webnovel

SURA YA NANE

Athalia alipomaliza na kutunukiwa shahada yake ya umahiri, mumewe Johnson aliondoka kwenda kusoma shahada ya uzamivu nchini Ukarimu. Athalia anampenda sana mumewe na anapenda elimu hivyo alimruhusu mumewe aende kusoma. Baada ya miezi sita Johnson aliamua kufanya makazi nchini Ukarimu kwa kumshirikisha mkewe katika mchakato wa kufanya makazi nchini Ukarimu. Semista ikaisha, Johnson akarejea nchini Mafanikio, alikuta Furaha usemaji umekuwa mara dufu.  

Kama ilivyo ada ya mwanaume tangu enzi za Adamu na Hawa, Johnson alipofika nchini Mafanikio alianza mchakato wa kutafuta pasipoti ya mkewe pamoja na Bahati mfanyakazi wao. Ama kweli Johnson anaishi katika maadili ya wazazi wa ulimwenguni kwani vijana wa sasa na wanaume wengi utawasikia hamsini hamsini. Eti ni ulimwengu wa haki na usawa kwa jamii. Ama kweli usawa huu naamini unapatikana katika taaluma ya elimu na kazi za ofisini, lakini biolojia ya Mungu na majukumu ya familia hakuna kitu usawa. Tangu lini Tembo akabeba mimba ndani ya miezi tisa? Au ng'ombe kuzaa ndama watano kwa mimba moja? Binadamu wa leo yuko busy na usawa katika jamii lakini Mwanaume hawezi kusafiri kila mwezi, hawezi kunyonyesha, hawezi kubeba majukumu ya mwanamke, wala mwanamke hawezi kubeba majukumu ya mwanaume yote zaidi ya yale ya kusomea darasani. Wanawake ni mashujaa lakini mipaka ya kibiolojia ni sehemu ya utamaduni na dhamira ya Mungu kumtofautisha mwanamke na mwanaume.  

Ndani ya miezi mitatu Athalia na Bahati walikuwa wameshapata pasipoti za kusafiria. Bahati ni binti mzuri na ana roho njema kwa watu mbalimbali. Athalia anampenda sana kwani wanaishi kama ndugu. Wazazi wa Bahati waliwapenda sana Athalia na mumewe, kwa jinsi walivyoonesha upendo mkubwa kwa Bahati. Athalia na mumewe walipopeleka ombi la kuondoka na Bahati kwenda kuishi nae ughaibuni wazazi wa Bahati waliridhia bila ajizi. Mnamo tarehe 27 mwezi wa Kenda walianza maandalizi ya safari. Mwezi uliofuata wakasafiri kwenda nchini Ukarimu.

Athalia na Bahati masikini ni mara yao ya kwanza kwenda nchi za ughaibuni, walizoea nchi yao Mafanikio. Safari zao zilikuwa ni Matamvua, Kaganga, Highway nakadhalika. Bahati yeye safari yake ilikuwa moja tu kutoka Matamvua kwenda Highway, lakini sasa Mungu amemhuluku, anakwenda nje ya nchi sawa na jina lake, kweli jina la mtu linabeba matukio ya maisha ingawa si yote.

Katika safari yao walipitia nchi ya Nipe Chako kisha wakaelekea nchini Ukarimu yenye mji mkuu wake uitwao Karimiwa. Athalia ni rafiki yangu mkubwa, nikikumbuka tukiwa shule ya msingi alikuwa akiniita Dorine, sasa huyo hata nchini hayupo. Hapo ndipo ninajifunza kuwa kama siku zisivyofanana hata binadamu hatufanani. Mimi nimebaki na ualimu wangu nchini Mafanikio lakini hata maendeleo hakuna.

Miaka kadhaa iliyopita nazikumbuka ndoto za Athalia kuwa yeye hawezi kuendelea kuishi katika dimbwi la Sahau bila kuona mabadiliko katika maisha yake. Athalia alikuwa na ndoto za kuwa mtu fulani katika siku za mbeleni. Siku moja aliniandikia barua nikiwa shuleni kwangu Burutwa ikisema:

        Athalia Daniel

S.L.P 103,

Chanua,

Matamvua.

