Ilichukua dakika chache kwa Edrian kufika hospitali ya City, kwa kuwa ilikuwa karibu sana na mahali walipotoka.
Njiani sauti ya Coletha na Frans ndio zilizosikika zikiongelea kile kilichotokea. Kwa upande wa Edrian na Aretha kimya kilitanda kati yao, kila mmoja moyo wake ukiwa katika machafuko. Kwa Aretha alikuwa akijilaumu kwa kile kilichotokea kwenye lile onesho
"Nisamehe sana Beruya hii yote ni sababu yangu" aliwaza Aretha na macho yake yalijaa machozi akitamani angeweza kubadilisha kile kilichotokea. Hili lilikuwa ni onesho muhimu kwa Beruya.
Kwa upande wa Edrian, moyo wake ulikuwa na fukuto la wivu na hisia za uchungu kuona Aretha aliamua kutomsikiliza na kuendelea kuzungumza na BM. Alijaribu kujifariji huenda Aretha alikuwa sahihi zaidi yake lakini bado alitamani kuona akiaminiwa na mpenzi wake.
"Itakuwaje kama huyu BM anataka kunitenganisha.....aaaargh"
Wakashuka kwenye gari, na kwa sababu Edrian alifahamika hapa City Hospital sababu ya ushirika wa hospitali hii na kituo cha watoto walichokiendesha, haikuwachukua muda kuwa wamefika kwenye chumba alikolazwa Beruya.
Muuguzi waliyeongozana nae akawapa ishara wasubiri pembeni ili aangalie kama kulikuwa na matibabu yakiendelea. Akarudi Na kuwaruhusu Edrian na Aretha kuingia huku wakiwaacha Frans na Coletha wakiwasubiri kwenye viti vilivyokuwa pembeni ya mlango.
Mara walipoingia, wakamkuta daktari yule aliyemhudumia Beruya akiwa ameketi pembeni huku akiandika mambo fulani kwenye simu yake. Akainuka na kuwasalimia huku wakishikana mikono.
Walipomaliza kusalimiana wakauliza hali ya Beruya ambaye alitundikiwa dripu iliyokuwa ikitelemka taratibu
"Atakuwa vizuri tu. Alizinduka lakini tumemchoma sindano ya usingizi aweze kupumzika zaidi." Daktari akawaambia.
Aretha akajikaza maana machozi yalikuwa karibu sana kumtoka. Edrian akamkumbatia alipoona hisia za Aretha alipomwangalia Beruya ambaye alilala katika utulivu mkubwa.
Walipomaliza wakamuaga daktari Damian kama alivyojitambulisha wakati akimsaidia Beruya. Kuna namna Edrian alihisi kitu kwa daktari huyu maana alikuwa akiwapa taarifa huku akionesha kubeba lawama kwa Aretha. Alimuangalia jicho la mashaka lililobeba uchungu na hata Ed alipomkumbatia Aretha ni alimwangalia kama mtu aliyewakasirikia.
Wakatoka mle chumbani, wakiwakuta Coletha na Frans wakiendelea na mazungumzo yao. Mara walipowaona wakainuka na kuanza kuondoka kuelekea nje na wakati huo giza lilianza taratibu kutawala.
Wakiwa kwenye gari, Aretha akashangaa barabara ambayo walienda akageuka kutaka kumuuliza Edrian, lakini kwa namna alivyokuwa kimya akaona anyamaze aone wapi walipelekwa. Frans akamjulisha kuwa mama yao anamtafuta kwenye simu
"Mbona haukunipa alipopiga maana nilizima tangu nilipoingia pale ukumbini?" Aretha akamuuliza Frans ambaye alitaka kujibu lakini Edrian akamuwahi
"Nilimkataza asimwambie mama kilichotokea" Edrian akajibu pasipo kugeuka kumwangalia Aretha
"Eeeeh kwa nini?" Aretha akauliza huku sauti yake ikionesha kukasirika
Edrian akageuka kujaribu kumwangalia kwa kutumia mwanga wa taa zilizowaka barabarani.. kabla hajajibu Frans akamuwahi
"Dada Retha, mama angejisikia vibaya na kwa hali yake angeweza pata mshtuko."
"Kwa hiyo hatajisikia vibaya tukienda kumwambia sasa Frans?" Sasa kulikuwa na hasira kwenye sauti ya Aretha
"Retha... tunaweza kumweleza taratibu sasa kuliko wakati ule" Edrian akamweleza huku naye akijaribu kushusha hasira ambazo zilichanganyika na wivu kila alipomfikiria BM na Aretha wakiongea.
"Retha dear, relax! Tutamuona mama na kumwelezea taratibu" Coletha akamwambia akijaribu kulainisha hali ya hawa iliyokuwa karibu kuharibika. Alimuona kaka yake na ule wivu wake lakini pia aliona Aretha uchovu na huzuni vilimvyomgeuza na kuwa mkali.
Kimya kifupi kikapita kati yao, kisha Aretha a mara alipoona mwelekeo wa gari akamwambia "Nataka niende nyumbani Rian"
"Nitakupeleka" akajibu kwa ufupi na kuendelea na usukani akimuacha Aretha kwenye maswali maana muelekeo wa gari ulienda kwa Edrian na sio kwao
"Kwa nini ananipangia kila kitu" akawaza Aretha.
Gari ikasimama kwenye geti la nyumba ya Edrian.