga akageuka kumtazama aliyemsalimu.

"We' nani?!" Hellena alimuuliza kwa sauti ya hasira baada ya kumwona yule mtanashati alivyokuwa anamkaribia kwa macho yaliyojaa tamaa kama chui anayevizia windo lake.

"Kuwa mpole dadangu eeh! Maisha ya chuo hayataki uwe na hamrere hamrere nyingi," Christabel aliyekuwa nyuma yao alimpoza kwa kumtolea tabasamu la kumkejeli.

"Ah! Mbona kwa haraka hivi Chris..." Hellena alidakia akitilia shaka urafiki wao, "umeshafahamiana na watu lukuki dakika chache tu baada ya kusajiliwa na kuingia chuoni?!"

"Hayo ndiyo maisha aise," yule kijana wa kiume aliingilia kati, "hapa chuoni lazima uwe na ukuta wa kukuzingira usiiunguzwe na moto."

Hellena alisonya akaanza kuvuta begi lake kuwaondokea, hakuwa ameshasikia historia za vyuo lakini kilichomfanya kuwaondokea ni kuwa hakuwa na uraibu wa kutangamana na ovyo haswa katika mazingira mageni kama yale.

Kwa haraka, Christabel na mwenzake walimfuata unyo unyo wakisemezana kwa sauti za chini, baada ya kumfikia, Christabel alimvuta mkono nusra aanguke chini kwa sababu ya uzito wa begi lake.

"Mishe!" Hellena alilaani akijinasua mikononi mwake, "kuna kipi cha kufanya unigandie kama kupe kwenye mkia wa ng'ombe!"

"Hapa chuoni hutokaa pekee yako, lazima utakuwa na marafiki," Christabel alimfahamisha, yule ghulamu aliyekuwa akiandamana nao alikuwa amesimama kando akibonyeza simu yake kwa madaha.

"Wakati wa kuwa na marafiki utafika, ila kwa sasa lazima nipafahamu mahali hapa kwanza," Hellena alipinga.

"Hutoweza bila mimi," Christabel alimkinai, "mazingira haya yana maudhui mengi m..."

"Hello, nimeshachangamkia mbili aisee," Christabel alikatizwa kwa sauti ya mwenzao aliyekuwa akipiga simu, "usitie shaka."

"And who is he!" Hellena alimuuliza rafikiye baada ya kusikia maongezi yale ya simu, "am already fed up with him!"