webnovel

chapter 63

"watu walikata tamaa na wengine wakimuona msafiri ni muongo wengine wakiamini mbegu zitakuwa zilishambuliwa na wadudu na kufa na wengine wakianzisha uvumi kuwa msafiri alileta laana.Watu waliacha kupanda na kulima mazao eneo hilo wakijua halifai kwa kilimo kwani eneo limelaaniwa linameza mbegu na wengine wakiamini mbegu ndio zinalaana.Baada ya miaka mingi kupita eneo hilo likawa ni pori lililopitika na watu wachache likiacha historia ya mbegu kubwa za ajabu zilizopandwa.Miaka ilikimbia kizazi kilichopanda kikapita na kizazi kilichosikia hadithi kwa washudiaji kikazeeka na kikawa na vitukuu.Siku Moja watoto walioenda kutafuta miti shamba walirudi kijijini wakiwa na matunda makubwa mikononi mwao mdomoni wakiwa na uchafu wa rangi ulioganda.

Watoto walisimulia kuwa walipita katika msitu wa laana wakitafuta dawa ndipo walipookota matunda makubwa yaliyoanguka kutoka kwenye mti mrefu usio na matawi majani yake ni marefu wameonja matunda na kuona ni matamu sana hivyo wakala na kuamua kuleta nyumbani.Wanakijiji waliamua kwenda kuangalia,walikuta miti mirefu kama walivyosema watoto yenye matunda yaliyorundikana na walipoangalia chini waliona mbegu kubwa walizolia watoto.Ndipo walipogundua kuwa ile miti iliyopandwa milongo mingi iliyopita iliota na Sasa imezaa matunda.Msafiri aliyeleta mbegu hakuwambia itachukua miaka mingapi kwa mti wa kuota au yeye mwenyewe hakujua kwani inawezekana hakuuliza alipokuwa anachukua mbegu hizo.Na Wana kijiji wali iita miti hiyo mihama"

Anamaliza Mzee Limbo na mpaka Sasa Dunila hajaelewa hadithi ya safari ya mhama inamaanisha nini kama siku zote.

" mbona hujaanza msako,mwenzio Inkula ameshavuruga karibia vijiji vyote" anauliza mtemi Limbo akimshtua Dunila na kumtoa katika mawazo ya kupasua kichwa ya simulizi ya mhama." Ana hamu sana ya kuwapata wanawake wote wawili Ili awe mtemi" anazungumza Dunila akipinda mdomo wake uso wake ukijikunja kama amekula ini la kuku lilopasukia nyongo.Mtemi haongei kitu kwani anajua nama kaka yake anavyowaza sambamba na kijana wake." ninaondoka kesho Kuna sehemu nahisi walipo" anajibu akirejea swali la awali la mtemi.

" wapi?"

" Kijiji Cha Ntungu,Kuna habari za kuvutia nimezisikia"

" kuhusu yule kijana aliyezua gumzo miaka iliyopita na Sasa kazua linguine kwa kuwinda"

Dunila anamwangalia baba yake akishangaa kuwa anajua lakini hakuona kama ni ajabu.

" hudhani kuwa labda alikuwa na bahati tu kwa sababu walikuwa maeneo yenye wanyama wengi?" Mtemi anamuuliza.

" we unahisi ni hivyo?" naye anamuuliza kwani kwenye akili ya Dunila hakuna kitu kama bahati nasibu.

" Haina haja nawaza nini" anaongea Mzee Limbo akivuta pumzi ndefu.

" Kuna nini?" Dunila anamuuliza.

" nini?"

" unaonekana kama Kuna kitu kinakusumbua?"

" hapana,ni kwamba tu mambo yatavurugika tena kutakuwa na mchafuko isitoshe damu kumwagika"anamjibu.

" huwezi kuongoza pasipo kuvuja damu,unadhani kwa kuacha kumuua baba mkubwa ulizuia hilo?ona Sasa Mimi na Inkula ndio tunaoenda kumwagana damu Mmoja wetu lazima afe hukusaidia hata kidogo" anamjibu akipandwa na hasira. Baba yake angemuua kaka yake Mzee Makiele angekuwa na nusu usumbufu Sasa hivi.Na kwa makosa yake anaenda kupigana na maadui wawili kama Inkula hatoshi ana mtoto wa utabiri ambaye hajui hata alipi bado wale wazee wasumbufu wasiokuacha ukae upumue kama jipu la tako nao wanamkosesha usingizi.Siku akiwa mtemi ataanza na wale vikongwe wanaopenda kunyonya nafasi za watu kuongezea nguvu na maisha Yao hapa duniani.Mtu ushakuwa mzimu baada ya kupumzika ndio unazidi tamaa huku akisumbua watu wazima.

