webnovel

WEWE NI DAWA

Tangu muda aliofika Edrian nyumbani kwao Aretha na kumsimulia mama yake mambo yaliyotokea, kazi kubwa ambayo alikuwa nayo ni kuthibitishia mama huyu juu ya usalama wa binti yako.

Mazungumzo haya yalikuwa ya muda mrefu wakiwa wamekaa nje, japokuwa mara kadhaa Aretha alitaka kuingilia lakini mama yake alimuomba anyamaze na akamtoa mahali walipoketi alimuomba aingie ndani..

"Mama, naomba kwanza uniridhie, nampenda Aretha inawezekana nilifanya makosa makubwa hapo nyuma lakini sitaki kumpoteza. Yoyote yaliyotokea nakubali ni uzembe wangu."

"Mwanangu huyu binti hajawahi kuwa na kesi yoyote na wala hafahamiki kiasi cha kuhatarisha usalama wa mtu mwingine. Lakini kumekuwa na mfululizo wa matukio ya fedheha yenye kuleta uchungu. Niambie kama mzazi wake najisikiaje?" Mama akamtazama sana

Edrian aliyekaa kwenye kiti kilichoangaliana na cha mama yake Aretha akakuna kidevu vyake kisha akamwambia

"Mama kuna njia rahisi ya mimi kulimaliza hili, naomba nipewe nafasi ya kutangaza mahusiano yangu na Aretha, kwa kuwa umebaki miezi michache amalize chuo nitahakikisha anakuwa salama. Kuhusu kesi wakili wangu akaendelea kufuatilia na hakuna namna aliyehusika ataachwa salama mama." Akameza mate na kumwangalia tena mama ambaye uso wake ulianza kulainika

"Nitafuata taratibu zote kwa maelekezo yako. Na kwa sasa mama anataka apate nafasi ya kuonana nanyi. Lakini ninalo ombi moja la muhimu sana kwa wiki mbili zijazo"

"Omba mwanangu nakusikiliza" mama akamwambia huku akiegama kwenye kiti

"Wiki ijayo nitakuwa na safari nje ya nchi kwa wiki mbili, naomba sana nipate kibali cha kusafiri na Aretha." Edrian akamwangalia mama

"Aaahm mwanangu, hili mbona zito sana" mama akamwambia akionekana kuwa na wasi wasi..

Kabla Edrian hajaendelea kumsihi, mama ni kama alipata wazi

"Mwanangu nakuomba nami kabla ya kukujibu hili niongee na mama mwenzangu."

"Unamaanisha mama Simunge?" Edrian akamuuliza

"Ndio mwanangu, nikionana na mama yako nitakupa jibu la ndio au la hasha" mama akamwambia.

"Sawa mama. Siku gani itafaa ili nimuandae?" Akauliza

"Jumamosi itafaa mwanangu. Nijulisheni muda mtakaofika tu"

"Nitafanya hivyo, na samahani mama, naweza kuendelea na maandalizi ya safari kwa kumtengenezea hati ya kusafiria Retha?" Ed akauliza huku akiwa ameinama kidogo

"Hahaha mwanangu na ikiwa nikakataa?" Mama akacheka kicheko chepesi na kuuliza

Edrian akacheka "Ni sawa tu mama. Hati itabaki na itafaa kwa wakati mwingine"

"Oooh basi sawa. Wewe fanya kile unaona chema. Nitakujulisha tu mara tutapomaliza" akamwambia huku akitabasamu

"Ombi jingine mama, nimeongea na mkuu wa idara ya sanaa chuoni kwao Retha, atapewa mapumziko ya mwezi mmoja lakini masomo yake yote yatatumwa kwenye barua pepe yake. Lakini bado sijamwambia Retha naomba unisaidie kufanya hivyo"

"Aahhha sawa mwanangu."

"Nashukuru mama kwa kunielewa" akashukuru sana huku akiweka mikono yake pamoja kifuani kisha akainuka

"Sawa mwanangu, lakini usisahau kuwa usalama wa Retha unaenda sambamba na usalama wako. Binti yangu anakupenda na sidhani kama atakuwa na amani ikiwa utapata matatizo" mama akamwambia naye aliinuka

"Sawa mama nitafanya hivyo." Edrian akamjibu kisha akapiga hatua kuelekea getini.

"Retha" mama akamuita

Dakika chache Aretha akatokeza na kumuelekea Edrian na mama yake.

"Mtoe mwenzio" mama akamwambia kisha akamgeukia Edrian, "mwanangu nashukuru sana"

"Asante pia mama" mama akawaacha na kuelekea ndani huku Aretha na Edrian wakaelekea getini.

"Rian mama amekwambia nini" akauliza Aretha mara walipotoka nje ya geti na kusimama mbele ya gari ya Ed

"Hahahha Retha unataka kujua?" Ed akamuuliza huku akitabasamu kwa utani

"Eeeeh" Aretha akashtuka na kuinama huku akitabasamu

Edrian akamuinua kidevu na kumwangalia, "nashukuru tuko pamoja Retha. Mama amenipa nafasi"

"Mmhhm" Aretha akaguna huku akimwangalia machoni Edrian kisha akamwambia

"Ulimwambia nini?" Akauliza

"Nilimwambia wewe ni dawa yangu siwezi kukaa mbali nawe" Ed akamwambia kwa sauti ya chini

"Eeeeh Rian" akashtuka Aretha huku akirudi nyuma lakini mkono wa Ed ukamuwahi kiunoni na kumfanya ashtuke zaidi

"Rian"

Next chapter