25/ 09/ 2007.

Kwako rafiki Mpendwa wangu Dorine Abel,

Ni matumaini yangu kuwa u mzima wa afya njema na Mungu anazidi kukutetea. Mimi sijambo namshukuru Mungu.

Lengo la barua hii ni kusema machache yaliyo ndani ya mtima wangu. Mimi na wewe rafiki yangu muhibu ni wana Mafanikio lakini nchi yetu haitujali kabisa, mimi ninaidai serikali shilingi milioni mbili za Mafanikio (2,000,000/=MSHS). Hizi ni malimbikizo ya mishahara yangu, tangu nianze kazi hadi hii leo.

Nimeona nikushirikishe rafiki muhibu wangu, kwa sababu mishahara ni haki yangu, lakini nchi yangu hainijali bali inakumbuka sana kunikata kodi kubwa mshahara wa laki mbili na nusu kuliko wanaotuibia raslimali zetu za madini, nishati na kwenye utalii. Bodi ya mikopo ya elimu ya majuu ya Mafanikio nayo haijakaa mbali na msumeno wake, nimeona sitakaa nitoke kwenye shimo hili la maradhi ya umasikini.

Muhibu Dorine nimeona sina jinsi bali lazima nivae kodrai kwa kwenda shule kusoma ili niondokane na adha hizi, lakini pia najishughulisha na kazi mbalimbali za mashamba. Hili nimeona litakuwa ufumbuzi kwangu katika kujikokota kung'oka kwenye shimo la maradhi ya umasikini. Sijui wewe unafikiriaje? Mimi mwaka huu nimeomba nafasi ya kusoma shahada ya umahiri.

Kwa kuhitimisha nakushauri rafiki yangu uwe na miradi mingine ili kuondokana na dhana ya ualimu ni umasikini.

Ndimi wako Muhibu

A. Daniel

Athalia Daniel.

Barua ya Athalia ilinifikisha mbali sana katika ulimwengu wa mawazo. Lakini nikajikuta siwezi kufanya lolote kwani nina watoto mapacha, mume wangu ni mlevi wa kupindukia ilibidi niridhike na hali niliyo nayo.

Sasa nabaini kuwa Athalia alikuwa sahihi na mume wake ni mwelewa, kwa sasa wako nchini Ukarimu wanaishi maisha mazuri. Athalia akiwa huko aliniambia kuwa anafanya kazi katika chuo Kikuu cha Karimiwa yeye akiwa katika Kitivo cha lugha za Kigeni, upande wa Kiswahili. Mume wake yeye yuko idara ya elimu maalumu.

Athalia ni mkuu wa idara ya lugha ya Kiswahili nchini humo. Athalia alipofika nchini humo alianza kufundisha lugha hiyo katika chuo Kikuu cha Karimiwa. Baada ya miaka miwili mkuu wa Kitivo cha lugha za Kigeni katika chuo hicho aliitisha kikao na kukaa na wanakitivo wote.  Profesa Hyman Meinholf alikuwa na ajenda ya kumpeleka Athalia nchini kwake akasome shahada ya uzamivu. Kitivo kilikubali azimio hilo kwa sababu Athalia alikuwa na umilisi katika lugha hiyo.

