webnovel

SURA YA SITA

Johnson mtoto wa Kinguu, kidume halisi ni msiri na si mkweli hata kidogo, akiwa nchini Ukarimu alimwandikia baruapepe Athalia kumweleza jinsi anavyompenda na kumtaka Athalia aulizie gharama za kumbi za kufanyia harusi. Athalia akaulizia na kumweleza Johnson gharama zote kuanzia mahari hadi vifaa vyote vya harusi na bila ajizi Johnson akakubaliana na Athalia. Wakati wakiwa katika hatua hizo, Johnson alikuwa ametuma maombi ya kujiunga na chuo ya kusomea shahada ya uzamili nyingine bila kumwambia Athalia.

Johnson akamaliza shahada yake ya uzamili huko nchini Ukarimu, huku Athalia akitarajia kumpokea Johnson uwanja wa ndege wa mwanafalsafa maarufu Andrew Luke maarufu sana nchini Mafanikio ambao una kumbukumbu ya jina la hayati baba wa taifa hilo. Hakika usilolijua ni usiku wa giza kumbe Johnson hana muda wa kurejea nchini Mafanikio hata kwa siku chache tu. Ghafla Athalia anapokea ujumbe kutoka kwa Johnson katika simu yake ya mkononi, ukimwarifu kuhusu mabadiliko ya safari yake. Johnson alidai kuwa profesa aliyekuwa akimsimamia shahada yake ya umahiri amemwomba amsaidie kufanya utafiti nchini Mpende Jirani, kwa muda wa mwaka mzima. Athalia akahamaki, lakini aliamini pia kwamba ni kwa ajili ya manufaa ya maisha yao ya baadaye. Athalia alimshauri Johnson kwamba, amwombe huyo profesa wake mwaka unaofuata amruhusu mwezi machi ili wafunge ndoa. Johnson alikubali na kudai kuwa atamweleza Jumatatu kwani ilikuwa ni siku ya Ijumaa mwezi Agosti, 2009. Jumatatu ikafika, Athalia akapokea simu kutoka kwa Johnson akielezwa kuwa profesa amemkubalia ombi lake Johnson na kuwa ameahidi kuhudhuria harusi yao.

Athalia alifurahi sana, akashukuru Mungu bila kujua siri ya moyo wa Johnson, kwa hakika nimeamini zimwi likujualo halikuli likakwisha. Johnson akawini kumdanganya Athalia, akaendelea na shughuli zake kwa sababu Athalia yuko Mafanikio na yeye yuko Ukarimu atajua lini. Johnson akaondoka Ukarimu na kwenda nchini Mpende Jirani bila kumwaga Athalia. Athalia kila akimtafuta kwenye simu Johnson hapatikani, baruapepe hazijibiwi. Athalia akawaza moyoni na kujisemea "huyu atakuwa tayari kishaondoka Ukarimu kwenda Mpende Jirani kwenye utafiti." Kumbe Johnson hajaenda kwenye utafiti bali ameenda kusomea shahada nyingine ya umahiri. Uongo waweza kuua au kuhuisha katika mahusiano ya wawili iwapo msamaha utakuwepo baina ya wawili wapendanao, lakini kuna hatari ya kufa kwa mahusiano ikiwa msamaha utakosekana na uongo ukikithiri baina yao. Uongo huwa haudumu milele bali kuna siku utafichuka na kujitenga na ukweli.

Siku zikaendelea Athalia hapokei simu wala ujumbe wowote kutoka kwa Johnson, Athalia akaamua kwenda kutembelea baruapepe yake, huko akakutana na muujiza ulioshuka kwake, muujiza mkuu huo ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa Johnson unaosema kuwa yeye tayari yuko Mpende Jirani na kazi ni ngumu sana. Athalia akaujibu ujumbe huo kwa kutoa pole pamoja na shutuma juu ya tabia ya Johnson ya kuondoka nchini Ukarimu bila kumwambia Athalia. Hakika Johnson ni mtu wa ajabu aliondoka mithili ya mnyama asiyefungiwa kamba shingoni. Baada ya siku si nyingi Athalia akiwa kusimamia mitihani ya kidato cha nne, alipata ujumbe mfupi kutoka kwa Johnson kwa njia ya simu, akiomba msamaha kwa yale aliyomtendea Athalia. Ujumbe huo ulisema "unajua leo ni tarehe 09/09/2009, omba sana Mungu akufikishe mwaka 2010/10/10." Athalia hakujibu ujumbe huo bali aliishia kubeep.

