webnovel

CHAPTER 6

Uwanja wa Golf.

Ariana, sekretari wa Janat, alikuwa makini akimtizama Janat na waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, bwana Magambo, wakicheza golf pamoja. Wawili wale walikuwa na ukaribu mkubwa ambao mtu anaweza kuhisi ni wapenzi. Waziri mkuu alikuwa na umri wa miaka 59. Alikuwa na mke na familia nzuri iliyompatia heshima zaidi ya cheo chake. 

Lakini pamoja na yote hayo, alitokea kuvutiwa sana na Janat, kuanzia mwili wake, sauti na uchapakazi wake. Tunaweza kusema walikuwa kwenye mahusiano yasio rasmi na pia Janat hakujipa wajibu huo. Alipenda kutumia muda wake na waziri mkuu, na mara tisa kati ya kumi aliitikia wito na mialiko yote iliyotoka kwa Bwana Magambo, lakini hakumpa uhuru wa kupitiliza. 

Janat alimtumia waziri mkuu kama ngazi za kumfungulia fursa nyingi zaidi za kibiashara za kimataifa. Bwana Magambo alikuwa ni moja ya tiketi zake za mafanikio.

"Kutakuwa na international business summit mwezi ujao, kwenye tarehe za katikati.", alisema Magambo, "Nimeweka jina lako.",

Macho yake yaliganda kwenye miguu ya Janat. Janat alivaa nguo ndogo zenye kuonyesha sehemu kubwa ya mwili wake. Alivaa kitisheti kidogo chenye kumbana hasa kifuani. Sketi yake ilikuwa juu sana ya magoti na kuacha mapaja wazi. Ngozi yake iling'azwa na miale ya jua. Ilikuwa ngumu kuona kasoro kwenye mwili wake.

Janat alimgeukia Magambo, usoni akiwa amevaa tabasamu, "Unafanya watu wahisi kama sistahili hiyo nafasi, mheshimiwa.", alisema kwa maringo kidogo.

"Hapana, sijamaanisha hivyo.", Magambo alijitetea, "Nimetaka tu usikie taarifa hii kutoka kwangu mimi kwanza kabla wengine hawajakutaarifu.", 

"Okay. Mkutano utafanyikia nchi gani?", Janat aliuliza.

"Australia.",

"So inabidi niandae my winter coats, right?",

"Yes.",

Magambo alipenda sana kuona furaha usoni mwa Janat. Kutokana na cheo chake na umaarufu wao wote wawili, hakuweza kumfanya Janat mpenzi wake rasmi. Ni vitu vidogovidogo kama hivyo vilivyomridhisha.

Kwenye gari, Ariana alikuwa na dukuduku la kusema, ila aliweza kujikaza. Lakini muda mwingi alitupa macho yake kwenye kioo cha kuona nyuma na kumtizama Janat kwa mashaka. Janat alikuwa akichezea simu yake, ila machale yalimcheza kwa mbali. Gari lilikuwa kimya sana, na ukimya ule ulitengeneza kelele kwenye kichwa chake.

"Unataka kusema kitu?", Janat aliuliza, macho bado yakiwa kwenye simu.

"Hapana boss. Kwanini unauliza?", Ariana alizuga.

"Nakuona unavoniangalia. Kama kuna kitu unataka kusema then ongea. Usikae na vitu moyoni.",

Ariana alishukuru Mungu kupata ruhusa ile. Aliuma mdomo wake akitafakari atumie maneno gani.

"Boss.", alianza,

"Mh, sema.", 

"Nahisi itakuwa vyema kama ukiacha kukutana na waziri mkuu kwa sasa.",

Janat alinyanyua uso wake na kumuangalia Ariana, "Kwanini?",

"Sijui huyo mtangazaji ni nani, na hatujui njia zake za kupata taarifa za watu. Akijua kuwa unakutanaga na waziri mkuu anaweza kutengeneza stori itakayowaharibia wote wawili.",

"Just because ameweza kumporomosha Suzy haimaanishi ananitisha. Sina kitu cha kuficha, na hata kama ningekuwa nacho, hana uwezo wa kujua. I've been so careful maisha yangu yote.",

"Sijui kuhusu wewe boss, ila mimi ananitisha. Nchi inamuonesha support kubwa sana. Ana nguvu.",

"Hakuna mtu mwenye nguvu zaidi yangu.", Janat aliongea kwa kejeli, "Nikupe siri ya mafanikio? Uwe na powerful connections. Ukiwa na hizo, hakuna atakayeweza kukugusa.",

Ariana alikosa cha kusema. Aliona yeye pekee ndiye mwenye hofu wakati anayehusika haoneshi kutetereka. Aliamua kufikiria maisha yake mwenyewe na sio ya mwanadamu mwingine.

"Hadithi, hadithi watanzania.", ilisikika sauti isiyo ngeni kutoka redioni.

Ilikuwa asubuhi na mapema, muda ambao watoto wanakwenda shule, na watu wazima wakienda makazini. Madaladala yalijaa abiria na migahawa ya chai na supu ilikwishakaribisha wateja wake pendwa. Kifaa pekee cha burudani mahali pote hapa ilikuwa ni redio, za umeme na za betri. Na kipindi ambacho kilikuwa pendwa zaidi nchini kilikuwa hewani. Kila mwenye kusikia alitega sikio lake.

