webnovel

KUNA MTU

Li hakuwa na namna zaidi ya kulala pembeni ya Beruya huku kifua chake kikitumika kama mahali salama ambapo binti huyu alijificha. Usingizi ulikuwa adimu sana kwa Li ambaye alikuwa akijitahidi kufikiri vitu vingine akilini zaidi ya yale ambayo yaliendelea walau aweze kuhakikisha halali ili aondoke mara atakapoona Beruya hayuko katika jinamizi ndotoni

Kama ilivyo kawaida ya mwili kuna wakati hata ungeulazimisha kuwa macho lazima utakusaliti, Li alijikuta usingizi umempitia. Kama mtu angeliingia mle chumbani angeshawishika kusema hawa ni wapenzi wa muda mrefu.

Saa ilipokaribia na kupambazuka Li alishtuka usingizi na ndipo alipoangalia pembeni na kumuona Beruya akiwa amelala na sasa hakuwa amejikunyata tena. Li akajigeuza taratibu kuhakikisha hawezi kumuamsha, akatembea kwa kunyata nyata hadi alipofikia mlango. Akamwangalia Beruya kisha akatoka kwa haraka akielekea chumba alicholala. Akaingia kabatini na kuchukua nguo za mazoezi kisha akatoka na kuamua kukimbia walau kusafisha fikra zake ambazo tayari zilikuwa kwenye msuguano. Alijisikia tofauti.....

****************

Mlango wa jikoni ukafunguliwa na Li akaingia akiwa amelowana jasho, shati ilikuwa begani kwake. Ni wazi hakujua kama angemkuta Beruya jikoni, mara alipoingia ndani alivutiwa na harufu ya chapati iliyofikia pua yake na kusababisha mate kumjaa mdomoni. Akidhani ni Annie aliyekuwa akipika aliingia jikoni ili aweze kuchemsha maziwa kabla ya kuelekea bafuni, lakini alipata kigugumizi aseme nini

"Li! Habari ya asubuhi?" Akasalimia Beruya huku akiachia tabasamu lake ambalo lilipokelewa na Li katika mshangao..

"Salama, mbona uko jikoni mapema hii? Annie am__"

"Yuko nje, nimeamka salama nikaona nifanye kitu walau kwa watu wanaonitunza" Beruya akamkatisha huku akiipua kikaangio kilichokuwa jikoni na kisha akaweka sufuria ya maziwa iliyokuwa pembeni

Li akapiga hatua chache kusogea aliposimama Beruya, akamtazama kama kuona kulikuwa na hali ya kutia shaka lakini hakuiona.

"Niko vizuri Li, tena najisikia nina nguvu kuliko jana" akasema Beruya

"Mmh! Ila bado unahitaji muda wa kupumzika zaidi" Li akamwambia huku akimimina glasi ya maji

"Lakini jana nilipumzika na nimekuwa na ndoto ambayo imeisha vyema" Beruya akamwambia

Li akageuka na kumkazia macho, "Inahusu nini hiyo ndoto?" akauliza kwa shauku kutaka kujua hasa

Beruya akajikung'uta unga mikononi na kwenye aproni aliyovaa na hakika uso wake ulionesha huzuni kwa sekunde chache kuwa lakini akaachia tabasamu akainama chini na kusema...."aaah niliota nimetekwa na Damian na alinitesa sana hata sikuwa na nguvu ya kujiokoa, lakini baada ya kulia nikiomba msaada kuna mtu__"

Kabla ya kuendelea mlango wa nyuma ukafunguliwa na mama akaingia

"Eeehn hukuondoka mwanangu?" Akasema mara alipomuona Li kwa kuwa hakutarajia kumuona asubuhi hii akijua aliondoka jana...

Li akamsalimia mama yake akikwepa kujibu swali aliloulizwa kisha akageuka kuelekea chumbani kwake kuoga.

"Aishhhh huyu mtoto sijui nini kimemsibu, binti yangu huyu Li alikuja kukuaga?" Mama akamuuliza Beruya huku akielekea kwenye meza na kuketi

"Aahm!" Beruya akashangaa

"Aliniambia anakuja kukuaga lakini namuona hapa sasa hivi" mama akamwambia

"Aaahm sikumuona mama, labda aah..." kama nuru iliyoangaza kwenye fahamu za Beruya, mshangao na aibu vikamshika akafumba macho

"Labda nini mwanangu_" sauti ya ķumwagika kwa povu la juu la maziwa vilimshtua Beruya na mama

"Oooh nimekusemesha mwanangu hadi umesahau.."

"Aah hapana mama" Beruya akajibu huku akifanikiwa kuyashusha maziwa na kuyaweka kwenye chupa, akaendelea na kusafisha

"Leo umeamka vizuri zaidi mwanangu" mama akamwambia

"Eehmm" Beruya akashtuka na kumtazama mama lakini baadae akaangalia pembeni na kumjibu

"Aaahm.. nashukuru Mungu leo najisikia vyema mama"

"Kweli mwanangu, natamani kukuona ukiendelea vyema. Nimemwambia Li akuletee vifaa vyako uendelee na uchoraji"

"Oooh nashukuru sana mama, kwangu kuna vifaa na picha chache naweza kwenda kuvifuata"

"Aaaahm ongea na Li atajua nini cha kufanya mwanangu"

Aliposikia kuongea na Li, Beruya akashusha pumzi na kuendelea kusafisha...

Next chapter