Johnson alijua ana makosa akaamua kumpigia simu Athalia, bila ajizi Athalia akaipokea simu hiyo na kuanza kuongea. Johnson alianza kwa utani "mbona una hasira kiasi hicho, au ndo hasira za Kinyachi?" Athalia akamshambulia kwa maneno akisema "nani mwenye hasira? Mimi au wewe? Umenifanyia mambo mengi sana lakini mimi nimenyamaza tu, unafikiri sina moyo? Nimeamua kunyamaza bado tu unanitafuta eeh! Samahani sana kama huna la kuongea zaidi naomba ukate simu yako." Johnson alipogundua kuwa Athalia ana hasira sana juu yake aliamua kuwa mpole, ooooh nisamehe mpenzi, niliogopa kukuambia kama nilipata scholarship ya kusoma masters ya pili mwaka mmoja huku Mpende Jirani, nilihisi nikikuambia, utanizuia kwenda masomoni." Athalia akajibu kwa hiyo unaniona sina akili kabisa, naona una dharau sana wewe mwanaume. Anyway huwa mimi sipendi hata kidogo hiyo tabia yako ya ajabu ajabu, maana si mara ya kwanza kufanya ujinga wako ukidai mimi ningekukatalia. Kwa kuwa ndivyo unavyoniona kama mjinga nisiye na akili na mbishi basi endelea na maisha yako utampata mwenye akili." Johnson alipoona hali ni tete aliamua kukiri makosa na kuomba msamaha kwa Athalia. Athalia aliongea yote yaliyokuwemo ndani ya mtima wake kwa kirefu sana, huku Johnson akiwa amebaki kumsikiliza amalize yote. Kwa kweli Athalia alikasirika sana mithili ya simba ambaye kitoweo kimemponyoka mdomoni. Alipomaliza kuongea, Johnson alimwambia Athalia "naomba uniambie kama umenisamehe" Athalia alimjibu ndiyo nimekusamehe." Wakamalizia mazungumzo na kutakiana usiku mwema. Hakika upendo una nguvu kuliko kitu chochote duniani.

Johnson akiwa huko Mpende Jirani alimwambia Athalia aulizie gharama za kumbi, na kila kitu kinachohitajika katika suala la ndoa. Athalia hakomi kama amewahi kulizwa, akamwamini Johnson na kuifanya kazi hiyo na kumpatia jibu kijana mtanashati wa Kinguu. Kutokana na majibu ya Athalia ilionekana kwamba ili Johnson ampate mke anahitajika kutoa gharama ya fedha zipatazo milioni mbili za Kimafanikio. Johnson hakuliona hilo kama kubwa wala halina shida. Akamtia moyo Athalia kwamba hilo litafanyika mwaka unaofuata mwezi Julai.

Siku zote uhai wa mahusiano ni mawasiliano hivyo ndivyo walivyofanya Athalia na Johnson. Katika kuwasiliana kwao, mwezi Novemba wa 2009 Johnson alimtumia Athalia ujumbe kupitia simu ambao ulikuwa kitendawili kwa Athalia. Johnson alimpa Athalia masharti ambayo alifahamu fika kuwa Athalia hayawezi kwa vyovyote vile. Johnson katika kukaa kwake nchi za ughaibuni kumempelekea kujifunza mambo mengi na kusahau utamaduni wake, wa nchi yake ya Mafanikio na kuisaliti imani yake. Katika suala la ndoa kuna mambo mengi, lakini mambo ya msingi ya ndoa yanahitaji kukubaliana nayo ni mke na mume kushirikiana katika ikulu zao, ikulu zao zinaposhirikiana Athalia anaamini kuwa hata Mungu huwabariki, ndivyo Athalia ajuavyo. Zaidi ya hayo katika ushirikiano Athalia hakubaliani kabisa bali kubadili mitindo ya mechi wawapo uwanjani hilo anaafiki. Lakini kinyume na hayo ndiyo yaliyosababisha Johnson na Athalia kipenzi wake kutofautiana, kwani Johnson anataka kula tigo, kitu ambacho Athalia anaamini ni laana halifai kabisa mbele za Mungu.

