Aretha alimtazama Ed huku akitabasamu, "nitaishi utakapoishi Rian"
Wakaketi pale kwa muda wakizungumza kuhusu kazi na mambo mbalimbali ya maisha. Jioni ilikuwa ni muda mzuri wa kutazama filamu pamoja baada ya kupata chakula cha jioni. Wakiwa katika mazingira yale muda wa usiku baridi iliongezeka na hivyo hawakuwa namna nyingine zaidi ya kuketi ndani hadi walipopitiwa na usingizi na wakalala kwa muda kwenye kochi hadi Ed aliposhtuka, kisha akamchukua Aretha wakaenda chumbani.
*********
Siku zikakimbia kwa haraka, wiki ikaisha Beruya akiwa tayari ameimarika kiafya na mara nyingi alitumia muda wake kuchora picha kwa ajili ya onesho baada ya Li kumnunulia vifaa vyote vilivyohitajika. Derrick na Yassin mara kadhaa walimtembelea kumpa taarifa za maandalizi, naye Li alimtembelea mara kwa mara kumjulia hali.
"Comrade siku hizi hatuungani kabisa kwenye mikeka, vipi ndio kusema umekuwa 'bae' eeeh" Allan akamtania Li mara tu alipoingia ofisini kwake ikiwa ni sehemu ya ukaguzi kuangalia shughuli ziliendaje pale Ashanti kwenye ofisi za SGC.
"Aaaah Comrade majungu hayo, mbona nipo sana na juzi tu nilikuwa hapa" akajitetea Li mara baada ya kuketi
"Ulikuja hapa, ila mitaa yetu hujaonekana comrade leo wiki na kitu una udhuru wa kwenda kwa mama kila mara.... hahaha vipi kuna jipya limeendelea au nimeachwa mbali" Allan akamuuliza
"Hahahha Comrade mambo ni shwari tu. Bro akirudi nitarudi mkekani"
"Ooooh basi sawa, nikajua 'painter' kashanizidi akili hahaha" Allan akamwambia huku akiinua nyusi zake
Li akanyamaza na kumwangalia kisha akatabasamu "So...Uliniambia kuhusu wasi wasi ulionao juu ya Renatha... Kwani bado anachelewa kutoka?"
"Comrade...sitaki kukuficha ila kuna wakati akichelewa inanilazimu nibaki, na mara kadhaa anaulizia sana lini Bro anarudi. Kitu kilichonifanya nikuite ni hiki" Allan akavuta pumzi kisha akaendelea
"Jana nilichelewa kutoka, na nilipomaliza nikashuka hadi chini lakini wakati naingia kwenye gari nikahisi nimemuona mtu akiingia kwenye lifti ambaye alimfanania Renatha. Tatizo nilipogeuka mlango wa lifti ndio ulikuwa unamalizia kufunga. Nikaamua kurudi, nilipofika mlango wa kuingia ofisini kwangu ulikuwa wazi wakati niliacha nimefunga kabla ya kutoka. Nikawaita walinzi ambao walikuja na kutazama dalili zozote za uvamizi. Na tulipoenda kwenye kamera hakuonekana mtu."
Li akashtuka na kumwangalia "Na vipi ofisini kwa Bro?"
"Huko palikuwa pamefungwa na hakukuonesha dalili zozote za kuwa mtu aliingia na isitoshe Captain alishaweka ulinzi, hata kugusa ule mlango akishawasha kile kifaa kitamjulisha" Allan akamjibu
"Na vipi humu ofisini kwako hakuna kitu kilichoondolewa? Akauliza Li huku akiwa na jicho lenye kubeba umakini
"Hakuna hata kitu chochote kilichoondolewa. Walinzi walisema watafuatilia kuona kama aliyehusika ni mtu wa ndani au la" Allan akamwambia huku akionesha wazi jambo hilo lilimsumbua
"Okay hujamwambia Bro?" Akauliza
"Hapana"
"Vizuri, sitaki apate mshtuko" akamwambia kisha akachukua simu yake na kumpigia Captain
Alipomaliza kuongea "Hilo tumelimaliza Captain anakuja, mjulishe Alphonce"
Allan akachukua simu na kumjulisha Alphonce ambaye ni mkuu wa kitengo cha Teknolojia na Mawasiliano.
"Comrade nina swali langu eeeh" Li akaendelea huku akitabasamu
Allan akamwangalia huku akishangaa "Uliza Comrade"
"Mara ya mwisho wakati nakuona ukimzungumzia binti huyu uso wako uling'aa sana, ninaweza kusema unavutiwa na Renatha, niko sawa comrade!" akamuuliza huku akiegama kwenye kiti
"Aaaahm. .aa hapana comrade" Allan akaongea huku akibonyeza kitufe cha kompyuta
"Allan..you are more than a friend.. you are my brother... uliwaambiaje watu wa ulinzi maana najua walikwambia kuhusu kuwataarifu polisi" Li akamwambia kisha akaweka mikono yake kwenye meza
Macho ya Allan yakawaka kwa mshtuko kisha akainama huku akiangalia kompyuta
"Ni. ...ni__" kabla ya kusema Li akamkatisha
"Najua comrade.....najua haukutaka kuwahusisha maana ingekulazimu umtaje Renatha"
"Bro...nashindwa kufungua mashtaka, nimejaribu kumuuliza asubuhi, alichoniambia ni kuwa sina ushahidi."