webnovel

MAONO

Aera, binti wa Heya, alikuwa njiani kuelekea shambani. Kichwani alibeba chungu cha mihogo ya kuchemsha. Alikuwa miongoni mwa mabinti warembo sana kijijini kwao. Alipenda kila mtu bila kubagua. Alikuwa furaha ya familia yake.

Himaya ya Natron ilitenganisha watu kutokana na uchumi wao. Uchumi wa juu ulikaliwa na viongozi wa ikulu. Uchumi wa kati ulikaliwa na wafanya biashara. Uchumi wa chini ulihusisha wakulima, wavuvi na wafanyakazi wa ndani. Familia ya Aera ilikuwa ni ya wakulima hivyo walikuwa masikini.

Akiwa njiani, Aera alikutana na Pim, jirani yao. Familia yake ilikuwa ya wavuvi. Pim na Aera walikuwa umri mmoja, miaka 25. Urafiki wao ulianza tangia wadogo. Pim alianza kumpenda Aera kimapenzi kuanzia miaka ya nyuma, lakini kwa bahati mbaya, Aera alikuwa na malengo ya kuolewa na watu wa uchumi wa juu yao ili aweze kuikomboa familia yake. Tofauti na hayo, bado Aera alimpenda sana Pim kama rafiki. Walikuwa na ukaribu ambao wengi waliuonea wivu.

"Wahi shambani. Wenzako wana njaa.", Pim alimtania Aera.

Yeye pia alikuwa akitoka ziwani kurudi kwao. Alikuwa kabeba ndoo mbili.

"Usiniongeleshe, nimeshachelewa.", Aera alisema huku akiongeza mwendo.

Pim aliweka ndoo chini na kuziba njia ya mwenzie, "Nimetoka kuchoma samaki wa kuuza. Nikupe mmoja?",

Aera aliguna, "Utanipa kweli au unatania?",

"Nasema kweli.",

Aera alisimama, "Haya, nigaiye mmoja",

Pim alifungua ndoo na kutoa samaki sangara mmoja wa kuchoma. Alimuweka ndani ya chungu cha Aera.

"Wazazi wako wakiuliza waambie mkwe wao amewapa.", Pim aliendelea kufanya utani,

"Bora niolewe na huyu samaki wa kuchoma kuliko wewe.", Aera aliongezea kwenye utani.

"Loh! Nashukuru. Haya nenda, usichelewe zaidi.",

Aera alichapa mguu kuelekea shambani, huku Pim naye aliendelea na safari yake.

Familia ya Aera iliketi chini ya mti ili wapate chakula cha mchana. Baba yake aliitwa Heya na mamaye aliitwa Foni. Pia alikuwa na mdogo wa kike aliyeitwa Gema. Gema alikuwa na miaka 18. Kwa kuwa alikuwa mdogo, urembo wake ulizidi wa dadaye. Wote walipendana na kuelewana sana.

Katika vitu ambavyo hawakutegemea ilikuwa ni samaki aliyenona juu ya mihogo yao ya kuchemsha. Hakukuwa na sababu ya kuuliza samaki ametokea wapi kwani walifahamu fika ukaribu wa Aera na Pim.

"Naona mkwe wangu katuzawadia samaki.", alisema Foni,

"Itabidi tuwapelekee mahindi machache. Hawawezi kutulisha vinono bure.", aliongezea Heya,

"Baba, mama, mimi na Pim ni marafiki tu.", Aera alieleza, "Mkianza maswala ya kupelekeana mavuno mtatupa mzigo mkubwa.",

"Mzigo gani? Kuolewa na Pim?", Gema aliuliza,

"Pim ni kijana mzuri sana. Akileta maombi ya ndoa hatuna budi kukubali.", alisema Heya, 

"Jamani, tuongelee mambo mengine. Msilazimishe ndoa ya watu wasiopendana.",

"Wewe ndio humpendi Pim, lakini Pim anakupenda sana.", Gema alisema kwa mkazo. Alipenda sana mada hiyo kwani alifahamu kuwa Pim ndiye mwanaume pekee atakayeweza kumpenda na kumthamini dada yake kwa moyo wote.