"Janat Marko, aka katoto, mmiliki wa JM Pharmaceuticals. Mwanadada mwenye tuzo zake, aliyeweza kusaidia maelfu ya wanawake. Jike shupa, mrembo _ ila ana cheo chake kipya; muuaji!", alisema mtangazaji yule.

Gumzo na mishangao ilitawala pembe zote za nchi.

"Njia ya mafanikio ya mwanadada huyu imetandikwa na damu zisozo na hatia; damu za watoto, damu za wadada waliomuamini Janat na sera zake za kuboresha afya za wanawake wote duniani. Lakini badala ya kuwasaidia, yeye alitumia binadamu wale kama majaribio ya dawa zake, na zilipofeli walifariki dunia kama ng'ombe machinjioni.",

Mioyo ya watu iliingiwa na huzuni.

"Tuongelee Upendo Pads; Ndiyo, zina harufu nzuri na ni laini. Ila mnakumbuka toleo la kwanza kabisa, hazikuwa maarufu lakini zilisambazwa kila sehemu, vijijini, mahospitalini, mashuleni ili zisaidie wasichana wasio na uwezo wa kununua mahitaji yao ya kike. Kumbe hazikuthibitishwa na TBS kwasababu foleni ilikuwa ndefu, na Janat alijua bidhaa hizo zikifika TBS hazitaweza kukubaliwa, hivyo akatumia connection zake kuziingiza sokoni. Je, mnamjua ni nani anayemfichia Janat dhambi zake? Sio mwingine bali waziri wetu mkuu, Bwana Magambo.",

Janat akiwa njiani kuelekea kazini alipokea simu kutoka kwa Ariana. Haikuwa kawaida ya Ariana kumpigia simu, hasahasa mida ambayo anajua Janat yupo barabarani akiendesha gari. Wazo la kwamba kuna dharura ndilo lililomfanya Janat apokee simu yake.

"Ariana, nipo barabarani.", alisema Janat.

"Boss, washa redio.", 

Janat aliingiwa na mashaka na hakungoja kuwasha redio. Kilisikika kicheko cha mtangazaji yule asiyejulikana.

"Ni majonzi, sijui kwanini nacheka. Wewe mzee Magambo, si una mke na watoto? Tena wengine ni watu wazima kabisa. Janat amekupa nini mpaka unaficha madhambi yake? Mheshimiwa nina swali? Uliposikia na kuthibitisha kuwa pedi zilizoingizwa sokoni bila kupitia TBS zimewapa watu cancer za vizazi, ulifanya nini?", 

Janat alisimamisha gari pembezoni mwa barabara. Uso wake ulivaa swali.

"Na wewe Janat, unafahamu fika ni watu wangapi wamefariki na wengine wengi wamejaa mahospitalini wakisubiri kupasuliwa au kutangulia mbele za haki, lakini umejikausha kau, utafikiri wewe sio sababu. Ni ushetani wa aina gani huu?",

Janat alipokea simu kutoka kwa waziri mkuu. Kwa hofu kubwa Janat alitizama jina lile ambalo siku zote alipenda kuliona kwenye kioo chake cha simu, kasoro siku hiyo. Hakuwa na budi la kupokea simu japokuwa aliogopa,

"Mr. Magambo, good morning _",

"Waambie hatufahamiani!", aliongea mheshimiwa kwa ukali,

Janat alipigwa na butwaa, "Unamaanisha nini?", aliuliza,

"Mimi na wewe hatujawahi kushirikiana kwenye jambo lolote.",

"But Magambo _",

"Unataka kuniharibia familia yangu na kazi yangu? Kwani nilifanya makosa kukusaidia? Taiweka wapi sura yangu? Naomba uliambie taifa kwamba mimi sihusiki na lolote. Sijui utatumia njia gani lakini usinichafulie jina langu.", 

"Mheshimiwa, hata mimi sielewi _",

"I don't care, Janat! Takuharibia njia zako zote, nitakuchakaza. Unanijua vizuri. Nenda kwenye vyombo vya habari, popote pale unirudishie hadhi yangu. Laa sivyo.",

Magambo alikata simu. Janat alipata kizunguzungu. Macho yaliona ukungu na mapigo ya moyo yalimwenda kasi. Ghafla alipoteza fahamu na kichwa chake kulalia kwenye honi. Mlio wa honi ulishitua watu waliokuwa wameketi na kusimama ng'ambo ya barabara na wote walijongea gari kujua ni nini kimemsibu dereva.

Vita vya panzi, furaha ya kunguru; Haikuwa siku nzuri kwa Janat, lakini bila shaka ilikuwa siku nzuri sana kwa Suzy. Japo kuwa alikuwa amejifungia ndani siku zote akipambana na mawazo hatari, habari iliyokuwa ikiendelea redioni ilimpatia faraja. 

Alikuwa akisubiri kwa hamu tofali limdondokee mtu mwingine, hasahasa Janat, na kilio chake kilisikika. 

"Usitukane mamba kabla hujavuka mto.", alisema Suzy huku akicheka peke yake sebuleni.

***