webnovel

STARA 7

Stara alipomaliza kunywa chai alipanda kitandani. Kila asubuhi na jioni alikuwa akitembelewa na mkunga mkuu ili kuona maendeleo ya mtoto. Tumbo lilikuwa kubwa na kilo zilikuwa zimeongezeka. Miezi ile nane ya ujauzito wake ilikuwa migumu kimwili, lakini furaha aliyokuwa nayo ilizidi machungu yote. Alitamani kumuona mwanaye hata dakika hiyohiyo. Lakini kama aliweza kuvumilia miezi nane, wiki mbili si kitu.

Jolani aliwasili na wasaidizi wake wawili. Walikuwa ni wanafunzi walioko siku za mwisho za mafunzo yao ya ukunga. Mmoja wao alikuwa binti wa Jolani wa kumzaa; jina lake lilikuwa Aisha.

"Umelalaje usiku wa leo?", Jolani alimuuliza Stara huku akipapasa kiganja chake kusikiliza mapigo ya moyo.

"Nimelala vizuri.", Stara alijibu,

"Maumivu?",

"Yapo, ila ya kawaida tu.",

Aisha alifungua vifungo vya gauni ya Stara na kuliacha tumbo wazi. Jolani alitoa kichupa cha mafuta na kumpaka juu ya tumbo lake huku akilikanda kwa makini. Alimhisi mtoto akichezacheza. Stara alicheka kidogo.

"Siku hizi ameongeza kucheza.", alisema,

"Siku zake zinakaribia, yupo anajigeuza.", Aisha alimweleza.

Jolani alimgeukia yule binti wa pili;

"Nimesahau kubeba maji ya mchaichai. Naomba urudi kibandani ukanichukulie. Yapo juu mezani.", alimtuma,

"Sawa, mkunga mkuu.",

Binti yule aliondoka mbio. Sasa hali ya hewa ilibadilika ndani ya chumba kile. Tabasamu lilipotea usoni mwa Jolani.

"Mtoto wako yupo hatarini.", Jolani alimjuza Stara.

Aisha alikwenda kusimama mlangoni kwa machale ili kuzuia mtu yeyote asiingie. Huku Stara alipigwa butwaa.

"Umegundua chochote kwenye vipimo?", alimuuliza mkunga,

"Hapana. Mtoto wako kiafya na kimwili yupo vizuri, naongelea hatima yake baada ya kuzaliwa.", alisema Jolani, "Takusimulia kitu. Naomba unisikilize kwa makini.",

Stara alikalishwa kitako.

"Zamani za kale, mamia yaliyopita, himaya yetu ilikuwa ni kijiji kimoja kikubwa kisichokuwa na kiongozi yeyote. Migogoro ilikuwa mingi maana kila koo ilitaka iwe kichwa, si mkia.", Jolani alisimulia, "Siku moja baba na watoto wake wawili walikwenda msituni kuwinda. Kwa bahati mbaya walizama kwenye shimo refu lililowapeleka pasipojulikana. Huko walikutana na mizimu.",

Stara aliweka mikono tumboni maana hadithi ilianza kumtisha.

Jolani aliendelea, "Ili kuokoa maisha yao, mizimu iliwapa kitendawili kigumu. Kwa bahati nzuri yule baba aliweza kujibu. Mizimu ilifurahishwa naye na kumuahidi kuwa yeye na ukoo wake utaibuka na kuwa viongozi wa himaya. Lakini sharti lilikuwa ni moja; kwa kuwa mizimu ndiyo iliyoanza kukalia ardhi ile kabla hawajaamia, ili wao waendelee kuwa viongozi na kuishi kwa amani, itabidi sadaka iwe inatolewa kwao kama njia ya kulipa deni la milele.", 

"Sadaka gani?", Stara aliuliza kwa woga, "Watoto?"

Jolani alitikisa kichwa, "Hapana, sio watoto, bali wake wa kwanza wa kila kijana mwenye damu ya kifalme ndani yake.",

Stara alishtuka nusura moyo uruke nje ya kifua. 

"Kwa vizazi na vizazi, sadaka hiyo ilitolewa na itaendelea kutolewa. Unakwenda kuwa mke wa kwanza wa Bazi. Hatima yako imekwishaandikwa.",

"Hapana.", Stara aliweweseka, "Bazi ananipenda. Hawezi kuruhusu nife.",

"Hivi unanielewa, Stara? Hauna familia wala pa kukimbilia. Damu yako imeshachaguliwa na mizimu kama sadaka hivyo hakuna sehemu utakayoweza kujificha. Isitoshe, mtoto wako anatakiwa kuuawa.",

"Nini?", Stara alisisimuka mwili. Machozi yalimtoka, "Mwanangu amekosa nini?",

"Makuhani wametabiri kuwa damu ya mwanao itawaletea majanga makubwa kama isipomwagwa. Nami nimepewa kazi ya kukinyonga kichanga chako pale tu kitakapotoka kwenye tumbo lako.",

Stara alijikunyata kwa woga. Alihisi kuwa Jolani alikuwa amekuja kukamilisha kazi. La hasha! Halikuwa lengo lake hata kidogo.

"Usiogope, Stara. Hatujaja hapa kukuumiza. Ukweli ni kwamba maisha yako hayawezi kuokolewa lakini ya mwanao yanaweza.",

"Wewe ni mama, Jolani.", Stara alizungumza kwa sauti ya chini, "Nipo radhi kufa, lakini mwanangu awe salama. Mtoto wangu hana damu chafu. Hastahili kuuawa. Wataniua mimi, siyo mwanangu. Naomba unisaidie.",

"Ndiyo maana nipo hapa.",

Jolani alitoa kichupa mfukoni mwake. Ndani kulikuwa na maji rangi ya kijani.