"Embu tuongelee mvua ya jana. Ilikuwa nzito sana.", Aera alibadilisha mada,

"Haikuwa mbaya. Mashamba yetu hayajaharibika.", alisema Foni, mama yao.

Aera aliangalia milimani. Wingu bado lilikuwa limetanda,

"Mnahisi bibi atakuwa salama?", aliuliza,

Ghafla sura zao zilibadilika. Hawakupenda kumuongelea sana bibi yao, mama wa baba yao. Kulikuwa na tetesi zilizosambaa miaka ya nyuma ikimuita mchawi, hivyo bibi alifunga virago vyake na kuhamia milimani kuishi mwenyewe. Tangia hapo, hakuna hata mmoja aliyekwenda kumtembelea zaidi ya Aera. Yeye hakuamini tetesi hizo. Alimpenda sana bibi yake.

"Nitakwenda leo jioni kumtembelea. Nitarudi kesho asubuhi. Ningependa mnifungie mahindi na mihogo ya kutosha ili nimpelekee.", alisema Aera,

"Uwe makini njiani. Usije ukateleza kwenye matope.", alisema mama yake kwa hofu,

"Tafika salama mama, usiwe na wasiwasi.",

Waliendelea kula pamoja.

Jioni, Aera alifungashiwa mizigo ya mihogo na mahindi. Baada ya kuaga familia yake, safari kuelekea milimani ilianza. Kulikuwa na mvua ya rasharasha hivyo muda alioutumia kufika kwa bibi yake ulikuwa mrefu kidogo. Alipowasili giza lilikuwa limekwishatanda. Boma ya bibi yake ilikuwa nzima lakini nje kulijaa tope. Mafiga yalikuwa yamelowana hivyo bibi yake hakuweza kupika chochote siku hiyo. 

"Bibi!", Aera aliita, "Ni mimi mjukuu wako, Aera.",

Bibi alifungua mlango wa boma lake na kuchungulia nje. Alifurahi sana kumuona Aera. Alikwenda kumsaidia mizigo yake na kumkaribisha ndani.

"Umelowana, mjukuu wangu.", alisema bibi, "Vaa nguo zangu kavu.",

"Sawa bibi. Kwenye mfuko kuna mahindi na mihogo ya kuchemsha. Naomba ule.",

"Asante. Nilikuwa na njaa sana.",

Huku bibi akila, Aera alianza kufukunyua nguo za bibi yake ili apate nguo itakayomtosha. Katika upekuzi, alikutana na gauni zuri jekundu lenye urembo ambao haujazoeleka kwenye macho ya watu. Kulikuwa na mtandio mweusi wa hariri, cheni ya shingoni na pete ya dhahabu. Aera alivutiwa sana na mavazi hayo, ila ilibidi aulize;

"Bibi, hii nguo ni yako?", aliuliza Aera,

Bibi alipoina nguo ile alitabasamu, "Hatimaye umeipata.", alisema, "Ndiyo. Hiyo ni nguo yangu.",

"Ya lini? Mbona sijawahi kukuona ukiivaa?",

"Niliivaa zamani nilipokuwa nafanya kazi ikulu.",

Aera alishangaa, "Umefanya kazi ikulu? Kazi gani?",

"Amini usiamini, nilikuwa miongoni mwa makuhani kipindi cha mfalme Zito.",

Aera alizidi kushangaa, "Mfalme Zito si babu wa mfalme Bazi? Alafu makuhani ni wanaume tu.", alisema,

"Zamani makuhani walikuwa wanawake, lakini vishawishi vilikuwa vingi. Wengi walijiingiza kwenye mahusiano na viongozi wa Ikulu na kubeba mimba hivyo idadi yetu ilipungua.",

"Wewe je?",

"Tuliobaki tulihukumiwa kifo. Wenzangu waliuawa ila mimi nilifanikiwa kutoroka.", bibi alielezea,

Historia hiyo ilimsisimua Aera. Alichukua mavazi yale na kwenda kuketi nayo pembeni ya bibi yake.

"Kwanini waliamua kuwaua? Mlifanya kosa lolote?", Aera aliendelea kuhoji.

