"Hivi niliposema utulie na usifanye chochote hukunisikia Lyn?" Martinez alisimama asubuhi hii chumbani kwa Joselyn huku binti yake akiwa bado kitandani
"Baba kuna nini kwani?" Akauliza Joselyn huku akiwa na macho yaliyokuwa na dalili za usingizi mzito
"Mimi baba yako eeeh, kama ni hivyo basi kwenye hiyo kesi uliyojitafutia usinihusishe hata kidogo" Martinez akazungumza kwa jazba huku kifua chake kilipanda na kushuka kwa hasira
"Kwanza amka na uanze maandalizi maana unarudi SA kesho au kesho kutwa?"
Lyn aliyekuwa amelala aliposikia hivyo akaamka na kuketi huku akimtolea macho baba yake kwa mshangao
"Una siku ya leo Joselyn fanya mambo yako vyema. Utarudi SA mpaka nitakaposema inafaa uje" Martinez akaongea kisha akageuka ili kuondoka lakini Joselyn akakurupuka na kurusha blanketi chini akamuwahi baba yake akimkumbatia kwa nyuma
"Baba nakuomba usinirudishe kwanza, nitatulia baba hadi mambo yakae Sawa nakuomba" Lyn akamsihi baba yake huku machozi yakianza kujaa kwenye macho yake.
"Niachie, unakuwaje binti yangu usiyenisikia, unampenda Simunge au unataka kuniharibia mimi eeeeh?" Martinez akasimama kisha akamtoa mikono Joselyn ambaye alikimbia mbele yake na kumpigia magoti baba yake
"Baba tafadhali sana sitafanya makosa kabisa nitatulia" Lyn akamuomba baba yake huku akiweka mikono yake pamoja kifuani
"Nitafanya nini na wewe hapa, hivi unajua ni kwa kiasi gani unaiingiza matatizoni? Inspekta Sunday ni mtu hatari akisimamia uchunguzi. Nimeishi nikikwepa kabisa kupita kwenye mistari yake anayochora sasa wewe unanidumbukiza kwenye shimo pamoja nae? Hivi huwa una akili kweli au ndio kama hizo za mama yako? " mtetemo wa hasira ulikuwa kwenye sauti ya Martinez
Lyn akamwangalia baba yake huku machozi yakitishia kulowesha kope zake, "baba, baba yangu nakuomba unisaidie tu. Nakuahidi nitampata Ed tena na mpango wetu utakaa v__"
"Sitaki ujaribu chochote kwa Simunge, hauwezi kupata chochote na huo ujeuri wako" akamkatisha
"Hapana baba, nakwambia Ed ananipenda sema tu yule___"
"Shut up Joselyn" sauti kali ya Martinez ikamshtua Joselyn na akainua macho kumtazama baba yake machoni. Asubuhi ile baba yake alitoka jasho
"Hutakiwi kutoka ndani wala kutumia simu yako. Nipe hiyo simu yako" Martinez akaamrisha
"Lakini ba_"
"Lete simu upesi. Mama yako atakuletea vyote unavyohitaji mpaka nitakapojua ni salama kiasi cha kutosha"
Joselyn akaichukua simu na kumkabidhi baba yake ambaye aliondoka mle ndani akimuacha amesimama
"I hate you Aretha" akasema kwa sauti kisha akaelekea kitandani na kuchukua glasi ya maji iliyokuwa pembeni ya kitanda akanywa yote. Akaokota blanketi lake na kurudi kupanda kitandani na akijifunika hadi kichwani.
"Nitawamaliza tu siku nitakayogundua mko pamoja bado"
*************
Edrian aliingia ofisini huku ratiba yake ikimuweka mara zote kwenye kompyuta iliyokuwa mbele ya kiti alichokalia. Sauti ya simu iliyokuwa mezani ilimshtua, bado alipitia maelezo mbalimbali kutoka kwenye operesheni za uchimbaji katika migodi inayomilikiwa na SGC.
Akabonyeza kitufe cha kupokelea,
"Bro, naweza kukuona?" Sauti ya Allan upande wa pili ilisikika
"Sawa" Edrian akamuitikia na mlio wa simu ikikatika ulisikika
Akarudisha macho kwenye kompyuta huku akitafakari juu ya mabadiliko ya ghafla ya uchimbaji wa madini.
"Nahitaji uchunguzi mapema, mwezi mzima kuna vikwazo vingi kwa kila oparesheni " akawaza
Mlango ukafunguliwa, naye Allan akaingia akiwa na tabasamu lake murua
"Karibu" akamkaribisha huku akimuelekeza kiti kilipo
:Asante, naona unapitia tathmini nzima ya operesheni" Allan akamwambia huku akiketi
"Mhhh, kuna mapendekezo nimeyaainisha kwa kila ripoti." Edrian akamwambia kabla ya kuegama kwenye kiti akimuangalia usoni
Wakazungumzia mambo yanayohusiana migodi na mambo ya msingi yaliyotakiwa kufanyika.
"Wiki ijayo kama ratiba yangu inavyoelekeza nitakuwa nje, natumaini tutaweka kila kitu sawa"
"Aaaah lile onesho la Paris, litatusaidia kuongeza ufanisi kwenye kuhifadhi na kusafirisha madini"
"Ndio. Hata hivyo bado nina mambo kadhaa ya kufanya huko. Nitachukua wiki moja zaidi"
"Eeeh" Allan akashtuka