Johnson alipoona kuwa Athalia ni mbishi na hataki kabisa kusikia habari za tigo, aliamua kufanya analotaka. Kumbe wakati anatoa sharti hilo kwa Athalia alikuwa tayari amempata dada mwingine aitwaye Princess, huyu mrembo walikuwa wakiwasiliana na kukubaliana kwa lolote atakaloambiwa kufanya. Wawasiliana na Johnson kwa muda kupitia baruapepe na simu. Johnson anampenda Athalia lakini wanatofautina katika suala la tigo. Johnson alipoona ushawishi wake umegonga mwamba aliamua kuachana na Athalia kwa maneno haya "Ok poa, endelea na maisha yako, mimi nataka kitu roho inapenda, waambie kwenu kuwa mi siji, tafuta mume ambaye atakubaliana na wewe." Athalia alishikwa na hasira, palepale aliinua simu yake na kumpigia mama yake na kumwambia ameachana na Johnson na wala hataki kusikia kuna ugeni uliokuwa ukitazamiwa haupo tena. Mama wa Athalia alimuuliza binti yake kwani vipi? Athalia akamjibu mama yake "wewe elewa jambo moja tu kuwa mahusiano hayapo tena baina yangu na Johnson." Mama akasema "sawa nimekuelewa mwanangu."

Siku zikapita, miezi ikayoyoma, Athalia akaendelea na maisha yake akimsubiri Mungu wake. Athalia akaona sasa wakati wa kufungua milango iliyokuwa imefungwa alipokuwa na mahusiano na Johnson umefika. Lakini wahenga husema kuwa mgaagaa na upwa hali wali mkavu, Athalia akakutana na kijana mmoja jina lake Patrick Lameck. Kijana huyu ukimwona utasema hakika Mungu anaumba viumbe. Patrick ni mweusi wa sura, mrefu wa wastani, ana umbo la mviringo na ushawishi wa hali ya juu kwani akitaka kitu hupata kutokana na ushawishi wake.

Kijana huyu alimtokea Athalia, naye Athalia aliona kuwa kijana mtanashati kamtokea alijua amempata mtu atakayemfuta machozi. Ni kweli Athalia alipata ahueni kwa kuamini kuwa Patrick ni mtu atakayetuliza mtima wake. Ehehehe! Patrick ni mtu mmoja anayefanya kazi kwa bidii sana lakini alivyo sivyo ndivyo. Athalia alifanikiwa kutulizwa mtima wake kwa siku chache tu. Patrick ni daktari katika hospitali ya Maji Marefu iliyoko wilayani Chanua. Patrick ana rafiki yake kipenzi aitwaye Paulo Mande huyu ndiye aliyemtibu Athalia alipokuwa akisumbuliwa miguu yake, kupitia tiba hiyo Athalia akafahamiana na Patrick kwani daktari Paulo alipokuwa amesafiri alimwelekeza Athalia amtafute Patrick ili amdunge sindano. Athalia alifanya hivyo na hicho ndicho chanzo cha Athalia kufahamiana na daktari Patrick.

Patrick baada ya kumdunga sindano Athalia, akamuuliza "hivi Athalia unaishi na nani?" Athalia akajibu "ninaishi peke yangu."  Patrick hakuishia hapo, akauliza tena "kwani umeshaolewa?" Athalia akajibu sijaolewa. Licha ya majibu hayo Athalia akasema hata hivyo wewe Patrick ni mdogo kwangu, Patrick aliona hapo Athalia anataka kumkata kauli asiendelee na kusudi lake. Akajitetea kwa ujasiri kama mwanaume, "la hasha Athalia mimi ni mkubwa kuliko wewe, ila Paulo analingana na wewe umri." Patrick akasema. Baada ya mazungumzo marefu Patrick akamrudisha Athalia kazini kwake kwa gari. Athalia akaendelea na kazi zake, kisha akaondoka kwenda kusahihisha mitihani ya utamilifu ya kidato cha nne, na kumwacha Patrick akiendelea na majukumu ya kazi yake ya utabibu.

Kwa kiasi fulani Athalia alihisi kuanza kupata faraja kuwa Patrick ni mtu mzuri anaweza kufaa kuwa mume wa mtu, kutokana na mwonekano wake, usemaji wake, na matendo ambayo kiuhalisia yalikuwa danganya toto. Hakika safari ya Athalia, mapenzi kwake ni ubatili mtupu kwani kila alipojaribu kugusa ni miiba, lakini Mungu wake mkuu atamjalia siku moja, atapata mume mwema kutoka kwa Mungu.