"Ndiyo. Ikulu ina siri nyingi. Mimi na makuhani wenzangu tuliweza kujua siri ambayo ni kuu kuliko nyingine. Ilitutia hatarini.",

"Siri gani hiyo bibi?",

Bibi alimtazama Aera kiundani. Aliweza kuona moyo wa Aera, moyo wa ushujaa na upendo. Umri wa bibi ulikuwa umekwenda sana na hakutaka kufariki na siri hiyo. Aliona ni vyema aiweke wazi kwa mjukuu wake. Hakuna ambacho angepoteza.

"Aera, dunia ina siri nyingi ambazo binadamu hatuzifahamu. Ni miungu yetu pekee ndiyo inayotambua siri hizi. Wakiona uhitaji, basi miungu huchagua mtu kama chombo cha kuhifadhi siri hizi ili ziweze kusaidia wengine. Vyombo hivyo ndiyo sisi, makuhani.", bibi alielezea, 

"Bibi, unamaanisha tokea enzi hizo mpaka leo, miungu bado wanazungumza na wewe?", Aera aliuliza, 

"Kila nifumbapo macho na kuomba, Miungu huniitikia.",

"Hauna woga?",

"Hapana, miungu nayoitumia ni miungu mizuri, tofauti na miungu inayoabudiwa na wana wa ikulu.",

Aera hakuelewa vizuri, "Unamaanisha nini?",

"Una maswali mengi, Aera.",

"Nataka kufahamu.",

"Jana nilipokuwa ninaomba, miungu ilinipa maono. Familia ya mfalme, kuanzia uzao wa kwanza mpaka huu wa sasa unatawaliwa na laana ambayo chimbuko lake halitambuliki. Kila mke wa kwanza wa mwana wa kiume mwenye damu ya kifalme lazima afe. Hiyo ndiyo siri iliyotuweka hatarini na kupelekea wenzangu wauawe.",

Aera hakuamini maneno ya bibi yake, "Malkia Omuro ni mke wa kwanza wa mfalme Bazi, mbona hajafa?",

"Kwasababu tayari Bazi alikuwa ameoa mke wa kwanza na kumtoa kafara.", alisema bibi,

"Mh, bibi. Mbona msiba haukusikika?",

"Kwasababu familia ya mfalme inahakikisha kuwa mke wa kwanza anatoka kwenye familia za chini zisizojulikana. Pendekezo la ndoa likishafikishwa kwenye familia na kupokelewa, binti aliyechaguliwa anahamishiwa ikulu. Yote hayo yanafanywa kimyakimya, hata jirani zenu hawatajua. Baada ya ndoa, bibi harusi anatolewa kafara usiku huohuo kisha familia yake huuawa siku ifuatayo.",

"Kwahiyo ndiyo maana hatujawahi kusikia?",

"Ndiyo.",

"Je, ni maono gani hayo ambayo miungu imekuonesha?",

Bibi aliweka chini chungu cha mahindi. Kitu alichokuwa anaeelekea kukisema kilikuwa na uzito;

"Katika maono, nimeoneshwa kuwa mtoto wa mwisho wa mfalme, Avana, amefikia umri wa kuoa. Wametambika na binti aliyechaguliwa na mizimu kuwa mke wake wa kwanza _ ni mdogo wako, Gema.",

"Nini!", Aera alishtuka, "Unasema uongo!",

"Nasema ukweli. Familia yako itapokea pendekezo la ndoa kutoka ikulu na watakubali. Nakwambia wewe kwasababu mimi hawataweza kunisikiliza.",

"Bibi, kwa _",

"Sitegemei uniamini. Nimeishi miaka hii yote kimaficho, sina sababu ya kukudanganya. Ninakwambia haya kwasababu umekuwa mtu mwema sana kwangu. Wote walivyonitenga, wewe pekee ulibaki upande wangu. Ndiyo maana nakupa nafasi ya kuiokoa familia yako.",

Aera aliangua kicheko, "Bibi bwana, umezidi utani.", alikunja mavazi ya bibi yake, "Nisamehe mimi kwa kuuliza.",

Bibi alitabasamu. Alitegemea Aera kupokea habari kwa namna ile hivyo hakusumbuka kuelezea zaidi. Alijua ya kuwa maneno yake yataaminika muda mchache ujao.

***