webnovel

SURA YA TATU

Likizo ikapepea kama bati lililochukuliwa na kimbunga kikali, Athalia akajiandaa na kidato cha sita. Akaondoka nyumbani kwao na kushika njia ya kwenda Maendeleo. Wanafunzi wamerejea shuleni bila kuchelea walimu wanaanza kufundisha masomo kwa bidii wakikimbizana na silabasi. Wanafunzi nao pilika pilika za darasani mara usafi wa mazingira zimepamba moto.  Mwalimu Keneth ndiye mwalimu msimamizi wa usafi wa mazingira, hana mchezo wala masihara, mara anawachapa wanafunzi ambao hawajafanya usafi,  mara awafokee wanaofanya usafi kwa uvivu, lengo ni kufikia malengo ya shule ya kuweka mazingira katika hali ya usafi.  Ana sauti kali utamsikia akisema "hey guys! Are you playing with me? Washenzi nyie mnafikiri mmekuja kusoma tu, hapa ni kusoma na kazi tu.''

Kidato cha sita wako busy kusoma kwani maji yako shingoni, mhula wa kwanza wanajiandaa kufanya mtihani wa utamilifu. Hakika siku hazigandi, kama mshale zikatimua mbio kwa kasi, mwezi Novemba ukafika kidato cha sita wakafanya mtihani wa utamilifu. Wakati wa mitihani ya utamilifu ikiendelea Athalia Daniel akafiwa na baba yake mpendwa bwana Daniel Abija. Siku ya Jumatano asubuhi kidato cha sita wakamaliza mitihani yao ya utamilifu lakini Athalia aliambiwa na mwalimu Mkuu Msaidizi kwamba asiondoke kwenda kwenye mkutano wa GALEFEMA-MAYOMI (God's Assembly of Learner's Fellowship Mafanikio – Mafanikio Youths Ministry) uliokuwa ukifanyikia jijini Highway.

Mwalimu Mkuu Msaidizi alikuwa tayari ameshapata taarifa za kifo cha baba yake Athalia kutoka kwa kaka yake Athalia bwana Hoshea. Athalia alipoambiwa na mwalimu asiondoke akadoubt Mh! Kwa nini au baba amefariki? Anyway akajipa moyo. Mara walipokuwa assemble ikatangazwa kuwa kaka yake Athalia anamsubiri ofisini kwa makamu mkuu wa shule. Athalia akaondoka kuelekea ofisini kwa makamu mkuu wa shule huko alimkuta kaka yake Hoshea kajaa tele, wakasalimiana. Baada ya salaamu Athalia akauliza hali ya baba yake, "baba anaendeleaje?" akajibiwa kuwa baba yao anaendelea vizuri. Hata hivyo Athalia alishinikizwa aondoke na kaka yake kwenda nyumbani kwao Matamvua. Kwa kuwa ni mdogo Athalia akakubali wakashika njia ya kwenda Matamvua majira ya saa tisa alasiri.

Wakiwa safarini Athalia alijua kuwa baba yake tayari amekuwa mfu kwani ni mwota ndoto mzuri. Sanjari na hilo mkuu wa shule bwana Harold aliropoka wakiwa hostel kuwa baba yake Athalia ameshatangulia mbele ya haki.

Safari ikanoga ndani ya basi la abiria la ABC challenge, wakafika mjini Matamvua saa sita usiku. Alfajiri, mapema kabisa muda wa saa kumi na moja wakashika njia ya kwenda wilayani Chanua katika mji wa Pakanga lakini wao walishukia katika kitongoji cha Katela. Basi liliwafikisha kitongojini hapo saa moja asubuhi, Mh! Loo! Baba yake Athalia ameshakuwa marehemu siku nyingi, ana wiki sasa kaburini. Athalia kuona tuta akaanza kulia kwa sauti kubwa, wasamalia wema wakamshika na kumwingiza ndani. Mungu wangu baba yangu amefariki, kwa mbali alimsikia mamaye akisema "baba alimpa Yesu Maisha". Athalia akapunguza kasi ya kulia, baada ya muda akanyamaza akasalimiana na ndugu zake na wanajamii wengine.

Wakamwombolezea mzee Daniel Abija kwa muda na kwa taratibu za Wanyacha, msiba ukaisha. Baada ya msiba kuisha Athalia akarejea shule kuendelea na masomo yake ya mhula wa pili wa kidato cha sita. Baba ndo huyo kishatwaliwa na Mwenyezi Mungu, Athalia hana budi kupigania maisha yake na jamii inayomzunguka. Aliwaza moyoni baba yangu hakuwahi kunisaidia lakini bado alikuwa ni nguzo muhimu katika maisha yangu. Alijisemea moyoni, "hata hivyo sina budi kujipigania ili kujisimamia mwenyewe". Shule ikapamba moto matokeo ya mitihani ya utamilifu yakatoka, Athalia akapata daraja la pili, hili halikumridhisha Athalia hata kidogo. Hivyo akaamua kusoma kwa bidii zaidi ya mwanzo.