" sitakufa kwenye mikono ya mtu" anaongea Dunila akisimama, amechoshwa na mazungumzo ya baba yake yasiosaidia kitu na kesho ana safari ndefu.

" kumbuka Dunila siku zote katika vita hata kama ukishindwa lakini ukiwa na busara wewe ni mshindi.Usiku mwema kijana wangu" Dunila anamsikia baba yake lakini anaondoka hatua zake zikiwa nzito zikikanyaga ardhi kwa nguvu utadhani alipita kwenye msitari wa siafu wamemganda kwenye miguu na anawatoa kwa kukanyaga kwa nguvu.

" kwa nini usimwambie tu mtemi?" nyampara aliyesimama pembeni mda wote huu kama hayupo anaamua kuonyesha uwepo wake.

" Dunila ana akili sana mda ukifika atakuja kugundua Kila kitu,ni mda wa kulala" anaongea Mzee Limbo akisimama kwenye kiti kwani anahisi matako yanakufa ganzi kwa kukaa mda mrefu.

" vipi kuhusu mkuu Lukumo unadhani hatagundua kwani tayari alishaanza kuuliza na..." Mtemi anamkatisha.

" shiiiiii,mara ngapi ni kwambie Nzila kuwa miti nayo ina Masikio,na kwa kuwa unaonekana hujachoka Leo utalala huku nje" anaongea Mzee Limbo akielekea ndani akimwacha Nyampara wake au kwa jina lake Nzila akijuta kuongea afadhali angebaki namna alivyokuwa awali.

Mtemi Limbo anatembea na mawazo yake yakienda mbali pindi akiwa mtoto na alipokuwa anamfuata kaka yake kokote anakoenda na kaka yake kumpatia chochote anachotaka lakini Kila kitu kilibadilika wakati wa mrithi ulipowadia mgogoro wa mtemi atakuwa nani uliwafanya kuwa mbali na baada ya Limbo kuwa mtemi ndio kukawatenganisha kabisa.Limbo alitakiwa kumuua kaka yake lakini hakuwa na ujasiri huo kwani alimpenda kupitiliza hata kama kwa sasa hawaongei kama zamani anajisikia faraja kumuona Kila siku akiwa hai.

Maumivu ya kupoteza ndugu kwa madaraka kulimfanya kuzaa mtoto Mmoja tu na alipokuja wa kiume aliamua kutumia dawa kuzuia kuzaa tena hakutaka mwanae kupitia alichokipitia yeye uamuzi wa kuchagua au kujua ndugu.Lakini inavyoonekana hakuna anayemwelewa hata Dunila mwenyewe au ni kwa sababu amekuwa mwenyewe.lakini hata kama hapatani na Inkula siku ikifika ya kupitisha panga au sime katika koromeo lake lazima ataelewa anavyojisikia kwani damu ni damu tena ya ndugu yako inauma zaidi.

Madaraka kitu gani kufanya mtu kufuta ukoo wake wote?anawaza Mzee Limbo akiingia ndani kwake.Kama ilivyosheria mtu atakayekuwa mtemi ni lazima aue ndugu zake wa kiume wote kuepusha usaliti.Ndugu uliye kula na kucheza pamoja mkiwa mnakuwa na wote kuja kuishia kufa kama wanyama wa kufuga ambao una uhakika siku itafika lazima umchinje. Sheria haijawahi kupindishwa mpaka Mtemi Limbo alipotoa amri ya kaka yake kuto kuguswa baada ya yeye kuwa mtemi.Ingawaalimwokoa kaka yake bado ana kipande kikubwa Cha mauaji mikononi mwake pale alipoua watu Kila waliposikia wakizungumzia hadithi ya utemi wao kufikia ukingoni habari iliyotabiriwa miaka mingi iliyopita enzi za mababu zake.bado ile idadi ya watu wake wasio na hatia ambao huwachukua Kila mwezi kuwapa wazee wake wa pangoni kunyonya nafasi zao kwa madai ya kuulinda utemi wake akiwatoa kama kafara.Mwanzoni alipokuwa kijana na mjinga alijua ni kweli lakini Sasa anaona ni unafiki wa wao kutaka kuwa sehemu ya Dunia na madaraka kwa kadri wanavyotaka" mwisho wake utafika?" anajiuliza Mzee Limbo akijitupa kitandani akiwaza hadithi zitakazo simuliwa kwa vizazi vijavyo zitakuwaje? je? atakumbukwa? na kwa mawazo hayo anaamua kulala.