Athalia alirejea nyumbani kwake na kumweleza mumewe yaliyojiri katika kitivo chao. Habari za Athalia zilimfurahisha Johnson lakini zilileta simanzi moyoni mwake. Johnson alishazoea kuwa na mkewe kwa muda sasa wa miaka mitano, jambo la Athalia kwenda masomoni ni la heri lakini lina simanzi ndani yake kwani linawatenganisha wapenzi. Johnson alijiuliza kwa nini wamefanya hivyo? Athalia akadakia kama vile mbuzi avamiavyo bila ishara yoyote, "hata mimi sikuelewa ajenda ilipoanza, lakini madai yao ni kwamba wanataka mkuu wa idara ya Kiswahili awe na shahada ya uzamivu. Johnson aliamua kuwa mpole kama kondoo aendaye machinjioni, lakini nafsini mwake akaazimia kwenda kumwomba mkuu wa idara yake amruhusu akafanye kazi miaka mitatu nchini Mafanikio katika Chuo Kikuu cha Highway ambako ndiko mkewe anatarajiwa kwenda kusomea shahada yake ya uzamivu.

Baada ya weekend kuisha Johnson alitia timu ndani ya ofisi ya mkuu wake wa kitivo, Profesa Henry Gregory. Profesa Greygory alimtazama Johnson kwa muda kisha akamuuliza what is wrong with you Dr. Johnson Paschal? Johnson alimjibu my dear professor, my wife Athalia Daniel has got a scholarship for further studies (PhD)! Prof. Akauliza where? At my mother country Mafanikio, Johnson alijibu. Greygory aliuliza tena now why you are so sad like that? Johnson alijibu my wife will be far from me for a moment that's why I'm sad! Gregory alipogundua hilo kuwa Johnson anampenda sana mkewe kama mwanasaikolojia akatambua kuwa Johnson yuko katika wakati mgumu kimawazo.  Greygory akauliza tena what do you want for this situation? Johnson bila kufanya ajizi alijibu "professor I request you to give me a permission from your office for three years to work at Mafanikio until my wife completes her PhD studies.

Greygory kwa muda alikaa kimya, baadaye akamjibu Johnson kwamba 'it is possible, but we need to clear something first through having meeting which will give the final decision on it. Baada ya juma moja Greygory na wenziwe wakakaa kikao ambacho kiliridhia Johnson aende Mafanikio kama expert katika chuo Kikuu cha Highway wanakitivo walikubaliana kuwa Johnson atakaa huko kwa muda wa miaka mitatu. Greygory aliufikisha ujumbe kwa Johnson na kumweleza "we have accepted your request but you will be in Mafanikio Country at Highway University as an expert in the department of Special Need Education" Alisema Prof. Greygory. Johnson alishukuru sana kwa furaha isiyo kifani kwani haja ya moyo wake Mungu ameisikia. Greygory aliuliza tena, Oooh! Dr. Johnson when is she expecting to join? Akajibu kwa haraka, next year prof. Greygory. Mambo yakawa mambo, Johnson akaagana na profesa Greygory, kila mtu akaendelea na shughuli zake.

Jioni imewasili kila mtu kamaliza majukumu ya siku, Johnson anarejea nyumbani kwake, anamkuta Athalia siku nyingi aliwasili nyumbani na kuandaa chai ya jioni. Johnson kabla hata hajaingia ndani alianza na mbwembwe zake mithili ya sungura kwa mwenyeji wake. "Hello my love, life has changed completely you can't imagine it" alisema Johnson. Kuna nini mwenzangu? Athalia aliuza. Mpenzi wangu, profesa Greygory na wanakitivo wamekubali ombi langu. Athalia alihamaki! Kweli! Johnson unashangaa nini habari ndo hiyo mama, nitaandikiwa barua ya kwenda kufanya kazi chuoni Highway kwa miaka mitatu as an expert. So tutakuwa wote mpaka utakapomaliza Ph.D yako. Athalia alifurahi kwa sababu sasa mumewe kafanikiwa ombi lake, lakini zaidi ni uhai wa ndoa yao utaendelea kuimarika.

Athalia aliingia jikoni tayari kwa maandalizi ya chakula cha usiku mezani. Akiwa huko jikoni bila kujua mtu huyu hapa, Athalia alijua ni Furaha anayeingia bila hodi, akaendelea na shughuli zake, ghafula alikuta mtu kamfumba macho. Athalia alipoona hivyo alijua huyu si Furaha tena ila ni mumewe. Athalia akasema bwana mwenzio nitaunguza darling! Johnson alijibu utaunguza vipi wakati mie nipo? Haya dear! Najua umekuja ili unisaidie kupika au sio sweetie wangu? Exactly my love! Nataka leo tupike wote, alijibu Johnson.