Siku zikayeyuka kama unga wa ngano ndani ya maji, mara Easter ikaingia, Athalia na wenzake wakaenda Easter Conference. Walipomaliza Easter Conference wakarejea tayari kwa mitihani ya taifa. Athalia alisoma usiku na mchana, mwezi Mei huo ukafika kidato cha sita wakaanza mitihani yao ya taifa. Wakafanya mitihani hiyo, wakamaliza, Athalia akashika njia kuelekea Kaganga kwa dada yake Hana kisha akarudi Matamvua.

Siku zikazidi kwenda mara mwalimu aliyemfundisha shule ya msingi akamwambia "Athalia sasa uolewe tu baada ya kumaliza kidato cha sita." Athalia akamjibu, "mimi nasubiri matokeo kwenda Chuo Kikuu, na nchini Mafanikio kuna vyuo viwili tu ambavyo naweza kusoma, navyo ni Chuo Kikuu cha Highway na Chuo Kikuu cha Kilimagenge." Yule mwalimu alimuuliza tena "hivi unajua alama wanazoenda nazo huko?" Athalia akajibu "ndiyo najua, ndiyo maana nakuambia hivyo."

Miezi ikayoyoma, siku zikaisha, matokeo ya kidato cha sita yakatoka. Athalia mwenyewe katafuta kazi ya kufundisha shule ya sekondari ya Apple. Hapo alikuwa na walimu waliohitimu stashahada zao nao wanasubiri matokeo yao. Mh! Wenzake wote wakapata matokeo yao lakini Athalia kila akitafuta matokeo yake hayapatikani, "dah! Inakuaje mwanangu? Au Athalia amefeli?" Wenzake walijiuliza. Salma mwenye stashahada alijitosa na kumuuliza Athalia "Athalia utakuwa umefeli mbona matokeo yako hayaonekani? Athalia akamjibu "wewe wasema, ila mimi najua nimefaulu vizuri sana." Naye dada yake aitwaye Doris akauliza "Athalia kwani vipi matokeo bado tu hujayapata?" Athalia akajibu "dada nimepata daraja la kwanza ila bado kujua pointi tu, usijali."  Doris ni mtoto wa mama yake mkubwa. Kuandamwa kwa Athalia hakukuishia hapo, mkuu wa shule ya Apple Bw. Chukua Chako Mapema alimwambia Athalia asiende kusoma mwaka huo wa masomo, na kama akikubali kubaki atamsomesha. Athalia alikataa katakata shauri hilo, kisha akampigia simu kaka yake Hoshea kumuulizia matokeo yake. Hoshea alimwambia kuwa amepata daraja la kwanza la pointi nane. Athalia alifurahi sana siku hiyo.

Matokeo hayo yalifunua ukurasa mwingine wa ndoto za Athalia, akarudi shuleni na kumwambia mkuu huyo na walimu wote kuwa amepata daraja la kwanza la pointi nane. Taarifa hizi ziliwafanya waduwae kama Chatu aliyemeza mbuzi. Makubwa! Kweli! Hee! Hongera mwaya! "Sasa una mpango gani?" Salma alimuuliza Athalia. Naye Athalia hakuchelea kuwajibu kuwa mpango wake yeye ni kutuma maombi Vyuo Vikuu ili mwaka unaofuata ajiunge na chuo. Hii ni kwa sababu katika wakati huo mitihani ya taifa ya kidato cha sita ilikuwa ikifanyika mwezi Mei na wanafunzi walitakiwa kujiunga mwaka wa kwanza vyuoni mwezi Septemba mwaka unaofuata, kwa mujibu wa utaratibu wa Mafanikio.

Siku hazigandi, wakati wa kujaza fomu za maombi ya kujiunga na vyuo ukafika, Athalia akaomba ruhusa kazini kwa ajili ya kwenda kujaza fomu za kujiunga na chuo. Athalia akaondoka kuelekea Highway, akafika na kuchukua fomu, akajaza na akarejea akipitia Kaganga kwa dada yake Hana.

Huko akakaa muda mfupi kisha akarejea Matamvua akisubiri mtihani wa Malticulation. Siku zikaenda, muda ukafika, Athalia, Lusekelo na Ayubu wakaenda kufanya mtihani wa malticulation. Sasa ni kusubiri matokeo, swali la kujiuliza nilipanda magugu au ngano? Lakini pia je wachaguzi watanichagua au la? Yote haya yalikuwa yakizunguka katika vichwa vya wanafunzi waliofanya mtihani wa malticulation.