Katika hospitali ya wilaya ya Chanua huko Mpakani ambako ni kituo cha kazi cha Patrick, kuna dada mmoja anaitwa Catherine ambaye ni mkunga. Dada huyu ni mnene, mkarimu sana na amepanga nyumba moja na Athalia. Dada huyu anampenda sana Athalia anamchukulia kama mdogo wake. Catherine pia anaheshimiana sana na Patrick kama kaka na dada. Wameivana haswa, siku moja wakiwa kazini Patrick akaamua kumweleza Catherine juu ya upendo wake kwa Athalia. Patrick alianza kwa kuuliza hivi "dada Catherine hivi mgonjwa wa Paulo ana mume?" Catherine kabla ya kujibu swali alirusha swali naye "kwani vipi?" Patrick alijibu "dada yangu nahisi ni mwanamke anayenifaa." Catherine alijibu "mmmh! Mdogo wangu yule ana mchumba wake." Patrick alihuzunika na kuvunjika moyo, "basi dada kama ndo hivyo amenishinda."  Patrick alijibu, wakaendelea na kazi.      

Jioni moja wakiwa nyumbani Athalia na Catherine wanaangalia runinga, Catherine alimuuliza Athalia "vipi mdogo wangu shemeji yangu mzima? Hajakupigia simu au kutuma ujumbe?"Athalia alimjibu dada alichoniambia mimi sijakubaliana nae na hivyo ameamua tuachane, kwa hiyo wewe elewa kwamba hakuna tena mawasiliano baina yangu mimi na Johnson. Catherine alihamaki sana "hehehehe! Mdogo wangu pole sana, lakini yote hupangwa na Mungu. Halafu wiki jana tu nilikuwa na Patrick alikuwa ananiniulizia kuhusu wewe." Haaaa kuhusu mimi, alikuwa anasemaje? Athalia akauliza. Nakuambia ndugu yangu wacha ajikanyage na kujiumauma, ooo dada, lakini acha tu lakini nikambana aniambie akaniambia. Mmmh! Akakuambiaje?  Ndugu yangu akasemaje dada nampenda sana Athalia lakini mimi sikujua kama tayari mmeshaachana na Johnson kwa hiyo nikamjibu Athalia ana mchumba wake.

Athalia akiwa katika bahari ya mawazo alifika mbali sana katika ulimwengu usiofikika bali Athalia mwenyewe. Athalia akiwa katika ulimwengu wa sirini alianza kufikiri juu ya Patrick, akakumbuka alipokutana naye kituo cha bajaji alipomuuliza shemeji hajambo? Hapo ndipo Athalia alibaini kuwa Patrick alikuwa akimtaka. Athalia aliunganisha matukio mbalimbali na kauli za Patrick na kupata majibu, lakini hatujui kama Patrick ana mapenzi ya dhati.

Siku moja Athalia alikuwa anaumwa akaamua kumpigia simu Patrick ili kufahamu kama yupo kazini siku hiyo au la. Athalia alifanya hivyo kwa kuchelea kuchelewa kwenye foleni ya wagonjwa kwani alikuwa na kipindi kinachoanza saa saba na dakika ishirini. Patrick alimjibu kuwa yupo kazini kwake hospitalini, Athalia alipoona hivyo akamwambia nakuja basi muda si mrefu. Patrick alimjibu karibu utanikuta. Athalia alipofika hospitalini hakumkuta Patrick ofisini, akaamua kukaa kwenye benchi akimsubiri mlangoni pa ofisi yake. Kwa bahati nzuri daktari Paulo akatokea bila Athalia kusema neno lolote, Paulo akauuliza "Athalia mbona umekaa hapa unaumwa?" Athalia akajibu ndiyo ninaumwa na nilipokuwa nakuja niliwasiliana na Patrick kama yupo ofisini ili nije akaniambia atakuwepo lakini sijamkuta. Paulo akamruhusu aingie na kumhudumia. Akamwandikia dawa kisha Athalia akaondoka.

Athalia akiwa nyumbani akapokea simu kutoka kwa Patrick akaulizwa kama alifika hospitalini. Athalia alijibu ndiyo kuwa alifika hapo hospitalini na kwamba alionana na Paulo kwa bahati nzuri akahudumiwa. Patrick aliomba msamaha kwamba kulikuwa na mgonjwa mahuhuti alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa haraka sana hivyo aliingia chumba cha upasuaji ili kumfanyia upasuaji mgonjwa huyo na kufunga simu yake ya mkononi.  Hata hivyo majira ya jioni Patrick alienda kumtembelea Athalia na kumkuta Athalia na rafiki yake Neema wakiwa wanapiga soga. Neema alipoona mgeni aliaga na kuondoka. Patrick alikaa muda mfupi kisha akasepa kwenda nyumbani kwake.

