Geti dogo likafunguliwa huku Coletha akitangulia kisha Frans aliyevaa suti ya rangi ya bluu iliyokolea akafuata kwa nyuma. Aretha akafuatia nyuma ya Frans, macho yake yalihama chini kwa aibu ya kuogopa kuonana na macho ya Edrian.
Edrian alimwangalia Aretha kama mtu aliyeona malaika na akapigwa ganzi. Alikiri ndani yake kuwa kazi waliyofanya watu wa V ilistahili heshima yake.
"Rian" Aretha akamwita na kumshtua kutoka kwenye pumbaziko lililompata..
"Retha..." akatamani kusema lakini akakumbuka mama alikuwa pembeni akameza funda zito la maji kisha akataka kuelekea kumfungulia mlango lakini Coletha akamuwahi na kufungua mlango wa mbele upande wa abiria...
"Asante Coletha" Aretha akashukuru kisha akapanda
"Mama ngoja tuwahi" Edrian akamuaga mama ambaye alitabasamu kwa kuona athari ya muonekano wa Aretha jinsi ulivyomuathiri kijana huyu..
"Hapana shida mwanangu ila usisahau kumrudisha mwenzio nyumbani" mama akaongea huku akicheka akijua kabisa Ed pekee ndio atakuwa amesikia maana Coletha na Frans tayari walikuwa ndani ya gari.
Akatabasamu na kuelekea kwenye gari! Mara alipopanda kwenye gari alimwangalia tena kwa haraka. Uso wake uling'aa kama nyota, nywele zake zilifungwa kwa nyuma na kutengeneza mlima mdogo ulipitishwa maua upande mmoja. Gauni ile ya njano ilimkaa vyema na kumfanya aonekane kama binti mfalme mdogo.
"Umependeza Retha" akaweza kumwambia na kisha akawasha gari na wakaondoka kuelekea kwenye onesho.
Coletha na Frans waliendelea na maongezi ya hapa na pale kupunguza ukimya ulioendelea wakati Edrian akiendelea kuiba kumuangalia Aretha ambaye alikuwa akiangalia kucha zake zilizotengezwa vyema na kunakshiwa kwa rangi nzuri.
Edrian alitamani angebaki na Aretha tu pekee kwenye gari. Akajilaumu kwa nini hakumwambia Derrick amchukue pacha wake na pengine wangeenda na Frans
"Aaaaargh" akaugulia ndani maana sasa alitamani kumkumbatia Aretha na kubusu midomo yake ambayo ilipakwa rangi ya mdomo iliyofanya tamaa ya Ed kuwa kama moto wa gesi. Aretha alimvutia zaidi.
Alijaribu kuendesha katika spidi ya kawaida lakini kila wazo na kumuweka Aretha mikononi mwake lilipogonga mawazoni mwake, liliathiri mwili wake na mguu wake ulikanyaga mafuta mwendo ukungeza.
"Rian unakimbia sana hatujachelewa" Aretha aliongea akiwa ameshtuka ghafla kuona gari inaongeza mwendo.
"Big brother unataka tupae jamani" Coletha nae akalalamika.
Edrian akameza mate na kisha akatabasamu na kupunguza mwendo. Iliwachukua muda mfupi kuwa wamefika kwenye Jengo lenye ukumbi wa Southern Pole.
Wakashuka, lakini Edrian akamshika mkono Aretha mkono kumrudisha kwanza...
"Retha" akamuita huku mkono wake ukimvuta taratibu kurudi ndani.
"Aaahmmm" Aretha akageuka kumuona Edrian, macho yake yakawasilisha tamaa yake kwa namna alivyomtazama
"Retha, I love you" Edrian akamwambia na kuinama taratibu hadi karibu na midomo ya Aretha kisha hakuendelea zaidi japo alitaka kumbusu lakini asingefanya bila ridhaa ya Aretha
"Rian, umependeza sana na nakupenda pia" Aretha akajibu huku macho yake yakiinuka kumwangalia Edrian. Kwa Edrian alitamani dunia yote isingekuwa na watu wengine zaidi yake na Aretha kwa sasa. Alijizuia vya kutosha wakati Coletha na Frans walipokuwa kwenye gari lakini sasa alitaka walau kuishibisha kidogo tu tamaa yake.
Akiangalia midomo ya Aretha na akamshika kidevu na kumpigia busu jepesi akiogopa asije akaharibu rangi ya mdomo iliyopakwa vyema.
"Kila la heri princess, twende sasa" akamwambia mara alipoacha kumbusu na kukutana na macho ya Aretha yakiwa yamefumbwa akitegemea busu lingeendelea lakini Ed alikuwa ameacha.
"Twende Retha" akamshtua huku akitabasamu kwa furaha kujua sio yeye tu aliyetamani kumbe hata Aretha alitamani
Aretha akaangalia pembeni kwa aib baada ya kufumbua macho akapeleka haraka mkono kwenye mlango ili kutoka lakini ghafla akageuka nyuma na kurudi, akampigia busu la kushtukiza shavuni kisha akatoka huku akihema
"What?" Edrian akashangaa na kutabasamu akashuka kwenye gari kujiunga na wengine waliosimama nje wakiwasubiri na Aretha.
Wakaelekea mahali ambapo Beruya aliwaelekeza wakutane kabla ya onesho.