Mwezi wa sita ukafika, matokeo ya malticulation yakatoka, wasemaji wa lugha ya Mafanikio husema kuwa "ng'ombe wa maskini hazai mapacha, hata akizaa watoto hufa." Lakini methali hii ni kinyume kabisa kwa Athalia ng'ombe wa maskini huzaa mapacha na mapacha hao huishi, kwani Athalia aliomba chuo kimoja tu na akachaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Highway, wakati Lusekelo na Ayubu walikosa licha ya kuomba vyuo zaidi ya kimoja. Watu wenye kinyongo na mafanikio ya Athalia walishindwa kumpa hongera.

Vikwazo havikuishia hapo, mwalimu wa Athalia wa shule ya msingi aliyemfundisha akiwa darasa la tatu, nne na la sita aitwaye Chalamila, alimuuliza kwa kumkejeli, "Athalia umetafuta hati miliki ya nyumba au shamba?" Athalia naye alimjibu mwalimu huyo kwa jeuri akisema; "hati miliki ataitafuta raisi Edward Martin kwa sababu huyo ndiye mdhamini wangu. Ehehehe! Yaliwashuka kama mtu aliyefumaniwa ugoni na mke wa mwenzie. Athalia akaendelea kusubiri, mbiu ikatangazwa Mafanikio kote kuwa mwaka wa kwanza wote wanatakiwa kuripoti tarehe 20 mwezi Septemba. Athalia akajiandaa hata wakati ulipotimu wa kung'oa nanga hapo kitongojini kwao katela kuelekea Highway.

Hakika mfa maji haachi kutapatapa, mwalimu mkuu wa shule ya Apple alipoona Athalia amechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Highway aliamua kumwachisha kazi kabla ya wakati kutimu. Moyoni mwake akifikiri amefanikiwa kumbe Athalia hilo hakuona kama ni tatizo bali alishukuru na kuondoka kuelekea nyumbani kwao. Hata hivyo wakati Athalia anaondoka shuleni Apple aliacha anawadai mishahara ya miezi miwili ambayo ilikuwa sawa na shilingi laki moja na elfu ishirini. Lakini Athalia ana akili hivyo alitunza pesa zake alizozipata mahali hapo kwa ajili ya nauli na mahitaji mengine. Cha ajabu mkuu wa shule ya Apple Bw. Chukua Chako Mapema alijikuta anaaibika baada ya kuona Athalia anaendelea kunawiri huku akiendelea na shughuli za shamba.

Muda ukafika, Septemba hiyo tarehe kumi na saba (17) Athalia akaondoka Matamvua akielekea mkoani Mtamani kwa kaka yake Hosea. Tarehe 18 akafika mjini Mtamani, siku iliyofuata akaanza safari ya kwenda Highway, akasafiri siku nzima na jioni akawasili Highway huko akisubiriwa na rafiki yake Joanita Raphael. Athalia akapokelewa na Joanita na kuelekea Lamala ambako ni muda wa nusu saa kufika kutokea stand kuu ya Offside ya jijini Highway. Walipanda basi maarufu kwa jina la daladala pamoja na mizigo yao. Wakafika nyumbani, Athalia alipokelewa vizuri sana na hakujiona mpweke tena. Athalia alikumbuka jinsi wana GALEFEMA walivyompa rambirambi ya shilingi elfu arobaini alipokuwa amefiwa na baba yake, tangu hapo aliamini kuwa amepata ndugu.

Joanita ni mkarimu pamoja na wazazi wake, kwa umbo Joanita ni mrefu wa kawaida, mwimbaji, ana uso mwembamba na umbo lake ni la wastani. Joanita alimwandalia Athalia maji ya kuoga, baada ya Athalia kuoga wakala chakula. Baada ya hayo Athalia aliwakabidhi mizigo aliyokuja nayo. Usiku ukaendelea wakamshukuru Mungu wao kisha wakaenda kulala.

Asubuhi imeingia ni siku mpya, Joanita na Athalia wakashika njia ya kuelekea Chuo Kikuu cha Highway, kwani Joanita alikuwa akifanya kazi mahali hapo. Walipofika chuoni hapo kila mmoja aliendelea na pilika zake. Athalia yuko busy kujisajili kama mwanafunzi, mara akapige picha ili apate kitambulisho cha uanafunzi, mara kushughulikia chumba cha kulala, mara kuchukua ratiba ya masomo. Hadi jioni Athalia kachoka mithili ya mbwa kichaa. Joanita baada ya kumaliza muda wake wa kazi alimtafuta Athalia lakini bila mafanikio kwani Athalia alikuwa yuko kushughulikia chumba cha kulala. Athalia alipomaliza alirejea nyumbani huko alimkuta Joanita ameshafika mapema, wakaendelea na ratiba ya mambo mengine.

Wiki ikapita Athalia akasajiliwa, akapatiwa kitambulisho cha uanafunzi, akapatiwa chumba Hall Three (III) chumba namba 123. Maisha ya shule yakaanza rasmi kwa kasi ya ajabu.

***************************