Siku zikapita, Patrick akampigia simu Athalia, majira ya saa mbili usiku, kuwa atakuja kumtembelea, na ilipofika saa nne na nusu akatia timu ndani ya himaya ya Athalia, akiwa nje ya geti akampigia simu tena Athalia. Athalia kuona simu ni ya Patrick, akaipokea akasikia "helo niko hapa nje ya geti njoo unifungulie." Athalia alishuka ngazi na kwenda kumfungulia, Patrick kama vijana wengine akaanza kumwaga sera zake, ooooh Athalia ninakupenda sana please naomba unielewe ombi langu". Athalia na Patrick ni wabishi utafikiri wanafalsafa, walibishana mpaka saa sita usiku. Hata hivyo hawakufikia muafaka, licha ya kwamba Athalia hakumvunja moyo Patrick, lakini Patrick alitaka jibu siku hiyohiyo, ushawishi wake uligonga mwamba.

Mambo ya mapatano yakizidi kukaziwa Patrick alimuuliza Athalia ili kujua kama amepima HIV, Athalia alijibu nimepima mara kadhaa. Patrick hakuishia hapo kama askari wa upelelezi, akauliza tena "ulipima wapi, mbona sijakuona hospitali?" Athalia akamwambia kuwa alipima katika kituo cha afya cha karibu zaidi kuliko hospitali anayofanyia kazi Patrick. Patrick akakazia "wewe mwongo" ingawa alitaka kuhakikisha kwamba Athalia aende kupima katika hospitali ya Maji Marefu akampime yeye mwenyewe au yeye mwenyewe aje na kipimo nyumbani kwa Athalia ampime. Hilo Athalia halikuwa shida alikubali bila hofu, Patrick alipoona Athalia ameitikia bila tashwishwi, aliishiwa pozi kwa kuona ujasiri wa Athalia.

Mazungumzo yamenoga, Patrick bado hajaridhia anasubiri labda Athalia atabadili msimamo na kumpa jibu la ndiyo au la kama atakavyo, alisahau kuwa Athalia ni Mnyacha, Mmafanikio halisi ana kasumba za Kimafanikio, binti aliyefundwa ni lazima afikirie kwanza. Patrick aliwaza akafika mbali, kisha akauliza "au sababu hulijui kabila au dhehebu langu Athalia?" Athalia alimjibu kuwa si hivyo ingawa inawezekana. Patrick alimjibu kuwa yeye ni Mnyacha, na dhehebu lake ni Mafanikio Assemblies of God (M.A.G) pamoja na familia yake, yaani wazazi wake na ndugu zake wa kuzaliwa. Kisha akamuuliza Athalia kuhusu dhehebu lake analoabudu, bila kuchelea Athalia alijibu kuwa yeye anaabudu dhehebu la Evengelical Assemblies of God of Mafanikio (E.A.G.M). Patrick ni mbishi kwenye kundi la wabishi hakosi, alimbishia Athalia, eti kanisa hilo halipo hapa Mpakani. Sasa kazi ikawa kazi, Athalia mbishi, Patrick mbishi, wakabishana hatimaye Patrick akaona bora akubali kushindwa, maana Athalia ni mbishi balaa akijua amesimamia kweli.

Patrick ukimwangalia kwa mwonekano wa nje utajua ni mpole sana na si mwongeaji kumbe chiriku atoke nyuma. Katika kushawishi akajiona, nisije nikaponyokwa na kitoweo kilichofika mdomoni mwangu. Patrick akakazia "Athalia napenda sana kuabudu but the way people are dancing, worshipping there I don't like at all, sipendi hata kidogo, anyway lakini kwa nini hutaki kunipa jibu Athalia?"  Athalia alimjibu "nitakupatia jibu lako wiki ijayo." Patrick alilazimika kusubiri jibu kwani wiki iliyofuata alikuwa anaenda Highway kwenye harusi ya kaka yake wa kwanza. Patrick alimwomba Athalia asimjibu kwa njia ya ujumbe bali mpaka atakaporejea, wakae ana kwa ana. Athalia aliridhia.