Katika harakati za kupika baba na mama wakiwa jikoni huku wakiendelea na mikakati yao ghafla Furaha huyu hapa! Baba Furaha, ooh my daughter! How are you? I'm okay dady!  Furaha alijibu. Do you want some juice? Furaha alijibu no dady, I've taken it, I need rice. Mama Furaha alidakia, worry not my daughter soon you will've it, but go back to your nun Bahati. Okay mumy! Furaha akaondoka kwenda kwa Bahati. Baba Furaha anamwambia mkewe, Furaha ni mtundu sana na anaonekana ana akili sana au siyo? Mama Furaha; kweli ni mtundu sana lakini bado mapema sana. Anyway! Lakini huwa unamfundisha kuongea Kiswahili? Athalia alijibu ndio namfundisha sana, jaribu kuongea naye uone kama haongei Kiswahili. Tatizo ni wewe mwenyewe kila ukifika ni Kiingereza tu. Okay sweet nimekuelewa. Baba Furaha aliita, Furaha njoo! Furaha nakuja baba, mama Furaha akahoji, umeona sasa.

Furaha, "nimekuja baba unasemaje"? Baba Furaha: "nilitaka kukuuliza kama shuleni wanakusumbua au la." Hapana baba wakinichokoza nawapiga, nina nguvu baba, Furaha alijibu. Baba Furaha: vizuri sana mwanangu. Furaha akaita baba! Johnson aliitika naam mwanangu, unasemaje? "Jana Clinton alinichokoza, nikamwambia mwalimu, Clinton akinichokoza tena nitampiga." Furaha alisema! Sasa mwalimu hakukasirika? Aaah! Hapana baba, ila alimwonya tu Clinton aache uchokozi. Johnson alibaini kuwa mwanae anaweza kuzungumza lugha ya Kiswahili vizuri. Athalia akadakia, Furaha mwanangu naomba uende sebuleni kwa dada Bahati umwambie aniletee hotpot. Sawa mama naenda, nikimwambia tuje wote? Baba Furaha alidakia wewe baki huko, sasa hivi atarudi.

Bahati akaingia jikoni na kuchukua chakula na kukipeleka sehemu ya maakuli. Athalia na mumewe wao bado wako jikoni. Furaha ni mjanja mithili ya nyoka, alipoona wazazi wake hawaji mezani aliwafuata jikoni, "mama mimi njaa inaniuma." Furaha alimwambia mama yake. Athalia akamwambia: tangulia basi, sasa hivi nakuja. Furaha "siendi mimi, twende wote." Baba Furaha alipoona hayo aliinuka na kumwambia mkewe, twende dear! Huyu ana njaa si unamjua? Wakainuka na kuelekea mezani. Furaha akapewa chakula chake, wote kwa pamoja wakaanza kula.

Baada ya chakula, Athalia alimpeleka kulala Furaha chumbani kwake na kumuaga Bahati. Furaha kama kawaida saa mbili na nusu yeye ndo muda wake wa kulala. Athalia alihakikisha mwanae amelala, ama kweli ulezi kazi, kulea mwana kibarua kizito lakini si kulea mimba. Athalia kila siku lazima ahakikishe Furaha kalala naye ndipo alale. Mara nyingi husaidiana na mumewe hukaa na mtoto wao chumbani kwake, akishalala humwacha nao tayari kwenda kulala. Mara zote wako bega kwa bega kama kumbikumbi.

Akishalala Furaha nao hupata nafasi ya kupumzika chumbani kwao. Wanaishia usingizini huku wakiwa na maongezi lukuki juu ya maisha yao na familia yao. Ama kweli maisha ni mipango kila siku, ni kupanga na kupangua.

*******************************************