Moto mkubwa unawaka katika nyumba za Kijiji kimoja zikiungua na kusababishia mwanga unaioleta vivuli virefu na vifupu vya watu wakikimbia huku na kule wakipiga makelele ya woga au wengine wakiomba msaada vinaendelea kusikia katika usiku huu wa kiza kinene ukiwa haupo katika eneo hili la tukio.Wanaume wenye silaha mikononi mwao,panga,mikuki,sime,pinde na podo zao zilizojaa mishale wakiendelea kupigana na atakayewahiwa ndiye atakayeonja umauti kwa kifua chake kuwa wazi kwa sababu ya roho yake kutolewa au kiwiliwili kikiwa peke yake na kichwa hakionekani au mwili ukiwa umelala na kupoteza uhai kwa kukosa damu.

Maangamizi ya watu yakiendelea katika usiku huu wa hofu iliyomjaa Kila mtu ambaye anakimbia huku na kule kutafuta msaada au kama atanusurika.Wakati haya yote yakiendelea anafika kijana mwenye umri kama wa miaka ishirini na tano akiwa kwenye mbio utadhani makalio yake yamewaka moto.Nyweke zake zikiwa sio ndefu sana na wala hazijajisokota macho yake ukiangalia kwa haraka unaweza kuona yakiwaka moto ikiwa ni nusu ya ukweli. chini ya jicho lake la kushoto mpaka kwenye shavu likionekana kovu ambalo limekuwa likijaribu kufutika kutokana na miaka lililoishi usoni hapo lakini bado inashindikana kutokana na ukubwa wa jeraha liloacha kovu hilo kufanya kutokutoweka kabisa.

Kifua chake kilicho wazi kikiwa kimejazia misuli ikienda mpaka kwenye mikono,misuli ya mapaja pamoja na miguu.Mkononi akiwa na mkuki pamoja na sime yake inayovuja damu kuonyesha kuwa njia aliyopita haikuwa safi.mgongoni kwake akiwa na podo yake iliyojaa mishale na pegani akiwa ameweka upende wake.Anatumia sime yake kumchinja mwanaume aliyekuwa anamjia na panga yake na pasipo kuitoa kifuani kwa yule mwanaume anamwacha anaanguka nayo chini.Macho yake yanaenda huku na kule kama anamwangalia mtu lakini anachoona ni watu wakipigana na miili mingine ikiwa chini ikiwa imeshabadilika jina na kuitwa maiti.

Anaweka mkuki wake chini na kuchukua upinde wake anavuta mshale mgongoni kwake na kuanza kuwapunguza wanaume waliokuwa wanamjia.Baada ya kuona wamepungua anarudisha upinde wake begani anabinua mkuki kwa mguu unaruka juu na Kisha kuudaka kwa mkono wake wa kushoto.Macho yake yanaenda kwa mwanaume anayetaka kumuua mwanamke haraka anauhamisha mkuki wake uliokuwa mkono wa kushoto na kuuweka mkono wa kulia anaurusha nao unaenda kutua katika mgongo mwa mwanaume huyu na kutoka tumboni.

anainama macho yake yakiwa bado yanamwangalia mwanaume aliyemchoma mkuki anachomoa sime yake kwa maiti ya mwanzo na kukimbia kwa Kasi anaruka na kwenda kuchomoa mkuki wake kabla mwanaume huyo hajafika chini damu zinakimbia zikimwogesha yeye pamoja na mwanamke aliyemwokoa na kishindo chake akitua chini kinasikika kikifuatiwa na Cha marehemu.Anaangaza huku na kule sime na mkuki vyote vikivuja damu utadhani vyenyewe ndio vimedhurika na sio kudhuru.

"nitakuwa nimechewa au?" anajiuliza akiendelea kuangalia kwa umakini wa kivita pumzi zake zikiwa sawa utadhani kazi aliyoifanya ilikuwa ni kupasha mwili tu.