Siku zikaendelea kutimua vumbi, Athalia kazi imepamba moto, wanafunzi nao pilika pilika za masomo haziishi. Athalia naye mara darasani mara kusahihisha mitihani ya wanafunzi. Pangu Pakavu naye yuko busy kuwakandamiza walimu, hakuna kazi watakayofanya aridhike nayo. Pangu Pakavu ni kuwafuatilia walimu kama mchunga kondoo walio zizini. Jamani hata mbuzi huruhusiwa kwenda kunywa maji lakini watumishi wa shule ya sekondari Magamba hata kwenda kununua kalamu ya kuandikia tu ni balaa. Utajiuliza Pangu Pakavu ni mtu wa kawaida au la, lakini hayo ndiyo maisha ya Athalia na walimu wenzake.

Watumishi wa shule ya sekondari ya Magamba wana desturi ya kujituma katika utendaji kazi, hata wakati wa likizo wao huendelea na ufundishaji ama kweli wana moyo, ni watu wa taifa moja la Mafanikio lakini wachache wanahenya na wengine wanakula raha. Labda wanaridhika na maneno ya Pangu Pakavu, eti ni kazi ya kujitengenezea maisha ya milele. Pangu Pakavu kweli mjanja hata hela ya kuwashukuru walimu hawa haipo. Enyi viongozi wa taifa la Mafanikio mbona walimu wafanya kazi ngumu lakini hamuwatazami? Mishahara midogo lakini kazi kubwa. Roho gani iliyomo ndani yenu, hivi tunaweza kupata mwanasiasa, daktari, mhandisi, nahodha, mwanasheria, mwanaanga, mwanamaji, na taaluma mbalimbali zinazojulikana duniani bila ya mwalimu? Kwa nini mnadharau kiasi hicho? Nesi wa ngazi ya cheti mshahara wake sawa na mwalimu mwenye shahada, Lichunguze kwa jicho pevu hilo, Mafanikio ya leo ya wasomi wenye ufahamu siyo itakayokuwepo miaka 50 ijayo. Lazima serikali ya nchi hii ilitazame kwa umakini. Usipoziba ufa utajenga ukuta na kuona kuwa una wingi wa wasomi kumbe ni pua kubwa lakini hakuna kamasi nyingi ndani yake.

Athalia anaona ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma maendeleo yake. Udadisi wa Athalia mithili ya mwanazuoni anayefanya utafiti juu ya elimu ya akili ya mwanadamu na elimu ya uchawi kwa Mwaafrika. Athalia katika ulimwengu wake wa Ghubi anatafakari sana kusudi la Pangu Pakavu na jinsi ya kuepukana na mzee huyu machachari, anajaribu kwa kila njia lakini njia nzuri pekee ni ama kuolewa au kuendelea na ratiba yake ya kwenda shule kusoma ili kutima azma ya ndoto yake ya kuwa profesa.

Ni muda wa kutuma maombi katika vyuo mbalimbali duniani kuomba nafasi ya kusoma shahada mbalimbali ikiwa ni pamoja na shahada ya umahiri na uzamivu. Athalia naye anajitosa kuomba nafasi nchini Greenland, lakini lazima aombe kwanza udhamini kwa ajili ya malipo ya ada.

Fomu za scholarship ziko mtandaoni, bila kufanya ajizi Athalia anajaza fomu hizo akisaidiwa na Johnson kwa njia ya simu, kwani Johnson alikuwa bado hajarejea nchini, lakini bahati mbaya sana Athalia anakosa nafasi. Hata hivyo Athalia hakati tamaa anavumilia, mwaka unaofuata anatarajia kuomba tena akimshirikisha mhadhiri wake bwana Maringo, ambaye hakika ni mcheshi kwa kila mtu tofauti na jina lake.

Maisha nayo yanazidi kupanda bei kwani kila kitu kimepanda bei. Athalia ana madai ya malimbikizo ya mishahara miezi sita lakini hajapata tangu aanze kazi yapata miaka mitatu sasa. Kwa kuwa Athalia ni mjasiriamali anaendelea na shughuli zake za kilimo hataki taabu kabisa, anajituma kama kichaa. Kweli siku moja Athalia atalia kivulini lakini wazo lake la kuondoka Magamba bado liko palepale. Je ataondoka Magamba sekondari? Hilo ni gumu kulitabiri lakini linawezekana.