Baada ya kumaliza kipindi chake kwa leo Derrick alitoka darasani akiwa na baadhi ya wanachuo wenzake. Akatoa simu yake kuangalia kama Charlz alimpigia. Naam ndivyo ilivyokuwa simu 7 zilipigwa na tatu zikitoka moja kwa moja kwa mtu aliyemtaka.
Akampigia Charlz akitupilia mbali kwanza namba nyingine zilizomtafuta. Leo alitaka mpango wake ufanikiwe kwa hatua ya kwanza.
"Kiddo, nimeona missed calls, umefanikiwa?" Alianza moja kwa moja na swali kwa Charlz
"Nimefanikiwa ila nitakutafuta baadae kiddo naingia lecture" alijibu Charlz upande wa pili.
"Niambie ndio ukapige ki..." kabla Derrick hajamaliza
"Kiddo baadae, ukitaka jizamishe majini naingia class" aliongea Charlz na kukata simu
"Aaaaarhggg" alilalama Derrick kwa hasira kisha akaangalia saa akajua mwendo wa kutoka chuoni alipo hadi Ashanti Tower atachelewa kwa dakika 15 kulingana na muda wa Aretha kama alivyoambiwa na Loy.
Akawaaga wenzake na kuondoka na pikipiki yake aina ya Ducati.
Alipoingia Ashanti Tower hakuelekea ofisini kwa Ed bali alipanda ghorofa ya tano ulipokuwa mgahawa ili apate chakula maana alikuwa na njaa.
Derrick akamcheki tena Loy na akamthibitishia kuwa Aretha yuko ofisini kwa kaka yake. Akamuomba amjulishe mara atakapotoka. Akaagiza chakula chepesi huku akiendelea kusubiri kwa shauku na akiomba si Ed wala Linus asijitoe kumsindikiza Aretha. Nini kiliendelea kwenye kichwa chake alikijua mwenyewe.
"Mbona hatoki, bro anazungumza nini tena au anajieleza?" Alijiuliza Derrick lakini wazo la kaka yake kubadili msimamo haraka alijua ni gumu kama kuukusanya upepo kwa kiganja.
Alikumbuka ila sura ya Ed alipoangalia kile kipindi akajua bila shaka kuna kipimo kidogo cha hisia kilibadili uso wa kaka yake. Hakuna ambaye angejua isipokuwa watu pekee waliopata kukaa na Ed ndio wanaweza kufahamu hilo.
Alishtuliwa na ujumbe kwenye simu yake ambapo alipofungua alikuwa ni Loy akimjulisha Aretha ametoka. Akatoka mgahawani na kupanda lifti ya kushuka chini kisha akaelekea mbele ya ofisi ya mapokezi akaomba faili dogo. Akaelekea kukaa kwenye eneo lililowekwa makochi kwa ajili ya kusubiri.
Macho yake yalikuwa kwenye milango ya lifti mbili, akaona inayoshuka akajua Aretha atakuwa ndani ya hiyo hiyo. Akaweka vyema faili lake huku akichungulia mlango ulipofunguka.
Akatoka binti aliyevaa blauzi nyepesi rangi ya chungwa huku chini akiwa na suruali isiyoshika mwili rangi nyeusi. Alivaa raba nyeusi na juu nywele zilifungwa pamoja.
Alionekana kuwa huru katika uvaaji wake, hakuwa na urembo wa kuongeza maana alionekana kuwa asilia zaidi.
Akiwa ameshika mfuko alitembea kuelekea mlangoni. Derrick akiinuka na kuongeza mwendo nyuma yake alipokaribia, akafungua faili na kuangalia. Akilini kwake alilenga kuugonga ule mkono uliobeba mfuko. Na kwa mahesabu yake mguu wake wa kulia ulifaa kwa ajali hiyo. Kama alivyokusudia ndivyo ilivyokuwa.
Ghafla alimgonga kwa nyuma na kusababisha mfuko wake kuanguka kwa mbele huku faili iliyokuwa mkononi mwake akaiachia chini na kusababisha karatasi kuzagaa pale chini
"Ooooh samahani sana" alisema Derrick huku akiwahi kuokota ule mfuko.
"Hamna shida"alisema Aretha na kugeuka kumuangalia usoni Derrick kisha akaangalia karatasi zilizoanguka chini. Akainama haraka kuokota kama ambavyo Derrick alifanya.
Baada ya kumaliza, Derrick akamkabidhi mfuko kisha akasema
"Samahani sana nilikuwa naangalia karatasi na sikukuona mbele." hakuwa na namna nyingine ya kusema zaidi ya kuongopa
"Usijali, hata mimi nilikuwa na earphone sikusikia hatua zako nyuma yangu" alijibu Aretha kama kawaida usoni akionesha aibu kumuangalia usoni
"Naitwa Derrick, mwenzangu" alinyoosha mkono kumuelekea Aretha ambaye aliuangalia kisha akaupokea na haraka akauachia
"Aretha"
Akaanza kuondoka, Derrick akatumia nafasi hiyo
"Unaelekea wapi nikusogeze kwa usumbufu mdogo niliokupa" akaongeza na tabasamu lake ambalo humfanya mtu ashindwe kukataa.
Aretha alimwangalia usoni mara moja na kushusha macho yake akatabasamu,
"Naenda Moon Street" alijibu kwa sauti ya chini
"Great twende sasa" alijibu Derrick na kwa haraka akachukua mfuko mkononi kwa Aretha. Wakaondoka.