"Haya ni maji ya uchungu.", alimweleza Stara, "Mtoto wako yupo tayari kutoka. Tarehe yako rasmi ya kujifungua ni wiki mbili zijazo. Fahamu za kila mtu ikulu zitakuwa zimesimama hivyo itakuwa ngumu kwangu kufanya kinyume na maagizo.",

Alimkabidhi kichupa.

"Lakini ukijifungua leo usiku, hakuna ambaye atategemea. Tutakuwa peke yetu na tutaweza kufanya ujanja.", Jolani alimwambia,

"Ujanja gani?", Stara aliuliza kwa hamasa,

"Kuna mwanamke ametoka kujifungua leo asubuhi ila kwa bahati mbaya mwanae amefariki. Imemuharibu saikolojia yake, hataki kukubaliana na ukweli. Hivyo ukijifungua, tutamchukua mtoto wako na kumpeleka kwake, kisha maiti ya mwanae tutakukabidhi wewe. Familia ya mfalme ikijua kuwa umejifungua na mtoto amefariki hawatahoji maana ndicho kinachotakiwa kufanywa. Mwanao atakuwa salama.",

Stara alimeza fundo la mate na kukaribisha wazo lile ubongoni, "Mimi nifanyeje?", aliuliza,

"Usiku mzito ukiingia, kunywa hichi kichupa kizima. Uchungu utakushika. Mimi na Aisha tutakuwa karibu na maiti ya kichanga. Wahudumu wako wakija kutuita tutafika mapema na kukusaidia. Habari zitachukua muda kuifikia familia ya mfalme. Watakapowasili kwenye makazi yako, kila kitu kitakuwa kimekamilika.",

Stara alifuta machozi na kupiga moyo konde. 

"Nakuamini, Jolani.",

"Sitakuangusha, konsoti Stara.",

Binti aliyetumwa maji ya mchaichai alirudi, na kila kilichopangwa kuongelewa kilikuwa tayari kimeshaongelewa. Sasa yalibaki matendo.

Ilipokaribia usiku wa manane, Stara aliambatana na wasaidizi wake kwenda madhabahuni kusali. Ilikuwa ni kawaida yake. Aliamini kwamba kwenye usiku mnene, wote wakiwa wamelala, masikio ya miungu ndio huwa wazi, hivyo sala zake hupokelewa na kusikilizwa vyema. Lakini siku hiyo ilikuwa tofauti. Alikwenda akiwa na dukuduku zito kooni. Ilikuwa kinaya; ikulu ilijaa makuhani, madhabahu yaliheshimika kuliko kiti cha mfalme lakini nyuma ya pazia vyote vilikuwa unafiki.

Makuhani hawakuwepo kuiabudu miungu bali kuwakilisha mizimu. Hakuna hata mmoja aliyekuwa wa kweli. Wote waliabudu ushetani. Chimbuko zima la ufalme na viongozi wote liliimarishwa na damu za mabinti kama yeye zilizomwagwa bila hatia, bila kujua. Lakini Stara hakuwa hapo kujiombea yeye.

Wasaidizi wake walisimama nje ya malango na kumwacha Stara aingie mwenyewe. Alijongea madhabahuni na kupiga magoti. Kabla kauli haijatoka kinywani mwake alianza kulia kwa uchungu. Hakukuwa na mtu wa kumuhukumu, aliumwaga moyo wake mbele za miungu.

"Ni nini hiki?", aliongea kwa sauti ya chini, "Ni kama hadithi mbaya na ya kutisha. Miaka yote nilidhani mfalme aliniokoa toka mpakani, kumbe niliruka majivu na kukanyaga moto. Nakwenda kutolewa sadaka mimi kama kondoo na nimekubaliana na hatima yangu.",

Alifuta machozi na kuendelea;

"Lakini mwanangu hana hatia yoyote, hana kosa. Siamini kama anastahili kunyongwa kama mhalifu. Nipo hapa kuomba mnisaidie. Mimi siamini mizimu bali nyie. Kitendo tunachokwenda kufanya na Jolani ni hatari, na ikigundulika wote tunakwenda kupoteza maisha. Nitangulieni. Muepusheni mwanangu na balaa. Yaokoeni maisha yake. Hiki ndicho kitu changu cha mwisho kuwaomba.", 

Stara aliingiza mkono katikati ya maziwa yake na kutoa kichupa alichopewa na Jolani. Alikifungua na kukinywa chote. Alikunja uso kwa uchungu wa maji yale lakini ladha ilipotea baada ya muda mchache.

"Kama uhai wa mwanangu utaleta janga kuu kwa familia nzima ya mfalme, na ikawe hivyo.".

Alinyanyuka na kutoka nje. 

Walipokuwa njiani kurudi kwenye makazi yao, Stara alihisi maji yakichuruzika mapajani. Alijua wakati umefika. 

"Naomba mmoja wenu akamuite mkunga mkuu. Mwambie mfuko umepasuka.", alisema.

Wahudumu wake hawakutegemea kwani ilikuwa bado mapema. Mmoja aliinama na kuanza kumkagua Stara mapajani. Macho yalimtoka baada ya kugundua kuwa ni kweli. Alitoka mbio kuelekea nyumbani kwa mkunga. Waliobaki walimuwahisha Stara chumbani kwake na kuanza kumuandaa.

***